27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UTOMBO KUTOKA NJE: TATIZO LINALOWAKUMBA ZAIDI WATOTO WANAOHARA

Mchoro unaonesha utumbo wa mwanadamu

 

 

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MWAKA 2015, Mariam John alijifungua salama mtoto wake wa pili Elizabeth Peter (si majina yao halisi), huko mkoani Kigoma ambako ndipo yalipo makazi yao.

Maendeleo ya afya ya Elizabeth yalikuwa yanaridhisha kila walipohudhuria kliniki lakini miaka miwili baada ya kuzaliwa hali ilianza kubadilika ghafla.

Mariam anasema siku moja alipokuwa akimnawisha sehemu ya haja kubwa mtoto wake huyo, baada ya kumaliza kujisaidia alishangaa kugusa kinyama ambacho kilijitokeza kwa nje.

“Awali sikutilia maanani suala hilo, nikadhani kwamba labda kimejitokeza na kitarudi baada ya muda fulani lakini kadri muda ulivyosonga mbele hali ilizidi kuwa mbaya,” anasema.

Anasema kinyama hicho kiliendelea kuongezeka urefu kutoka nje hali ambayo ilimfanya awe na wasiwasi mkubwa juu ya afya ya mtoto wake.

Anasema aliamua kumjulisha mumewe na ndugu zake wa karibu juu ya hali hiyo.

“Kinyama hicho kilikuwa kikijitokeza kila alipokuwa akijisaidia haja kubwa, ikafika hatua siku moja nikaona utumbo umetoka nje kabisa katika sehemu hiyo,” anasema.

Anasema wapo watu ambao walimshauri kumpeleka hospitalini mtoto wake ili akapewe matibabu lakini wengine walimshauri ampeleke kwa waganga wa kienyeji.

“Walionishauri nimpeleke kwa mganga wa kienyeji walikuwa wengi, walinieleza kwamba hali hiyo si ya kawaida na kwamba mwanangu amerogwa, hivyo iwapo nitaendelea kukaa naye bila kumpeleka huko atapoteza maisha wakati wowote,” anasema.

Anasema hata hivyo, baadhi ya ndugu zake walimweleza kwamba ampeleke mapema hospitalini ili afanyiwe uchunguzi wa kina kujua anasumbuliwa na ugonjwa gani.

Safari ya matibabu

Mariam anasema alimpeleka katika zahanati moja iliyopo mkoani humo ambako hata hivyo baada ya kumfanyia vipimo hawakugundua tatizo lililokuwa likimsumbua.

“Waliniandikia dawa ambazo nilimpatia mwanangu lakini hakupona wala hakupata nafuu, kila siku hali ilizidi kuwa mbaya,” anasema.

Anasema aliamua kumshirikisha suala hilo rafiki yake ambaye anaishi huko eneo la Mburahati jijini Dar es Salaam.

“Nilibaki njia panda, sikujua nifanye nini ili kumsaidia mwanangu, rafiki yangu alinishauri nijitahidi nifike Dar es Salaam, kwamba tatizo hilo linatibika kabisa,” anasema.

Anasema mumewe alijitahidi kutafuta nauli, fedha za kujikimu na za matibabu, safari ikaanza kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam.

“Tulifika salama, namshukuru rafiki yangu alinipokea na kunikaribisha nyumbani kwake, ilikuwa mwishoni mwa Aprili, mwaka huu, nikaanza matibabu katika Hospitali ya Amana,” anasema.

Anasema madaktari wa hospitali hiyo baada ya kumfanyia vipimo mtoto wake walimweleza kuwa anahitaji huduma ya kibingwa ndipo wakampatia rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Tayari ametibiwa

Mariam anasema mwanawe amefanyiwa upasuaji wa kurudisha ndani sehemu ya utumbo uliotoka nje.

“Nawashauri wazazi na walezi wanapoona mabadiliko yoyote ya kiafya katika miili ya watoto wao wawapeleke hospitali na si kwa waganga wa kienyeji, huko watapoteza muda na watoto wao watazidi kuugua na kuteseka kila siku,” anashauri.

Elizabeth alipatwa na nini?

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Muhimbili, Zaituni  Bokhary anasema Elizabeth alipata tatizo linalojulikana kitaalamu Rectal Prolapse.

“Hii ni hali ambayo sehemu ya utumbo mkubwa iitwayo ‘rectum’ hutoka nje ya mwili katika njia ya haja kubwa. Hakuna sababu maalumu ambayo wataalamu tunaweza kusema moja kwa moja, kwamba tatizo limesababishwa ama na bakteria au wadudu. Lakini kuna viashiria au visababishi kadhaa ambavyo vinahusishwa kusababisha tatizo hilo kutokea,” anasema.

Visababishi vyenyewe

Dk. Bokhary anasema hali hiyo inaweza kusababishwa na kuharisha muda mrefu hali ambayo huchangia mtoto kupungua uzito na kukonda mwili.

“Hii ni sababu kuu, kuharisha muda mrefu husababisha mtoto kukonda hadi ile misuli ya haja kubwa hushindwa kukaza vizuri kama inavyotakiwa hali hiyo huifanya ile ‘rectum’ kutoka nje,” anafafanua.

Anasema kiashiria kingine cha awali ambacho mzazi anaweza kukiona iwapo mtoto anakabiliwa na tatizo hilo ni kupata viotea (vinyama) ambavyo hutoka katika njia ya haja kubwa.

“Vinyama hivyo hutoka nje ya mwili katika sehemu ya haja kubwa. Wakati mwingine tatizo huweza kujitokeza iwapo kuna maambukizi katika utumbo mkubwa,” anasema.

Daktari huyo anasema iwapo mtoto aliwahi kufanyiwa upasuaji wa utumbo mkubwa, inaweza kusababisha akapatwa tatizo hilo kwa namna moja au nyingine.

“Lakini wengine wanapata tatizo hili, ikiwa wamezaliwa na hawana chembe chembe maalumu ambazo kazi yake kuu ni kusukuma choo nje ya mwili, sasa kwa kuwa hajazaliwa na chembe chembe hizo mtoto huyo anaweza utumbo wake ukatoka nje kwa sababu ya kutumia nguvu kusukuma choo,” anabainisha.

Anasema kisababishi kingine kinaweza kuwa uvimbe unaotokea katika njia ya haja kubwa.

“Mtoto anaweza kupata uvimbe ambao unaweza ukawa ni saratani au si saratani, lazima afanyiwe uchunguzi mapema ili kumsaidia kwani akikaa nao muda mrefu ni hatari,” anasema.

Anasema kisababishi kingine ambacho kinadhaniwa kuwa moja wapo ya sababu zinazochangia mtoto kupata tatizo hilo ni maambukizi ya virusi viitwavyo kitaalamu Rota Virus.

“Virusi hawa hula baadhi ya seli zilizopo kwenye utumbo mkubwa (wanazishambulia) matokeo yake utumbo unakuwa unaingiliana, utumbo wa binadamu umegawanyika katika sehemu nne na kila mmoja haipaswi kuingiliana na nyingine, zikiingiliana kutokana na kushambuliwa na virusi hivi husababisha tatizo,” anasema.

Madaktari wakifanya upasuaji kwa njia ya matundu
Hatua za tatizo

Daktari huyo anasema ugonjwa huo hupitia hatua kuu nne na kwamba iwapo mzazi atawahi kumfikisha mwanawe hospitalini ni rahisi kumtibu akiwa katika hatua ya awali.

“Katika hatua ya kwanza mzazi au mlezi ataona ule utumbo unatoka na kurudi ndani wenyewe, sasa anapomleta hospitali mtoto tunamfanyia uchunguzi kujua nini kinasababisha hali hiyo, tunatibu chanzo kwa kutumia dawa maalumu na wala anakuwa hahitaji kufanyiwa upasuaji wowote,” anasema.

Anataja hatua ya pili ya tatizo kuwa utumbo unapotoka nje hushindwa kurudi ndani bila kusaidiwa kuurudisha.

“Yaani mtoto akijisaidia utumbo unatoka nje katika njia yake ya haja kubwa na hauwezi kurudi ndani hadi mzazi asaidie kuurudisha, bado katika hatua hii tunaweza kumtibu mtoto bila kumfanyia upasuaji, tunamchunguza na kutibu chanzo cha tatizo,” anafafanua.

Dk. Bokhary anasema hatua ya tatu huashiria kwamba tatizo linazidi kuwa kubwa na kwamba utumbo wa mtoto huweza kujitokeza nje hata kama hakujisaidia.

“Hata akiwa amekaa chini unakuta utumbo wake umejitokeza wenyewe na wala hajajisaidia haja kubwa na lazima umsaidie kuurudisha ndani,” anasema.

Anasema katika hatua ya nne utumbo unapotoka nje huweza kukaa wiki au mwezi kwani hata unaporudishwa ndani hutoka tena wenyewe.

“Unaona wazi kwamba katika hatua ya kwanza na ya pili ni rahisi kutibu tatizo kwa kutumia dawa maalumu baada ya kumfanyia uchunguzi wa kina mtoto husika lakini ikifika hatua ya tatu na nne tatizo linakuwa limeongezeka hivyo inakuwa lazima tumfanyie upasuaji,” anasema Daktari huyo.

Upasuaji unavyofanyika

Anasema kuna njia mbili za upasuaji ambazo huzitumia kumtibu mtoto husika ambazo ni njia ya matundu (Laporascopic-Rectal Sigmoidopexy na ile ya kufungua sehemu ndogo ya tumbo (Open Rectal- Sigmoidopexy.

“Lakini tunaweza tusifungue sehemu ya tumbo badala yake tukashona pale kwenye misuli (iliyopo kwenye sehemu ya haja kubwa) kuikaza kwa sababu inakuwa imelegea ndiyo maana utumbo hutoka nje.

 “Au tunafungua kidogo sehemu ya tumbo katika upande wa kushoto, tunashona ule utumbo kwa ndani kidogo kwa kutumia uzi maalumu ambao kwa kawaida huwa mgumu.

“Huwa tunashona kwa utaalamu wa hali ya juu, hatugusi hata kidogo kwenye misuli hivyo mgonjwa huwa si rahisi kuhisi maumivu makali, maumivu hutokea pale misuli inapoguswa,” anafafanua.

Anasema upasuaji kwa njia ya matundu ni mzuri zaidi kuliko ule wa kufungua sehemu ya tumbo.

“Kwa njia ya matundu mgonjwa anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani hata kesho yake baada ya kufanyiwa upasuaji, kwa sababu sehemu ndogo ya mwili huwa imefunuliwa kutibu tatizo, tofauti na ule wa kupasua lazima akae wodini kwa uangalizi kwa siku kadhaa,” anasema.

Hali ilivyo Muhimbili

Daktari huyo anasema watoto wengi wanaowapokea wamepata tatizo hilo kutokana na maambukizi ya kuharisha.

“Wengi hufikishwa general pediatric (kwa madaktari bingwa wa watoto) wazazi wanakuwa hawajajua watoto wao wanasumbuliwa na nini na kwanini utumbo unatoka nje.

“Wale wa Pediatric wakiona ni tatizo hilo, ndipo wanawahamishia kwenye idara yetu ya upasuaji, kwa mwezi tunaona watoto kati ya wanne hadi watano wanaosumbuliwa na tatizo hilo,” anasema.

Kwanini kuharisha sababu kuu?

Anafafanua kwamba watoto wengi ni rahisi kupatwa na hali hiyo hasa wale wanaoishi katika mazingira machafu.

“Inaaminika kwamba ukipata tatizo la kuharisha maana yake umekula kinyesi, sasa watoto wanapocheza hushika vitu vingi, na wengi hupenda kuweka vidole mdomoni.

“Sasa mazingira yanapokuwa machafu maana yake ni kwamba anakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi, ni vema mazingira yakasafishwa kila wakati yawe rafiki kwa watoto ili kuwaepusha,” anasema.

Changamoto

Daktari huyo anasema changamoto kubwa ambayo huweza kujitokeza baada ya upasuaji kumtibu mtoto mwenye tatizo ni uzi kumsababishia maambukizi.

“Anaweza kupata ‘infection’ hasa anapofanyiwa upasuaji wa kufunua sehemu ya tumbo, ndiyo maana huwa tunalazimika kuwalaza wodini ili tuwape uangalizi wa karibu hadi kidonda kinapofunga, lakini sasa hivi Muhimbili tumeanza kufanya upasuaji kwa njia ya matundu ambao tunaona ni salama zaidi,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles