24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UTAWALA WA MAGUFULI TUTASHUHUDIA MENGI

magu-na-jk

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

NILIWAHI kuandika andiko moja juu ya agizo la Rais Dk. John Magufuli kuhusu wamachinga, alipowaagiza viongozi wa Mkoa wa Mwanza kuwaandalia mazingira mazuri ili kuondoka katika maeneo ambayo si rasmi katika shughuli zao.

Katika andiko hilo, nilidokeza jinsi viongozi wa Mwanza walivyopewa mtego, ikizingatiwa kwamba tangu Magufuli achaguliwe kuwa rais kumekuwapo na hali ya watumishi kufanya kazi kwa presha na msukumo wa matamko bila kufuata sheria.

Wote tumeshuhudia katika siku za hivi karibuni jinsi wamachinga walivyoondolewa katikati ya Jiji la Mwanza na kupelekwa maeneo mbalimbali yakiwamo Nyegezi, huku wale wenye magari makubwa wakielekezwa kwenda kuyaegesha maeneo ya Sinai.

Hatua ya wamachinga hao kuondolewa ilitokana na agizo la Rais Magufuli alilolitoa alipokuwa Mwanza wakati wa ziara yake ya Kanda ya Ziwa.

Wakuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Leonard Massale, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, walitakiwa kukaa pamoja na wamachinga hao ili kukubaliana na kuboresha maeneo pendekezwa ili kuwahamishia huko.

Lakini cha ajabu, viongozi hao walianza kupishana kauli kitendo kilichofanya madiwani, wabunge, meya na naibu meya kutoelewana na wakuu wa wilaya, mkoa na mkurugenzi.

Hatua ya kutoelewana viongozi hao ilisababisha wabunge, madiwani, meya na naibu meya kuwa kitu kimoja na wamachinga kupambana na wakuu wa wilaya na mkuu wa mkoa waliojitapa wana vyombo vya dola watakavyovitumia kuwaondoa wafanyabiashara hao licha ya viongozi wa kisiasa kuwaunga mkono.

Ilifikia hatua ya kila mmoja kuonyesha jeuri dhidi ya mwingine. Tesha aliwahi kusema kwamba ikiwa hatofanikiwa kuwaondoa wamachinga, ni heri akajiuzulu. Hakika alifanikiwa kuwaondoa kwa sababu ilitumika nguvu kubwa ya vyombo vya dola kitendo kilichowaogopesha.

Cha kusikitisha na maajabu, Mongella, alifurahia mpango wa kuwaondoa wamachinga kwa sababu naye alivunja mabanda yaliyobaki, lakini wakati wakiwa wanatekeleza hilo, Rais Magufuli, aliwatangazia  wamachinga kurudi katika maeneo yao.

Hakika tulishuhudia jinsi mgambo waliokuwa wakilinda mitaa mbalimbali wakikimbia kuelekea ofisi za jiji ili kukwepa kupigwa na wamachinga waliokuwa wakishangilia baada ya tamko la Rais Magufuli.

Binafsi naunga mkono na wakati huohuo siungi mkono tamko la Rais Magufuli la kutaka wamachinga kurudi katika maeneo yao.

Pia amewarudisha mjini wakati tayari fedha za walipakodi zimetumika kutekeleza mpango wa kuwahamisha, huku kukiwapo na mvutano mkali katika makundi hayo.

Naweza kusema utawala wa Rais Magufuli umekuwa mgumu kwa watumishi wa umma kutokana na wengi kutojua nini anachotaka.

Baadhi ya watumishi wamekuwa wakifanya kazi kwa presha na hata wengine wamekuwa na kusudio la kuacha kazi kwa sababu mfumo unaotumika kuwaondoa kazini ghafla umekuwa ukiwashusha heshima zao.

Pia ndani ya watumishi hao, hususani wataalamu wakiwamo wachumi, wamekuwa katika mvutano juu ya kauli zinazotolewa na wanasiasa, ambazo haziendani na taaluma hiyo, lakini zinalazimishwa kutekelezwa kama mfumo jambo ambalo si jema.

Nimalize kwa kusema kuwa tutashuhudia mengi kwa miaka mitano, lakini nimpongeze Rais Magufuli kwa kuendeleza msimamo huo kwa sababu wengi walizoea kufanya kazi kwa mazoea.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles