23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Utata wizi wa kompyuta ofisi ya DPP

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linafanya uchunguzi wa wizi wa kompyuta katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Kanda ya Dar es Salaam.

Hata hivyo maswali yameibuka juu ya wizi katika ofisi hiyo nyeti isijulikane mwizi aliweza vipi kuingia na nini haswa kipo katika kamyuta hiyo. Tukio la wizi wa kompyuta katika ofisi hizo lilianza kusikika juzi na kuthibitishwa jana na Kamanda Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Mambosasa alisema taarifa walizipata Jumanne asubuhi na wanaendelea kufanya uchunguzi.

Alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Alipopigiwa simu, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga kuulizwa kuhusu tukio hilo, alijibu kwamba yuko kwenye kikao.

Tukio hilo limetokea ikiwa ofisi hiyo iko katika mchakato wa kujadiliana na kuingia makubaliano na watuhumiwa mbalimbali wa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Miongoni mwa kesi ambazo ziko katika hatua ya makubaliano ni kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa IPTL, Harbinder Sethi na James Rugemalira wanaodaiwa kutakatisha zaidi ya Sh bilioni 309.

 Watuhumiwa wengine ni mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera anayetuhumiwa kukwepa kodi na kutakatisha Sh milioni 173.

Mtuhumiwa mwingine ni Yusuf Ally maarufu Mpemba wa Magufuli, anayetuhumiwa kusafirisha nyara za Serikali zenye thamani zaidi ya Sh milioni 200.

Ofisi hiyo kwa wiki mbili zilizopita imeingiza zaidi ya Sh bilioni 40 ambazo kati yake zaidi ya Sh bilioni 3.6 zimepokewa na zilizobakia wahusika watalipa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati yao na DPP.

Pia Serikali imetaifisha nyumba sita za washtakiwa waliokuwa wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ndani ya wiki moja.

Oktoba 4, mwaka huu, mshtakiwa Yasin Katera aliyekuwa akishtakiwa pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Takukuru, Godfrey Gugai alilipa faini ya Sh milioni 100 na Serikali ikataifisha nyumba moja iliyopo Nyegezi, Mwanza.

Alilipa faini hiyo baada ya kukiri kosa la kutakatisha fedha huku akijua fedha hizo ni zao la kuficha ukweli baada ya kudai ni mmiliki wa nyumba wakati nyumba ni mali ya rafiki yake, Gugai.

Wafanyabiashara  Magdalena Uhwello na Halima Nsubuga walikiri makosa ya kutakatisha fedha wakahukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 101 na fedha zao  Dola za Marekani 388,000 kutaifishwa na Serikali.

Mahakama iliamuru washtakiwa wakishindwa kulipa  fedha hizo wataenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kuendesha upatu na wataenda jela miaka 20 kwa kutakatisha fedha.

Oktoba 7-11, mwaka huu, wafanyabiashara watatu,  Mohammed Yusufali, Arifali Paliwalla na Sameer Khan walilipa fidia Sh 1,201,000,000 baada ya kukiri makosa yao na nyumba nne zilizopo Bagamoyo mkoani Pwani na Masaki, Dar es Salaam zilitaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Elinaza Luvanda. DPP aliwapunguzia mashtaka kutoka 544 na kubakia matatu.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya alidai shtaka la kwanza na la pili yanamkabili mshtakiwa Yusufali pekee.

Kwamba katika vipindi tofauti kati ya Januari 2008 na Januari 2016 jijini Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Farm Plant Limited, kwa nia ya kukwepa kodi aliwasilisha ‘retuns’ za kughushi kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha ukwepaji kodi wa zaidi ya Sh bilioni 21.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2015 na Januari 2016, kwa vitendo kama hivyo, mshtakiwa huyo alisababisha ukwepaji kodi wa Sh 1,684,559,546.47.

Shtaka la tatu la washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2008 na Januari 2016, kwa vitendo vyao vya uwasilishaji wa nyaraka za uongo za ulipaji kodi, waliisababishia TRA hasara ya Sh 24,303,777,426.70.

Mahakama iliamuru mshtakiwa Yusufali alipe fidia ya hasara aliyoisababishia TRA ya zaidi ya Sh bilioni 24 na tayari alishalipa sh bilioni moja.

Wakili Tibabyekomya alisema kiasi kilichobaki kitalipwa kwa muda wa miezi 24 ambapo kila mwezi atalipa sh 970,990,726.08 pamoja na kutaifishwa kwa nyumba nne zilizo maeneo ya Masaki na Bagamoyo kuwa mali ya Serikali.

Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, wakili huyo aliomba alipe fidia ya Sh milioni 10 ya hasara aliyoisababishia TRA ambapo tayari alishalipa sh milioni moja.

Alisema kiasi kilichobaki kitalipwa kwa kipindi cha miezi 12 kwa kila mwaka Sh 750,000.

Kwa upande wa mshtakiwa wa tatu, wakili huyo aliomba alipe fidia ya Sh milioni 300 kutokana na hasara aliyoisababishia TRA na tayari alishalipa Sh milioni 200.

Alisema kwa mujibu wa makubaliano hayo, kiasi kilichobaki kitalipwa kwa kipindi cha miezi 10 kuanzia tarehe aliyoingia makubaliano na kila mwezi atalipa Sh milioni 10.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimwachia huru Mkurugenzi Mkuu wa Benki M (Tanzania), Sanjeev Kumar (63) na kumtaka kulipa fidia ya zaidi ya Sh bilioni 6 na faini ya Sh milioni 2 baada ya kukiri.

Mshtakiwa Kumar ametakiwa kuilipa fidia hiyo ndani ya miezi 24 na tayari ameshalipa Sh milioni 690.

Akisoma adhabu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi alisema kuwa katika mashtaka hayo mawili, mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni moja kwa kila kosa. 

Alisema pia mshtakiwa atatakiwa kulipa fidia ya Sh 6,039,103,579 ambazo atalipa kwa miezi 24, kwa kila mwezi Sh milioni 222.8.

Kigogo wa Michezo, Michael Wambura alikiri makosa ya kujipatia jumla ya Sh milioni 100.9  na wakakubaliana na DPP kurejesha fedha hizo kwa awamu tano na tayari Oktoba 7 alirejesha Sh 20,249,531.

Wakili maarufu, Dk. Ringo Tenga na wakurugenzi wenzake wa Kampuni ya Six Telecoms, wameachiwa huru baada ya kuingia makubaliano na DPP ya kulipa Dola za Marekani 3,748,751.19, ndani ya miezi sita, kuiachia Serikali nyumba iliyopo Mikocheni na mshtakiwa wa sita kulipa Sh milioni 30.

Wakurugenzi hao; Dk. Tenga, Hafidh Shamte na Peter Noni na Noel Chacha ambaye ni Ofisa Mkuu wa Fedha, wanatakiwa kulipa zaidi ya Sh bilioni 3 na Frank Mwalongo anatakiwa kulipa Sh milioni 30.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisema makubaliano mengine ambayo mahakama inatakiwa kuzingatia ni kwamba washtakiwa wamelipa Sh milioni 150, Dola za Marekani 150,000 na Dola 3,585,115 zilizobakia washtakiwa kuanzia wa kwanza hadi watano watalipa ndani ya miezi sita kuanzia Oktoba 7.

Mshtakiwa Mwalongo alilipa Sh milioni 35 alizokubali kulipa kama fidia na faini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles