27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

UTT AMIS YAJA NA SULUHISHO LA ADA

Na PATRICIA KIMELEMETADAR -ES SALAAM


GHARAMA zinazohusiana na elimu wakati mwingine zinaweza kuwa kikwazo na kuleta matokeo hasi katika maendeleo ya taaluma ya mwanafunzi husika.

Hii ni kutokana na kuwapo shule ama vyuo vinavyotoza ada kubwa na kusababisha wazazi wengi kushindwa kumudu kulipa.

Ziko familia ambazo zimeshindwa kupeleka watoto katika shule za sekondari au vyuo kwa sababu ya kushindwa kulipa ada na kukimu mahitaji mengine.

UTT AMIS ni miongoni mwa mifuko inayotatua changamoto za kielimu hasa katika suala la ulipaji wa ada kwa wanafunzi.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mkurugenzi wa Masoko wa mfuko huo, Daudi Mbaga, anasema kwamba mfuko huo una mipango miwili mikubwa ambayo ni mpango wa ada za shule na mpango wa pili ni mtaji kwa mwanao.

Anasema ili mzazi aweze kuchangia kupitia mfuko huo, anapaswa kuweka Sh 10,000 kwa kima cha chini na kwamba hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu.

Anasema mpango huo ulianzishwa mwaka 2008 kwa kima cha chini cha kipande cha kuanzia Sh 100 kwa kipindi hiki na tayari kipo takriban ya Sh 295.

“Tunawashauri Watanzania kuwekeza vipande vya mfuko wa UTT AMIS ili waweze kuhifadhi fedha za ada za watoto wao, kwani kima cha chini cha mfuko huu ni Sh 10,000 kiwango ambacho kila mmoja anaweza kununua kipande,”anasema Mbaga.

Anasema mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, wanaelimisha wazazi ili waweze kujiunga na mfuko huo ambao utawasaidia kuweka ada za watoto wao na kuondoa usumbufu wakati wa kufungua au kufunga shule.

Anasema mfuko huo una uwekezaji mwingine wa aina mbalimbali ukiwamo uwekezaji wa pamoja ambao na wenyewe umegawanyika katika aina mbili.

Anasema uwekezaji wa pamoja ni ule wa anuai yaani athari za uwekezaji zimetawanywa ambao unawekeza katika masoko ya mitaji na masoko ya fedha.

Anasema katika uwekezaji huo wa pamoja, mfuko mmoja unaweza kuwekeza sehemu mbalimbali ili kutawanya athari za uwekezaji mfano wa mfuko huu ni mfuko wa Umoja wa UTT AMIS.

“Mfuko wa Umoja wa UTT AMIS ni ule ambao athari za uwekezaji zimetawanywa, hali inayomfanya mwekezaji kuhifadhi fedha zake bila mashaka yoyote,”anasema.

Anasema katika mfuko huo pia, unaweza kuwekeza fedha zako bila ya kuweka kwenye soko la hisa.

Anasema mara nyingi hisa husaidia kipande cha uwekezaji kupanda au kushuka japo ndizo humpatia faida zaidi mwekezaji.

Anasema lakini pia, kuna faida nyingine kubwa katika uwekezaji wa mfuko huo ambapo mwekezaji kila siku anajua uwekezaji wake uko kiasi gani, umekua au umepungua.

Anasema kuwa katika mfuko huo, thamani ya kipande lazima ichapishwe kila siku kwenye magazeti na kwenye tovuti ya UTT AMIS hivyo uwekezaji huu unazingatia uwazi.

“Katika mfuko huu tumeweka uwazi wa hali ya juu, kila siku lazima tuchapishe kwenye gazeti thamani ya kipande ili mwekezaji aweze kujua kama imepanda au imeshuka,”anasema.

Anasema mfuko mingine ni ule unaoitwa ukwasi ambao huwasaidia wawekezaji kuweka fedha zao bila ya kuwa na hofu ya kupoteza endapo itatokea jambo lolote hatarishi.

“Baadhi ya wawekezaji wenye hofu ya kupoteza fedha zao pale wanapoona hali hatarishi yoyote, tunawashauri kujiunga kwenye mfuko wa ukwasi ili waweze kuweka fedha zao,” anasema.

Anasema mfuko huo ulianza mwaka 2013 kwa thamani ya Sh 100 kwa kipande lakini hadi sasa thamani hiyo imepanda na kufikia karibu ya Sh 170.

Anasema katika mfuko huu, mwekezaji huweka fedha zake katika akaunti za muda maalumu, hati fungani na katika namna zingine za kibiashara na taasisi zingine za fedha hususan benki.

Anasema hati fungani ni mikopo kwa serikali na makampuni ya muda mrefu na husimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Anasema katika mfuko huo, wananchi wenye uwezo wanaweza kuwekeza fedha zao ili waweze kupata faida na kunufaika na fedha zao.

“Tunatarajia kuanzisha mifuko ya hati fungani siku zijazo, lengo ni kuendelea kuhamasisha wananchi ili waweze kujiunga na mifuko yetu kwa ajili ya kupata faida kupitia hati fungani za muda mrefu tu, “anasema.

Akizungumzia faida zinazopatikana kwenye mfuko huo wa hati fungani, Mbaga anasema kuwa mwananchi anawekeza katika hati fungani zenye riba mbalimbali na za muda tofauti.

Anasema hati fungani nyingine unaweza kupata kwa bei nzuri zaidi na zingine kwa bei ya wastani kulingana na soko na cha muhimu zaidi ni kuwa unaweza ukakadiria kile utakachopata kitu ambacho si rahisi kupata kwenye hisa.

Anasema mtu anaweza kuwekeza faida anayopata tofauti na uwekezaji wa hati fungani moja bila kupitia uwekezaji wa pamoja.

Anasema ni rahisi kuuza hati fungani yako ikiwa ndani ya uwekezaji wa pamoja kuliko ikiwa imesimama peke yake.

Anasema changamoto iliyopo katika mfuko huo ni pale ambapo upo kwenye mfuko wa uwekezaji wa pamoja kupitia hati fungani hautakuwa na muda maalumu wa uwekezaji wako kuiva.

Anasema kutokana na hali hiyo, faida utakayokuwa unaipata itakuwa inabadilika mara kwa mara.

Anasema mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, mfuko huo unaendelea kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi ili waweze kujiunga nayo, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupata faida.

“Ikiwa wananchi watajiunga na mifuko yetu, wanaweza kupata faida kulingana na uwekezaji wao, hivyo basi tunawashauri waje ili tuweze kuwaunganisha,”anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles