27.4 C
Dar es Salaam
Thursday, December 9, 2021

Uteuzi wa Prof Ndulu kuwa mshauri wa uchumi wa Rais wa Afrika Kusini wachambuliwa

Leonard Mang’oha na mitandao

JOHANESBURG

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amemjumuisha Gavana Mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, kwenye orodha ya wajumbe 18 wa baraza jipya la washauri wake wa masuala ya uchumi.

Uteuzi huo ambao pia umewajumuisha wataalamu wa uchumi kutoka vyuo mbalimbali duniani ulifanyika juzi.

Profesa Ndulu na wenzake wanatarajiwa kuiongoza Afrika Kusini katika njia mpya na jumuishi ya maendeleo ya uchumi ambayo itaongeza ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya watu wa taifa hilo.

Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, alisema kwa wataalamu wa masuala ya uchumi kutoka nje si jambo la ajabu kwa sababu nchi hupata ushauri kutoka ndani na nje.

“Nchi hupata ushauri kutoka kwa wataalamu mbalimbali. Rais ameona amteue mtu kutoka nje ya nchi tena Tanzania, kwanza ni sifa kwake binafsi Profesa Ndulu kwa sababu tunamfahamu vizuri na ana uwezo huo.

“Lakini kwa maana hiyo ya uteuzi ni matakwa yake yeye binafsi pengine ameona anahitaji input kutoka nje achanganye na maoni kutoka ndani ya nchi yake inadasaidia. Siku zote unapopata external view (mtazamo kutoka nje) huwa ni afya kwa sababu kupata watu wa ndani kuna mambo mengi ila kupata watu wa n je ni afya kama atatumia hicho kichwa cha Profesa Ndulu vizuri,” alisema Profesa Ngowi.

Profesa Ndulu alihudumu kama Gavana wa BoT tangu Januari 2008, nafasi ambayo aliitumikia kwa miaka 10 hadi January mwaka jana aliporithiwa na Profesa Florence Luoga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Profesa Ndulu alianza kazi kama mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam mwanzoni mwa miaka ya 1980 kabla ya kujiunga na Benki ya Dunia kama Mchumi Kiongozi.

Mwaka 1997 alitunukiwa udaktari wa heshima kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kijamaa (ISS) mjini The Hague Uholanzi kama sehemu ya kutambua mchango yake katika kujenga wa uwezo na utafiti kuhusu Afrika.

Kutokana na shahada yake ya uzamivu katika uchumi aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Northwestern nchini Marekani, alifundisha na kuchapisha machapisho mbalimbali kuhusu ukuaji wa uchumi, marekebisho, utawala na biashara.

Profesa Ndulu amefahamika zaidi kutokana na kuhusika kwake katika kuanzisha na kuendeleza moja ya mitandao ya utafiti na mafunzo wenye ufanisi zaidi barani Afrika unaofahamika kama Jumuiya ya Utafiti wa Uchumi wa Afrika.

Baraza hilo huru na lisilokuwa la kisheria litaongozwa na Rais Ramaphosa mwenyewe. Wajumbe hao 18 kutoka ndani na nje ya Afrika Kusini, wameteuliwa kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitatu na hawatakuwa wakilipwa mshahara bali posho za kujikimu na usafiri kwa kipindi chote.

Ramaphosa alitangaza wazo la kuwa na baraza la ushauri wa kiuchumi kwa mara ya kwanza wakati wa hotuba yake kwa Taifa hilo miezi 18 iliyopita ambapo alisema baraza hillo litafanya kazi kwa ushirikiano na uthabiti katika utekelezaji wa sera za uchumi wa nchi hiyo.

Wakati akitangaza baraza hilo, Ramaphosa alisema baraza litakuwa kama kongamano litakalofanya majadiliano ya kina kuhusu muundo wa  ukuaji wa maendeleo ya kitaifa na kimataifa na litakutana katika robo mwaka ya kwanza kabla ya kuamua ratiba ya mikutano yake.

Mbali na Profesa Ndulu wajumbe wengine wa baraza hilo ni  Mtaalamu wa Biashara za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Profesa Mzukisi Qobo, Profesa Dani Rodrik ambaye ni mtaalamu wa Uchumi wa Kisiasa wa Kimataifa wa Chuo Kikuu cha Harvard Marekani.

Wengine ni Profesa wa Uchumi wa Ubunifu na Thamani ya Umma katika Chuo Kikuu cha London, Mariana Mazzucato, Mchumi Mkuu wa First National Bank, Mamello Matikinca –Ngwenya, Dk Renosi Mokate kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (SBL) ambaye pia alikuwa Naibu Gavana wa zamani wa Benki ya Hifadhi ya Afrika Kusini, Mtaalamu wa Uchumi kutoka chuo Kikuu cha Wits, Dk. Kenneth Creamer.

Pia wamo Profesa Alan Hirsch kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Mtaalamu wa Usimamizi wa Fedha katika Chuo Kikuu cha Stellenbosch, Profesa, Tania Ajam, Mchumi wa miundombinu na udhibiti, Dk Grové Steyn, Mchumi wa Kilimo na Mkuu wa Utafiti wa kilimo katika Sekta ya Biashara ya Kilimo ya Afrika Kusini, Wandile Sihlobo,  Mchumi Mkuu wa zamani wa Tume ya Ushindani na msomi wa sasa katika Chuo Kikuu cha Wits, Dk. Liberty Mncube.
 
Profesa katika Idara ya Uchumi na Uchumi katika Chuo Kikuu cha Johannesburg, Fiona Tregenna,  Profesa wa Uchumi na Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti wa Sera ya Maendeleo Chuo Kikuu cha Cape Town, Haroon Bhorat, Mchumi wa Maendeleo na Meneja wa Haki wa Uchumi wa zamani Oxfam Afrika Kusini,  Ayabonga Cawe.
 
Wengine ni Mchambuzi wa zamani wa Sera Kuu katika Uratibu na Huduma ya Ushauri wa Rais na Mkurugenzi Mwanzilishi wa Taasisi ya Uongozi ya Afrika ya Thabo Mbeki katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, Profesa Vusi Gumede, Mchumi wa Masuala ya Fedha, Dk Thabi Leoka na Mchumi na Mkuu wa Kitivo cha Biashara, Sheria na Usimamizi katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Profofesa Imraan Valodia.
mwisho
- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,672FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles