27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

UTEUZI WA BALOZI OMBENI SEFUE APRM UTUAMSHE

HIVI karibuni tumepokea taarifa kuwa  Balozi Ombeni Sifue amechaguliwa kuwa mmojawapo  katika jopo la watu mashuhuri  katika Mfumo wa Afrika wa kukaguana uitwao 'African Peer Review Mechanism'[APRM] kwa lugha ya Kiingereza.

Hii tunaona ni fursa nzuri sana kuwa mmoja kati ya Watanzania ameingia katika jopo hilo muhimu.Tunapenda kumpongeza sana kwa  kuonekana  kuwa anafaa kuwapo katika mfumo huu. Jopo hili  alilochaguliwa kuwapo ni sehemu ya  mfumo huo wa kukaguana   wa nchi za kiafrika (APRM) ambao ulianzishwa  mwaka 2003 na kamati ya wakuu wa nchi za Kiafrika   ya mpango wao unaojulikana kama Muungano (Ubia) Mpya kwa ajili ya Afrika (New Partnership forAfrica (NEPAP).  Mfumo au mpango huu wa NEPAD na hatimaye APRM vilianzishwa kutokana na uhitaji wa wazi ulioonekana barani Afrika wa kushughulikia hali dhaifu ya mpito kuelekea demokrasia ya kweli pamoja na uchumi uliooneka kutokukua na kuzorota  kwa ujumla.

Kwa Balozi Ombeni Sefue  ambaye ni  Mtanzanaia mwenzetu kuwa sehemu katika  mfumo huu inatupa nafasi  ya kujikumbusha nia na madhumuni ya mfumo huu na umuhimu wake kwetu kama taifa na kama  nchi mojawapo katika nchi za  Bara  la Afrika ambayo imewahi kuutumia mfumo huu mapema ulipoanza. APRM ni chombo  cha kujifuatilia kibinafsi kama nchi na kujiunga ni kwa hiari  ya nchi husika. 

Uwepo wa APRM ni kwa madhumuni  ya kuhimiza uwepo wa sera, maadili, vipimo na utamaduni wa utawala wa  kisiasa na kiuchumi utakaohakikisha  utulivu wa kisiasa, muunganiko wa kikanda  na wa bara zima la Afrika katika ukuaji wa uchumi  endelevu. Nchi ikiamua au kukubali kujiunga na mfumo huu wa APRM inakuwa imekubali kwa hiari yake yenyewe kujitazamisha  inavyotekeleza makubaliano ya kiutawala ya Afrika na kimataifa. Nchi hupimwa kwa kutumia  maeneo manne ambayo ni  Utawala wa Kidemokrasia na kisiasa; uUtawala wa Kiuchumi; Utawala wa kibishara na maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii.

Katika mfumo huu maeneo yanayokaguliwa ni Serikali, mahakama, bunge, sekta binafsi , mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari. Ukaguzi wa kwanza kwa nchi mwanachama hufanyika  miezi 18 tangu nchi ijiunge katika mfumo au mpango huu. Baada ya hapo ukaguzi huwa katika miaka miwili hadi minne baadaye na kuendelea.

Hata hivyo nchi husika huweza kuomba kufanyiwa ukaguzi katika nyakati tofauti na zile zilizoelekezwa iwapo yenyewe inaona inafaa. Pia nchi nyingine mwanachama huweza kutaka ukaguzi ufanyike kwa nchi ambayo si yake ila inaonekana kuwa ina matatizo  ya kiuchumi au kisiasa na kuna uhitaji ya kuikagua.

Kila  nchi inapokaguliwa  matokeo huwa uandaaji wa  mpango wa utekelezaji wa kushughulikia  matatizo au changamoto zilizojitokeza na kuoneshwa na taarifa ya ukaguzi. Chombo cha ufuatiliaji huandaa taaarifa ya mwaka kwa ajili ya kuiwasilisha kwenye mkutano mkuu wa wakuu wa nchi na serikali na taarifa hizi hupaswa kuwa wazi kwa umma.

Hadi Juni ya mwaka 2016, nchi 35 kati ya nchi 54 za Umoja wa Afrika zilishajiunga  na APRM kwa kutia saini hati ya  makubaliano. Kati ya nchi hizo, nchi 17 ikiwamo Tanzania zimeshajichunguza zenyewe na zimeshafanyiwa ukaguzi  na nchi wanachama wenziwe wakati nchi tatu zilishakamilisha ukaguzi binafsi na zilikuwa zikisubiri ukaguzi  katika kikao kitakachofuata cha wakuu wa nchi.

Nchi ya Tanzania  imeshafanyiwa ukaguzi wa kwanza. Nina ushahidi kuwa pamoja na kuwa wapo watu walioshiriki katika mchakato huo ni watu wachache sana wanaoufahamu mfumo huu wa APRM na jinsi unavyofanya kazi. Alipotajwa Balozi Sefue kuwa ameteuliwa katika chombo hicho cha APRM wapo watu waliouliza kuwa APRM ndio nini na kuwa atakuwa anafanya kazi gani.

Ukaguzi huo ulipofanyika ilitolewa taarifa na  hivyo  kuna mapendekezo ya kuboresha  hali ya kidemokrasia, siasa, uchumi  na masuala ya kijamii yaliyotolewa pia. Haya ni kwa ajili ya kuleta ubora nchini kwetu na yanapaswa kuwa wazi kwa Watanzania wote ili waone jinsi Serikali yao ilivyojitoa  kukaguliwa na ukaguzi una mapendekezo yapi muhimu.

Mfumo wa APRM una vyombo vikuu vitatu; Jukwaa la wakuu wa nchi wanachama wa mfumo huo, hiki ndio chombo kikuu cha uamuzi na utawala. Jopo la watu mashuhuri wanaoteuliwa na jukwaa la wakuu wa nchi na sekretariati

Kazi ya jopo la watu mashuhuri ambapo ndipo Balozi Sefue ataingia ni kuhakikisha mfumo wa ukaguzi ni huru,wenye weledi na unaoaminika.. Wajumbe wa jopo hili huchaguliwa  na Jukwaa la wakuu wa nchi na hushika wadhifa kwa  muda wa miaka minne ila mwenyekiti wao hutumikia kwa miaka mitano. Katika kipindi hicho cha miaka minne jopo hufanya kazi zake katika  nchi zile ambazo ziko katika  mchakato wa ukaguzi.

Kipindi cha Balozi Sefue kituamshe Watanzania kufuatilia mapendekezo ya ukaguzi ule wa mwanzo. Pia nchi yetu kwa sasa imeshafikia muda wa ukaguzi mwingine, tunapaswa kujua mifumo iliyoko katika nchi inayohusu APRM ikiwa ni njia nzuri sana ya nchi yetu kujitazama yenyewe kuona na kukiri udhaifu wake kwa nia ya kutaka kuyasahihisha. Yapo mengi ya kujitazamisha katika maeneo yote hayo hasa katika eneo la demokrasia, uchumi na Siasa.

Katika ngazi ya APRM ya kitaifa zipo kanuni zinazoitaka nchi kuweka mifumo ya kuwezesha ukaguzi huu. Hapa nchini kwetu ipo na ndio maana tuliweza kujiangaliza na kisha kukaguliwa.  Tunapokuwa tunamfurahia na kumshangilia Balozi Ombeni Sefue kwa nafasi hii hebu tuanze kufuatilia katika mfumo wa  APRM nchini kuona maendeleo yake  na iwapo mapendekezo yale ya awali yameshatekelezwa kwa kiasi gani. Itakuwa si vyema iwapo tutaendelea kutokufuatilia na kujua vyombo muhimu kama hivi ambavyo vimewekwa na nchi ikavikubali kwa hiari  na mmoja wetu amepewa wadhifa huko kisha tusifanye inavyotakiwa.

Iwapo mfumo huu ulikuwa umetulia sasa uinuke uendelee na kazi kwani shughuli imetusogelea na inatubidi tushughulike. bHongera sana Balozi Ombeni Sefue na Watanzania kwa ujumla.

Imeandaliwa na Dk. Helen Kijo Bisimba

Mkurugenzi Mtendaji

LHRC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles