23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

UTATA MTUPU PEDI ZA KUFUA

Jenipher Shigoli akionesha taulo hiyo ilivyo
Jenipher Shigoli akionesha taulo hiyo ilivyo

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MWILI wa binadamu hupitia mabadiliko mbalimbali katika ukuaji wake, kipindi hicho huitwa balehe ambapo uhusisha mabadiliko yote ya kimwili – kimawazo na kihisia.

Mabadiliko hayo huwapata jinsi zote yaani ya kike na kiume. Ni katika kipindi cha mabadiliko ya mwili ambapo msichana huanza kupata damu ya hedhi.

Hatua hiyo muhimu huitwa kupevuka  au kuvunja ungo kama inavyojulikana, ni kipindi maalumu katika maisha ya mwanamke aliyefikia umri wa kuzaa.

Hedhi hutokeaje

Zipo ovari mbili (vifuko vya mayai) katika mwili wa mwanamke, moja upande wa kushoto na nyingine kulia ambazo hutengeneza mayai ya uzazi ambayo husafirishwa hadi katika mji wa mimba kupitia mirija ya uzazi.

Kila mwezi ovari moja huachia yai, mchakato ambao huitwa kitaalamu ovulation na wakati huo mabadiliko ya homoni huuandaa mji wa mimba (uterus) kutengeneza ukuta mpya uitwao endometrium kwa ajili ya kujiweka tayari kwa mapokezi ya mimba inayoweza kutungwa.

Yai linalofika katika uterus iwapo halitarutubishwa na mbegu ya mwanamume, ukuta huo humeguka na kutoka nje ya mji wa mimba kupitia ukeni ukiwa pamoja na damu.

Zamani wanawake wengi wamekuwa wakitumia vipande vya khanga kujihifadhi wakati wa hedhi. Lakini kukua kwa teknolojia kukasababisha kutengenezwa taulo za kisasa za kutumia na kutupa ambazo huuzwa kwa bei tofauti tofauti madukani.

Ni changamoto kwa wasichana

Nchini Tanzania suala la hedhi salama kwa wasichana hasa waliopo shuleni linatajwa kuwa bado ni kitendawili na changamoto kwa walio wengi hususan vijijini.

Hali hiyo inasababishwa na hofu ambayo huwakumba wakiwa katika kipindi hicho ya kuchafua sare za shule, kuchekwa na kutaniwa na wanafunzi wenzao hasa wa kiume walio chini kiumri.

Tafiti mbalimbali ikiwamo ya Haki Elimu ya mwaka 2013, unasema kutohudhuria kwao masomo huchangia kuzorotesha kwa kiasi kikubwa ufaulu wa wanafunzi husika.

Abuni taulo za kufua

Hali hiyo ndiyo iliyomchochea mjasiriamali Jenipher Shigoli, kufanya utafiti akiwa na nia ya kuja na mbinu itakayowasaidia wasichana kutohofia na kuhudhuria masomo yao pasipo kujali kipindi cha hedhi.

“Kitaaluma ni mwanasheria pia ni mwanadiplomasia lakini napenda mno ujasiriamali, nimekuwa nikijihusisha na utengenezaji wa bidhaa za usafi tangu mwaka 2013. Kupitia biashara hiyo nimeweza kupata tenda za kusafisha vyoo vya shule mbalimbali nchini kupitia kampeni ya choo salama inayoendeshwa na kampuni ya Malikia ambayo mimi ndio mkurugenzi wake,” anasema.

Anasema kupitia kampeni yake hiyo ameweza kufika katika shule nyingi za Mkoa wa Dar es Salaam, Dodoma na Iringa.

“Nikiwa katika shughuli hizo za kampeni ya choo salama, ndipo nikagundua kwamba wasichana wengi hasa kwa shule za kule vijijini hushindwa kuhudhuria masomo wakiwa katika kipindi cha hedhi kwa hofu ya kuchafuka na kuchekwa,” anasema.

Kilichomsukuma kubuni taulo hizo

Shigoli anasema alipata nafasi ya kuwahoji baadhi ya wanafunzi ambao walimueleza kuwa ili kujihifadhi hutumia manyoya ya kuku, udongo, magunzi ya mahindi, ugali au soksi.

“Wapo ambao walinieleza huwa wanatumia vitambaa vya khanga au vitenge lakini wataalamu wa afya wanasema si salama kwa afya kwani rangi inayotumika kutengeneza bidhaa hizo kwa kawaida huchuja zinapokuwa zimelowa majimaji.

“Walimu nao walinieleza kuwa baadhi ya wanafunzi huacha masomo na kuamua kukaa nyumbani kwa sababu ya hedhi, kwani hata wale wanaovaa vitambaa huwa hawajiamini, hali ambayo huwaathiri kisaikolojia,” anasema na kuongeza:

“Kwa kuwa wengi wanashindwa kumudu gharama za kununua taulo za kutumia na kutupa nilipata wazo la kutengeneza taulo za kutumia zaidi ya mara moja,” anasema.

Alivyofanikisha wazo lake

Anasema baada ya kupata wazo hilo aliwashirikisha watu mbalimbali wakiwamo wataalamu wa maabara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shirika la  Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ambao walimsaidia.

“Walinishauri na tulichukua muda wa miezi sita kukamilisha bidhaa hizo,” anasema.

Malighafi ni pamba halisi

Shigoli anasema taulo hizo zimetengezwa kwa ustadi wa hali ya juu na kwa kutumia pamba halisi, kitambaa na nailoni maalumu ambayo huweza kupokea damu ya hedhi hadi kiwango cha mililita 30 hadi 40.

“Uwezo huo unalingana na ule wa taulo zingine zinazouzwa huko madukani na huweza kuvaliwa kati ya saa sita hadi saba. Baada ya saa hizo unalazimika kuifua na kuianika ikauke vizuri kwa ajili ya kuitumia tena na hudumu hadi mwaka mmoja,” anasema.

Atunukiwa tuzo

Anasema kupitia bidhaa yake hiyo aliweza kuibuka mshindi katika shindano la kusaka wabunifu barani Afrika mwaka jana linalosimamiwa na taasisi ya ‘African Entrepreneur Award’.

“Niliibuka mshindi wa kwanza na nilizawadiwa Dola za Marekani 150,000 sawa na Sh milioni 300 za Kitanzania,” anasema.

Serikali yampa eneo la kiwanda, mtaji

Jenipher anasema anaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu kwa kumpatia mtaji wa Sh milioni 30 ili kukuza biashara yake.

“Kupitia wizara hiyo, nimepewa eneo la kutosha kujenga kiwanda huko Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya kuzalisha bidhaa hizi tunatarajia kukizindua ifikapo Machi, mwaka huu,” anasema.

Anasema tayari pia ameshapeleka barua Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwamba anatarajia kupata ushirikiano wa kutosha katika kuisaidia jamii.

Jenipher anawasihi Watanzania hasa wanawake kutokuwa na wasiwasi juu ya taulo hizo alizobuni.

“Nimepitia taratibu zote kisheria, zimepimwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na zimeonekana zina ubora, nimeenda pia Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) nimepewa ‘certificate’ na kama nilivyoeleza awali kuna wataalamu ambao nashirikiana nao kutoka UDSM na SIDO,” anasema.

Simulizi ya Monica

Monica Elius (si jina lake halisi) anasema ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu aanze kutumia taulo hizo za kufua na kwamba amebaini tofauti kubwa ikilinganishwa na zile za kutumia na kutupa.

“Sikujua kama kuna mbunifu Mtanzania ambaye ameanza kuzitengeneza pia taulo za aina hii nchini, maana nilianza kuzitumia muda mrefu sasa umepita na nilikuwa najua kwamba zinatoka nje na kuletwa kama msaada.

“Nina dada yangu ambaye mume wake alikuwa akifanya kazi katika kambi ya wakimbizi iliyopo Ngara mkoani Kigoma, wanawake na wasichana waliokuwa wakiishi katika kambi hiyo walikuwa wakigawiwa na mashirika ya misaada,” anasema.

Alianzaje kuzitumia

“Awali nilikuwa natumia taulo za kawaida zinazouzwa madukani, lakini kila nilipotumia nilikuwa napata muwasho mkali mno, hali yangu ilikuwa mbaya,” anasema.

Anasema alikuwa analazimika kwenda hospitalini kupima na kupewa matibabu kila mara ingawa haikugundulika tatizo lilikuwa nini hadi anapatwa na hali ya namna hiyo.

“Nakumbuka kuna wakati nilikuwa mkoani Morogoro nilitokewa na hali hiyo nikaenda katika zahanati moja na kumuelezea daktari niliyemkuta, alinipima na kugundua kuwa nina mzio na hizi taulo za kawaida.

“Hivyo, alinishauri ninunue khanga mpya nikate vipande vya kunitosha au ninunue gozi (kitambaa maalumu ambacho hutumika kufunga vidonda) pamoja na pamba ili nijitengenezee taulo zangu mwenyewe,” anasema.

Gozi ni gharama kubwa

Anasema; “… nilishindwa kumudu hilo kwani nilikuwa natumia fedha nyingi kununua gozi ambalo huuzwa kati ya Sh 25,000 hadi 30,000 na pamba ni kati ya Sh 25,000 hadi 30,000 kwa hiyo nilihitaji Sh 60,000 ili niweze kupata bidhaa hizo na kutengeneza taulo za kutumia miezi mitatu hadi minne, ni gharama kubwa mno.

Anasema siku moja akiwa na dada yake huyo alimshangaa kuona anahangaika kutengeneza vitambaa vya kujihifadhi jambo ambalo lilimlazimu kumsimulia sababu za kufanya hivyo.

“Alinishangaa, ikabidi nimsimulie ndipo akaniambia atanipatia hizo taulo za kufua, sikuamini kama zipo hadi siku aliponiletea,” anasema.

Anasema taulo hizo huuzwa kati ya Sh 5,000 hadi 8,000 na kwamba tangu ameanza kuzitumia ameondokana na ile adha ya kupatwa muwasho katika sehemu zake za siri.

“Unaona kama hii niliyobeba (akimuonesha mwandishi wa makala haya) ina mwaka sasa lakini bado naitumia, haijachoka kama unavyoiona,” anasema.

Uzoefu wake

Monica anasema taulo hizo zimetengezwa na malighafi ya pamba pekee na kitambaa maalumu hali ambayo inaifanya kuwa laini na murua wakati wote anapokuwa ameivaa.

“Yaani ni laini kiasi kwamba unajisikia raha ukiwa umeivaa hakuna michubuko wala huwezi kujihisi harufu mbaya unapokuwa umeitumia, hata ukipata muwasho si kama ule unaotokea ukiwa umevaa taulo zile za kutumia na kutupa,” anasema.

Zinafuliwaje?

Anasema suala la usafi wa taulo hiyo ni wa muhimu kuuzingatia ili mtumiaji asipate matatizo mbalimbali ya kiafya kama vile muwasho na hata harufu mbaya.

“Huwa nafulia sabuni ya unga, naona ndiyo inafaa zaidi kuliko zingine. Hii unapaswa kuifua na kuisuuza vizuri kwa maji mengi, ukisuuza na maji kidogo ikikauka unaikuta ina alama za mistari zimekatisha katikati.

“Alama hizo hufanya muonekano wake kuwa wa kuudhi, uzuri ni kwamba unapoifua na kuianika kukiwa na jua kali haichukui zaidi ya saa mbili unaikuta tayari imekauka na unaweza kuivaa tena,” anasema.

Anaongeza kuwa ukiwa safarini na ukawa umetumia taulo hii ni tofauti na zile za kutupa, ukijisafisha hubaki na harufu, unahifadhi vizuri taulo yako na kwenda kuifua nyumbani pindi unapofika,” anasema.

Anasema taulo hizo zinasaidia kupunguza gharama kwani mtu anaponunua huweza kukaa nazo hadi mwaka mzima.

Daktari

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya kinamama na Uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Belinda Balandya anasema kipindi cha hedhi ni muhimu kwa afya ya mwanamke.

“Mwanamke anapokuwa katika siku zake hulazimika kutumia taulo hizo ambazo kazi yake kuu ni kupokea ile damu inayotoka, kama hatavaa maana yake ni kwamba itapitiliza kuchagua nguo zake.

“Taulo za kutumia na kutupa jinsi zilivyotengenezwa zina ‘layer’ maalumu kwa ndani ambayo hufyonza damu ya hedhi, hulazimu kubadili mara nyingi (kiasi cha kila baada ya saa nne) hasa inapokuwa inatoka kwa wingi,” anasema.

Athari

Daktari huyo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas) anasema kuna athari kubwa iwapo mwanamke hatazingatia usafi akiwa hedhi.

“Kwa kuwa inanyonya damu maana yake ni kwamba hufika wakati unakuwa kama vile umevaa kitu kibichi, hivyo ngozi huanza kupata michubuko. Kwa wale ambao ngozi yao ni ngumu kidogo huwa si rahisi kuona michubuko hiyo lakini wanapojisafisha kwa maji na sabuni huhisi maumivu,” anasema.

Anaongeza kuwa damu ni sehemu ambayo bakteria huota kwa urahisi kwa sababu wanakuwa wanapata chakula wanachohitaji kwa urahisi, mtu anaweza kuendelea kuvaa kwa sababu hajui jambo hili lakini ni hatari.

Kuhusu taulo za kufua

“Sijaziona, sijawahi kuzisikia, wewe ni wa kwanza kunieleza, lakini zamani mabibi na wazazi wetu walikuwa wakitumia vitambaa… sijui hizo zipoje.

“Kumbuka kwamba nimesema bakteria huzaliana kwa urahisi kwenye damu, sasa kama itafuliwa, isikauke na kubaki na unyevunyevu maana yake ni kwamba bakteria waliozaliwa watabaki na kuendelea kukua hivyo muhusika atakuwa amejiweka kwenye hatari ya kupata tatizo,” anasema.

Akizungumzia taulo za tampons zilizo tengenezwa mfano wa unene wa  kidole na imewekwa kamba kidogo, anasema ni mbaya zaidi.

Anasema kuwa wanawake huzitumia kwa kuingiza ndani ya uke ili kufyonza damu na huitoa kwa kuvuta kamba hiyo inayokuwa imebaki nje ya uke.

“Hizi ni taulo mbaya, wengine wanapoweka wakati wa hedhi chache hujisahau kuzitoa na hivyo kujiweka kwenye hatari ya kupata madhara,” anasema.

Anasema bakteria hao huenda kutengeneza kovu katika mirija ya uzazi mwishowe huziba kabisa na kwamba huweza kupenya na kuingia hadi katika mfumo wa damu na kuleta athari zaidi.

Kauli ya TBS

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Egid Mubofu anasema ni kweli shirika hilo lilipokea maombi ya kupima taulo hizo za Elea.

Anasema bidhaa hiyo bado haijaruhusiwa kuingizwa sokoni.

“TBS tulipokea maombi kutoka kampuni ya Malkia ambao ni wazalishaji wa bidhaa za Elea. Upimaji wa awali wa bidhaa hiyo ulifanyika na matokeo yalionesha kuwa bidhaa hiyo haikidhi kiwango cha bidhaa husika ambacho ni TZS 1659:2014, hivyo mzalishaji akatakiwa  kufanyia marekebisho bidhaa hiyo,” anasema.

Mubofu anasema mpaka sasa mzalishaji wa bidhaa hiyo hajafanyia marekebisho bidhaa hiyo, hivyoTBS bado haijathibitisha ubora wa bidhaa hiyo.

“Bidhaa za pedi ziko katika orodha ya bidhaa za lazima, hii ni kutokana na madhara ya kiafya yanayoweza kujitokeza endapo bidhaa hizo hazitakidhi matakwa ya kiwango husika. Hivyo basi, bidhaa za aina hii hazipaswi kuingizwa sokoni mpaka hapo ubora wake utakapothibishwa,” anasisitiza.

Kauli ya wizara

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Televisheni EATV hivi karibuni, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangalla alisema serikali inafanya tafiti mbalimbali ili kubaini na kuona kama kuna uwezekano wa kupata taulo za hedhi (pedi) ambazo zinaweza kutumika zaidi ya mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles