31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

UTEUZI WA TILLERSON UWAZIRI MAMBO YA NJE MAREKANI ZAWADI KWA URUSI?

wakisalimianaUTEUZI wa Rex Tillerson, ofisa mtendaji mkuu wa moja ya kampuni kubwa kabisa ya nishati duniani, ExxonMobil kuwa waziri wa mambo ya nje Marekani ulileta mshtuko kwa wengi.

Kubwa ni kwa sababu ya utumishi wake wa muda mrefu katika kampuni kubwa ya nishati duniani na urafiki wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye kwa miaka mingi anahesabiwa kuwa ‘adui’ wa Magharibi.

Kwamba kutokana na namna taasisi za kijasusi za Marekani kuamini kuwa Urusi ilishawishi matokeo ya uchaguzi wa urais wa Marekani ili kumsaidia Donald Trump kushinda rais, urafiki huo unatia shaka na utampa wakati mgumu wakati jina lake litakapowasilishwa mbele ya Seneta ili kuthibitishwa au kukataliwa uteuzi huo.

Bila kujali wasiwasi wa maseneta wa Marekani, Trump alienda kutangaza kupitia akaunti yake ya Twitter kuwa Tillerson ni chaguo lake la uanadiplomasia namba moja wa Marekani.

Alimsifu Tillerson kuwa mmoja wa viongozi wakubwa kabisa wa kibiashara duniani.

Licha ya uswahiba huo huku kukiwa na maelewano chanya baina ya Putin na Trump yaliyojengwa katika msingi wa kusifiana pengine kinafiki tangu wakati wa kampeni za urais, uteuzi huo unaashiria azma ya Trump kuiongoza Marekani kibiashara zaidi.

Urafiki baina ya kachero wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Urusi (KGB) na Tillerson – wote wakiwa na umri wa miaka 64 sasa unarudi nyuma mwishoni mwa miaka ya 1990 wakati Tillerson alipoeneza shughuli za Exxon nchini Urusi.

Kipindi hicho Putin alikuwa mwanasiasa mchanga bado, ambaye ndiyo alikuwa ametokea kuteuliwa uwaziri mkuu katika Serikali ya Rais Boris Yeltsin.

Mwaka 2013, Putin alimtuza Tillerson medali ya urafiki, moja ya tuzo za juu kabisa za Urusi maalumu kwa wageni waliochangia uhusiano mwema na taifa hilo.

Mwaka mmoja kabla, Tillerson alisimamia dili la mkataba wa mabilioni ya dola lililolenga kuisaidia Moscow kufaidika vilivyo na utajiri wa mafuta katika ukanda wa Aktiki, dili ambalo hata hivyo lilifeli kutokana na vikwazo vya magharibi kwa taifa hilo.

Vikwazo hivyo vilitokana na hatua ya Urusi kulimega jimbo la Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014.

Tillerson pasipo kuficha hasira zake alivishambulia vikali vikwazo hivyo, ambavyo viliigharimu mabilioni ya dola kampuni yake.

Na sasa, wakati Tillerson akiwa mwanadiplomasia asiye na uzoefu na Putin mwanasiasa mzoefu, anayeongoza kwa mkono wa chuma, wakosoaji wa Kremlin wanashangaa iwapo uhusiano huu utaashiria ukurasa mpya wa namna Washington inavyoshughulika na Moscow.

Wadadisi wa mambo wa upinzani nchini Urusi wanahofia uteuzi huo utakuwa na manufaa kwa Putin na kwamba Tillerson anaonekana atakuwa kiungo muhimu katika kutengeneza mazingira mazuri zaidi kiongozi huyo mwenye hulka ya kibabe kujenga daraja la ushirika na Marekani hata Magharibi kwa ujumla wake.

Kitendo cha Urusi kuimega Crimea, kuwaunga mkono wanamgambo waliokuwa wakiendesha kampeni ya kujitenga mashariki mwa Ukraine na uungaji wake mkono Serikali ya Damascus nchini Urusi zilifanya uhusiano wake na Magharibi kurudi zama zile za Vita Baridi.

Lakini mwelekeo wa kizalendo, uhafidhina mambo leo na uwekezaji zaidi katika vitendo kuliko siasa unaofuatwa na Rais mteule Donald Trump unaonekana kukinzana na miaka mingi ya sera za Washington kuelekea Urusi na kimastaajabu sera zake zinaonekana kuoana na zile za Kremlin.

Sehemu kubwa ya utawala wake, Putin alitaka Magharibi kuichukulia Moscow kama mshirika aliye sawa bila kujali ukandamizaji wake wapinzani, ufisadi na ulimbikizaji wa sekta muhimu mikononi mwa mashirika ya serikali.

“Uongozi wa Urusi umeonesha kuweka mbele uzalendo katika sera zake za kigeni. Iwapo Marekani itachangia msingi ule ule wa sera, sidhani kama kutakuwa na matatizo yoyote baina yao,” alisikika Alexey Mukhin, mkuu wa taasisi ya taarifa za kisiasa mjini Moscow alisema.

Wakati wakosoaji wa Kremlin wakiwa na wasiwasi kuhusu uteuzi huo, wale wanaouunga mkono utawala huo wameushangilia na wanauombea upitishwe.

Miaka ya 1998-1999, Tillerson alitumikia kama makamu wa rais wa Exxon (kabla ya kampuni hiyo kuungana na Mobil) katika uendeshaji wa shughuli katika Bahari ya Caspian na Sakhalin, kisiwa kikubwa katika Pasifiki kilichopo kaskazni mwa Japan.

Lakini kushughulika na mamlaka za Urusi si kitu rahisi daima.

Aprili 2015, kampuni hiyo iliifikisha mahakamani Urusi katika Mahakama ya Usuluhishi ya Stockholm nchini Sweden ikidai ililipa zaidi ya kiwango halisi cha kodi kutokana na faida iliyopata katika mradi wa Sakhalin.

Lakini licha ya hayo, Tillerson alibakia kuwa mmoja wa watendaji wakuu wa kampuni kubwa za nishati duniani wanaowaminiwa pasipo shaka na Moscow.

Septemba 2005, Putin alikutana na Tillerson – akiwa Rais wa ExxonMobil kipindi hicho pamoja na aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu Lee Raymond, na mameneja waandamizi wa kampuni za Conoco-Phillips na Shevron-Texaco.

Kwanini? Miezi kadhaa kabla, mfanyabiashara mkubwa wa mafuta nchini humo, Mikhail Khodorkovsky alipewa adhabu ya kifungo cha miaka tisa jela kwa tuhuma za ufisadi ambazo zinaonekana kama kisasi cha Kremlin kwa msaada wake wa kifedha kwa wapinzani nchini humo.

Wawekezaji wa kigeni waliingiwa na hofu kuhusu kifungo hicho na mkutano huo ulilenga kuwahakikishia kwamba Moscow bado ni mshirika wao asiye na shaka.

Sehemu kubwa ya utajiri wa kampuni ya Khodorkovsky ukaenda kwa ile inayomilikiwa na serikali Rosneft, mshiriki mkuu wa ExxonMobil nchini Urusi.

Igor Sechin, mfasri wa zamani wa kireno na mshirika muhimu wa Putin, ambayo mara nyingi huelezwa kama mtu wa pili mwenye nguvu nchini Urusi anaiongoza Rosneft kwa sasa.

Igor pia ni rafiki mzuri wa Tillerson, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Urusi na Magharibi.

Mwaka 2011, ExxonMobil iliipiku kampuni kubwa ya mafuta ya Uingereza (BP) kusaidia Urusi kuzalisha hazina kubwa kabisa duniani ambayo haijavumbuliwa ya hydrocarbons.

Ukanda wake wa Aktiki una hazina ya mapipa zaidi ya bilioni 90 ya mafuta, ambayo bado haijavumbuliwa lakini ambayo kiufundi yanagundulika, ikiwa moja ya saba ya akiba ya mafuta ambayo haijavumbuliwa duniani.

Aidha ni pamoja na mabilioni ya mita ujazo za gesi ya asili kwa mujibu wa tathimini iliyofanywa na taasisi ya tafiti za Kijiolojia Marekani mwaka 2008.

Kwa mujibu wa maofisa wa Norway, Urusi ina asilimia 41 ya akiba ya mafuta na asilimia 70 ya gesi, lakini ina uhaba wa teknolojia na vifaa na mwanya huo ndio ulioiingiza ExxonMobil.

Mwaka 2011, Putin alisimamia utiaji saini wa kimkakati wa mkataba baina ya Rosneft na ExxonMobil kuchimba mafuta katika visima vya mafuta na gesi katika ukanda wa aktiki kwa kubadilishana miradi sita ya ExxonMobil nchini Marekani.

Katika hilo kampuni za Urusi hazikuonekana kuambulia kitu katika akiba za nishati zilizopo Marekani wakati Wamarekani kupitia Exxon Mobil walielekea kupata maendeleo mazuri Urusi.

Kwa mujibu wa Tillerson katika moja ya sherehe za utiaji saini, ExxonMobil ilipanga kutumia dola bilioni 3.2 kutafiti visima vya nshati ambavyo vingeipatia hazina ya mabilioni ya mapipa ya mafuta.

Uchimbaji ukaanza mwaka 2014, lakini mkataba huo sambamba na ubia mwingine magharibi mwa Siberia ukaingia doa kwa sababu ya vikwazo kuhusu  Crimea. ExxonMobil iliripotiwa kupoteza dola bilioni moja.

Tillerson aliwaambia wanahisa wa  ExxonMobil kuwa wamekuwa wakiwasisitiza watoa maamuzi kuangalia hasara inayemwangukia kwa vikwazo vyao kichaa.

Hata hivyo, vikwazo havikumzuia kuitembelea Urusi, kwani alifanya hivyo mara mbili akikutana na waziri wa nishati huku akihudhuria jukwaa la uchumi mjini St Petersburg, anakotoka Putin.

Hivyo, swali kubwa ni sasa je Tillerson atakuwa kiungo muhimu cha kuondoa vikwazo, ambavyo bila shaka vitainufaisha shughuli za sasa na baadaye za ExxonMobil nchini Urusi.?

Yeye na  Donald Trump wanaonekana wako kibiashara zaidi na hivyo wakijua sera zilizopelekea vikwazo hivyo za zama za Vita Baridi haziinufaishi Marekani, huenda wakawa tayari kuviondoa.

Lakini pia hilo litategemea maamuzi ya Bunge na Seneti na iwapo hawatabadili mawazo hapo baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles