26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Utulivu watawala uchaguzi Zanzibar

IMG_4639NORA DAMIAN NA SARAH MOSSI, ZANZIBAR

UPIGAJI kura za uchaguzi mkuu jana umefanyika kwa amani Visiwani Zanzibar, licha ya kuwapo kwa kasoro ndogondogo.

Vituo vingi vya kupigia kura vilianza shughuli zake saa moja asubuhi na wananchi walijitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwachagua viongozi wanaowapenda.

Jana MTANZANIA ilitembelea vituo vya Shule ya Msingi Bungi, Jimbo la Tunguu, Mkoa wa Mjini Magharibi, Shule ya Maandalizi ya Msingi Kiembesamaki, Mtoni Kidatu na Malindi na kushuhudia wananchi wengi wakiwa kwenye mistari wakisubiri kupiga kura.

 

  1. SHEIN

Wakati hali ikiwa hivyo, Rais anayemaliza muda wake, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye anatetea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipiga kura katika kituo kilichoko Shule ya Msingi Bungi, ambapo aliwasili kituoni hapo saa moja asubuhi.

Baada ya kuwasili kituoni hapo, Dk. Shein alifanya taratibu zote za kupiga kura kama walivyokuwa wakifanya wapiga kura wengine.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupiga kura, Dk. Shein alisema maandalizi yalikuwa vizuri na kwamba ana matumaini makubwa ya kushinda kwa kishindo kuliko ilivyokuwa mwaka 2010.

“Nimejipigia kura mwenyewe na wagombea wengine wote waliowekwa na CCM, wananchi wategemee mambo yatakuwa mazuri.

“Tume iko huru kwa mujibu wa Katiba, sina mamlaka ya kuwaingilia, hivyo watakaoshindwa wakubali matokeo ili tuijenge nchi yetu na si kuleta mtafaruku nchini,” alisema Dk. Shein.

 

MAALIM SEIF

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayemaliza muda wake ambaye anagombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alipiga kura katika kituo cha Mtoni Kidatu, kilichoko katika eneo la Galagala, saa 3:57 asubuhi.

Kama alivyofanya Dk. Shein, Hamad naye alizungumza na waandishi wa habari na kusema aliridhishwa na maandalizi ya uchaguzi huo.

“Sina wasiwasi, kama uchaguzi utaendeshwa kwa haki na huru na wa wazi, nitakuwa mshindi,” alisema Hamad.

Kuhusu suala la kupokea matokeo, alisema itategemea kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki, ingawa CUF wanaamini watashinda kwa asilimia 72.

 

MGOMBEA ADA-TADEA

 MGOMBEA Urais kupitia chama cha ADA-TADEA, Juma Ali Khatib, alipiga kura katika kituo kilichoko Shule ya Maandalizi ya Msingi, Kiembesamaki A na kuahidi kukubali matokeo baada ya kutangazwa mshindi.

“Unaposhindana siku zote kuna kushinda na kushindwa, nisiposhinda nitakubali matokeo, nawaomba na wagombea wengine wakubali matokeo ili tuweke masilahi ya Taifa letu mbele,” alisema Khatib.

 

SAMIA HASSAN

 Mgombea Mwenza wa Urais wa kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, alipiga kura katika kituo cha Mombasa kilichoko eneo la Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Baada ya kupiga kura, Samia aliwaambia waandishi wa habari kwamba CCM kitashinda kwa kishindo kutokana na mwitikio wa wananchi ulioonekana tangu wakati wa kampeni.

“Nitapokea matokeo ya kushinda na haitakuwa vinginevyo kwa sababu chama chetu kina sera nzuri na kina uzoefu wa kutosha,” alisema Samia.

DUNI HAJI

Mgombea Mwenza wa urais wa Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Juma Duni Haji, alipiga kura katika Kituo cha Malindi kilichoko eneo la Hoteli ya Bwawani na kusema yuko tayari kukubali matokeo ikiwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

“Kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki, tutakuwa wa kwanza kuwapongeza watakaoshinda, lakini si kwa kulazimisha,” alisema Duni.

 

  1. BILAL

Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipiga kura katika eneo la Kiembesamaki na kusema wanategemea uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

“Walinzi wote wa kura wako kwenye vyumba vya kupigia kura, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi uchaguzi utakuwa huru na wa haki,” alisema Dk. Bilal.

WALEMAVU

 Katika baadhi ya vituo ambako MTANZANIA lilitembelea, lilishuhudia watu wenye ulemavu wakiwa wameongozana na ndugu zao kuletwa vituoni na wengine walifika wenyewe na kusaidiwa na makarani waongozaji wa wapiga kura.

Abdulkhadir Amir ambaye ni mlemavu asiyeona, alipigia kura katika Kituo cha Malindi kwa kusaidiwa na ndugu yake.

“Kwa upande wa kuchagua rais wa Zanzibar, wawakilishi na diwani ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) iliweka vifaa saidizi, lakini katika upande wa kuchagua rais wa muungano na mbunge, hakukuwa na vifaa hivyo, nimelazimika kusaidiwa,” alisema Amir.

 

KASORO MBALIMBALI

 Katika kituo cha kupigia kura kilichoko Kijitoupele, karatasi za kumchagua mwakilishi zilichelewa kufika, hatua iliyosababisha wananchi kupiga kura za kuwachagua rais wa Zanzibar, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Pamoja na hayo, baadhi ya wananchi walilalamikia kutoona majina yao, licha ya kuwa na vitambulisho vya kupigia kura.

Mmoja wa wananchi wa Mbweni Kanisani, Winfrida Gabriel Busumabu, alifika katika Kituo cha kupigia kura kilichoko Kiembesamaki, lakini alishindwa kupiga kura kutokana na jina lake kutokuwapo katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Katika eneo la Tomondo, baadhi ya mawakala wa wagombea wa CCM walikataliwa na mawakala wa vyama vya upinzani kutokana na vitambulisho vyao kutokuwa na picha. Hatua hiyo ilisababisha mawakala hao kutolewa nje.

Naye mgombea wa uwakilishi katika Jimbo la Kiembesamaki kupitia CUF, Mohamed Nassoro Mohamed, alilalamikia kuchelewa kwa vitambulisho vya baadhi ya mawakala huku vingine vikiwa havina picha.

“Tulipeleka majina wiki mbili zilizopita, lakini tunashangaa leo baadhi ya mawakala vitambulisho vyao havina picha na wengine hawajapata kabisa,” alilalamika Mohamed.

 

UTULIVU

 Katika maeneo mbalimbali ya Unguja, hali ilikuwa tulivu, lakini baadhi ya shughuli za kijamii zilikuwa zimesimama, kwani maduka mengi yalikuwa yamefungwa, hasa katika Soko Kuu la Darajani maarufu kama Marikiti na Mwanakwerekwe.

Pia baadhi ya wananchi walilalamikia kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, hasa vyakula ambapo viazi mbatata vilipanda kutoka Sh 800 hadi Sh 3,000 kwa kilo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles