26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Uteuzi Waziri Mambo ya Nje Uingereza waishtua dunia

Theresa May
Theresa May

LONDON, UINGEREZA

WAZIRI Mkuu mpya wa Uingereza, Theresa May, juzi usiku alitangaza baraza lake jipya la mawaziri, huku akimteua meya wa zamani wa London, Boris Johnson, kuwa waziri wake wa mambo ya nje, uamuzi uliowaacha wengi kinywa wazi.

May alianza rasmi wadhifa wake mpya kama waziri mkuu wa 76 wa Uingereza, baada ya David Cameron kukabidhi barua ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth II kufuatia kushindwa kujiondoa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya (EU).

May, ambaye pia anakuwa waziri mkuu wa 13 kuhudumu chini ya Malkia Elizabeth II na mwanamke wa pili Uingereza kushika wadhifa huo, aliwatema vigogo kadhaa akiwamo Kansela George Osborne.

Mshtuko wa kumteua Johnson kuwa mwanadiplomasia namba moja wa Uingereza, na pia kulisimamia Shirika la Ujasusi la MI6, unatokana na ukweli kuwa haivi na viongozi wengi duniani na huipinga wazi wazi EU.

Wakosoaji wanasema kumteua kinara aliyechangia Uingereza kujitoa EU kuwa taswira ya diplomasia ya taifa hilo, kunalifanya taifa hilo kuwa ‘kituko’.

Aprili mwaka huu, Johnson alimshambulia Rais wa Marekani, Barack Obama kuwa ni nusu Mkenya ambaye anatumia chuki za kale za kikoloni dhidi ya Uingereza kwa kudai ikijitoa EU kutalifanya taifa hilo ‘kupanga foleni’ katika masuala ya kimataifa.

Akihojiwa kuhusu hilo juzi, Johnson aligoma kuomba radhi, huku akimrushia kijembe Obama kuwa atakuwa ‘katika foleni ya kusubiri’ zamu ya mazungumzo.

Johnson pia Mei mwaka huu alimshambulia kiongozi wa Uturuki, Recep Erdogan kuwa amekuwa akifanya mapenzi na mbuzi.

Usiku wa juzi msemaji wa Obama kwa Masuala ya Mambo ya Nje, Mark Toner hakuweza kujizuia kucheka wakati alipojulishwa waziri mpya wa mambo ya nje ni Boris Johnson, lakini alisisitiza Marekani itafanya naye kazi kwa karibu.

Aidha Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, alimkaribisha May kwa mazungumzo, lakini hakuwa tayari kumzungumzia Johnson.

Uteuzi wa Johnson unakuja wiki chache tu baada ya harakati zake za kuwania uwaziri mkuu kutoswa na mshirika wake aliyekuwa Waziri wa Sheria, Michael Gove, ambaye alitangaza kuingia mwenyewe katika kinyang’anyiro hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles