24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

UTAZIPENDA STORI ZA ‘NINI’ KUHUSU MAISHA, MAPENZI, MUZIKI

Na JOHANES RESPICHIUS

WENGI walianza kumfahamu baada ya kujiunga Mj Records pamoja na tetesi za kutoka kimapenzi na rapa, Ney wa Mitego, huyu ni Agness Antony maarufu kama Nini.

Katika uga wa Bongo Fleva ana nyimbo kadhaa ikiwamo Niwe Dawa aliomshirikisha Ney wa Mitengo pamoja na Kolo, unaofanya vizuri kwa sasa katika redio na runinga.

SWAGGAZ tumepiga stori na mrembo huyo mapema wiki hii alipotembelea Ofisi za New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya Mtazania, Rai, Bingwa na Dimba hapa Dar es Salaam na mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo:-

Swaggaz: Kuna tofauti gani kati ya usimamizi wa Ney wa Mitego na ule wa Mj Records katika ufanyaji kazi?

Nini: Ufanyaji kazi umebadilika kwa sababu nilipokuwa MJ, sikuwa na uhuru wa kufanya kazi nje ya studio lakini sasa hivi nina uhuru wa kufanya kazi na prodyuza yeyote.

Muziki ninaouimba ni tofauti na ule ambao nilikuwa naimba nikiwa Mj Recods, kwa hiyo naweza kusema kibiashara na kimuziki nimebadilika sana.

Swaggaz: Ni kweli Ney wa Mitego alikuwa mpenzi wako?

Nini: Baada ya mimi kuondoka MJ Records kuna tetesi nyingi ambazo zilizuka ikiwemo hiyo ya kutoka kimapenzi na Ney.

Mimi na Ney tunafanya kazi na kama unavyojua sasa hivi rasmi nipo chini ya lebo yake ya Free Nation kwa hiyo kiufupi naweza kusema kuwa ni bosi anasimamia kazi zangu, hayo mambo mengine yalianzishwa baada ya kuondoka Mj na hayana ukweli wowote.

Swaggaz:  Unadhani kwanini tetesi hizo zilianza kusikika hata kabla hujatoka Mj Records?

Nini: Naweza kusema Ney ni rafiki yangu wa karibu lakini Watanzania tumeshakariri kwamba wakikuona na mtu basi wanajua ni mpenzi wako.

Pia hali hiyo ilichangiwa na aliyekuwa meneja, Daxo Chali, kusema kuwa nimetoka kwenye uongozi kwa sababu ya tofauti zake na Ney ile picha ikawafanya watu kuamini kwamba natoka na Ney.

Swaggaz: Ilikuwaje urafiki wako na Ney ukaingia kwenye kazi?

Nini: Sababu ni kujiunga Free Nation na Ney amekuwa mtu ambaye ananisapoti katika muziki wangu baada ya kuachana na Mj Records, akaamua kunisaini ili kupunguza zile stori za kunisaidia ningali si msanii wake.

Swaggaz: Una mawasiliano gani na Daxo tangu utoke MJ?

Nini: Kiukweli sina mawasiliano yoyote na Daxo, sijawahi kukutana naye hata kwa bahati mbaya.

Swaggaz: Kulikuwa na tatizo lolote na Daxo mpaka akaondoka MJ?

Nini: Familia yangu ndiyo ilianza kumtafuta Daxo na kumwambia ni bora nifanye kitu kingine kwa sababu siku zilikuwa zinaenda hawaoni mafanikio yoyote ni bora nirudi shule kwa kuwa unaweza kukaa mwaka mzima unatoa wimbo mmoja.

Daxo alikubali kwani na yeye alikuwa tayari amekuwa na sababu zake hivyo aliniambia kutokana na ‘situation’ hiyo hatutaendelea kufanya kazi pamoja lakini si kweli kwamba nilifukuzwa.

Swaggaz: Una mpango wa kuchora ‘tattoo’ kama alivyo Ney?

Nini: Sina ‘tattoo’ yoyote na siwezi kuchora, hata huyo Ney ‘ha-wish’ kuniona nimechora.

Swaggaz: Mashabiki zako watarajie nini baada ya Kolo.

Nini: Watarajie mambo mazuri na muziki wenye ladha tofauti kwani kuwa chini ya Free Nation si kwamba kazi zangu zote zitatoka chini ya lebo hiyo, nitafanya na watu mbalimbali ilimradi kazi iwe nzuri.

Swaggaz: Upo kwenye uhusiano wa mapenzi?

Nini: Nipo kwenye mahusiano sema si mtu ambaye anapenda mambo ya ‘social media’, maana kutokana na tetesi hizi ningekuwa nimeshamposti ili ‘ku-prove wrong’ maneno yao.

Swaggaz: Ni kweli wewe ndiyo sababu ya msanii B Gway aliyekuwa chini ya Ney kuondoka Free Nation?

Nini: Si kweli kwa sababu ni kitu ambacho sihusiani nacho kabisa na ni mtu ambaye nilikuwa namwona tu studio, sielewi chochote kuhusiana na makubaliano yao na uongozi wake.

Swaggaz: Kitu gani ambacho mashabiki zako hawakijui kutoka kwa Nini?

Nini: Mimi ni msichana mdogo ambaye nina majukumu yanayonizidi umri, niliamua kuanza kujitegemea nikiwa mdogo licha ya kuishi nyumbani nikuwa na mama na dada yangu.

Nini ni mpole sana unajua watu wengi wakiangaliaga picha zangu wanaona ni mtoto mwenye mambo mengi lakini ni mpole, sipendi kwenda klabu labla niwe na sababu maalumu.

Kitu kingine ambacho watu hawakijui kuhusu Nini ni kwamba, nimeanza kuimba nikiwa shule ya msingi kama kiongozi wa kwaya, kwa bahati nzuri nilisoma shule ya dini kwa hiyo kulikuwa na misa za kila mwezi kwaya yetu ilikuwa inaimba.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,853FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles