24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Utata mpya mikataba NSSF

Mkurugenzi wa NSSF Prof. Khyarara
Mkurugenzi wa NSSF Prof. Khyarara

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

UTATA umeibuka dhidi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambalo linadaiwa kuuza nyumba 87 zikiwa chini ya kiwango, huku huduma za kijamii zikikosekana katika maeneo hayo.

Wakazi wa nyumba hizo zilizopo Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, wamefungua kesi namba 225 ya mwaka huu dhidi ya shirika hilo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi, wakilalamikia shirika hilo kwenda kinyume na mikataba yao.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Jaji Penterine Kente, ambapo wadai walikuwa wakiwakilishwa na Wakili Benito Mandele, huku Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF ikiwakilishwa na Wakili Opio Marcels.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF na Kampuni ya udalali ya Majembe.

Wadai  hao kupitia wakili wao Benito waliamua kukimbilia mahakamani kufungua kesi, baada ya kushindwa kupata ufumbuzi wa madai yao katika Taasisi ya Usuluhishi kutokana na walalamikiwa  ambao ni NSSF kutofika.

Katika hatua za awali wadai hao walifikisha suala hilo katika usuluhishi kutokana na mkataba wao kuwataka kufanya hivyo kabla ya kuamua kwenda mahakamani kama walivyokubaliana kwa mujibu wa sheria.

Katika madai waliyowasilisha mahakamani, wanadai mdaiwa wa kwanza ambaye ni Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF, ameshindwa kutekeleza matakwa ya mkataba kwa mradi huo kukosa huduma za kijamii.

Inadaiwa nyumba walizouziwa hazina ubora, ndani ya miezi sita baadhi ya nyumba madirisha hazifungi, dari zinavuja, vigae (tiles) vimebomoka na wakati wa mvua maji yanatuwama ndani na hakuna umeme wa kutosha kwa nyumba zote.

Wanadai kutokana na wadaiwa kushindwa kuwasikiliza mahitaji yao katika barua walikuwa wanalazimika  kutumia fedha zao kufanya ukarabati.

“Kwa kushindwa kufikia mwafaka baadhi yao waliamua kuacha kurejesha mkopo ambao ni zaidi ya Sh milioni 1.5 kila mwezi, ilipofika mwezi na wengine miezi mitatu Kampuni ya Udalali ya Majembe walifika kuwapa notisi na kuwatangazia kuwaondoa,”  walisema kupitia sehemu ya hati ya madai yao.

Wakazi hao wanaiomba mahakama kuiamuru bodi hiyo kurejea mikataba, kutambua majukumu ya msingi ya kila upande na nyumba ziwe za kuwawezesha kuishi na kuwe na huduma za kijamii.

Nyumba hizo ziliuzwa mwaka 2014 kwa mkopo kuanzia Sh milioni 105 hadi Sh milioni 130 kwa kipindi cha miaka 15 ambapo pamoja na riba deni kuu linafikia Sh milioni 200 kwa kipindi hicho.

Inadaiwa kuwa taarifa kuhusu nyumba hizo zilizopelekwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke zinatia shaka, kwani kuna nyumba zilizouzwa kwa Sh milioni 110 lakini taarifa za nyumba hizo katika halmashauri zinaonyesha kuwa thamani yake halisi ni Sh milioni 52, kwani kodi ya pango hudaiwa kwa kuzingatia thamani ya nyumba.

Katika maombi yao, wakazi hao wanaiomba mahakama iamuru hali ilivyo katika makazi yao ibaki kama ilivyo, hadi hapo kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Katika kesi ya msingi, mlalamikiwa wa pili ni Majembe ambaye hakufika mahakamani, hivyo Wakili Mandele aliieleza mahakama kwamba hakuweza kupatikana kwa sababu alipokuwa akifanyia shughuli zake awali alihama.

Waliomba kupatiwa hati nyingine ya wito, ambapo Jaji Kente alikubali kutoa hati nyingine ya wito kwa walalamikiwa hao kufika mahakamani.

Wakili Mandele aliomba kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine ambapo iliahirishwa hadi Oktoba 17, mwaka huu.

Wakati huo huo, maombi ya wakazi hao ya kutaka mahakama kutoa amri ya hali ilivyo ibaki kama ilivyo yamepangwa kusikilizwa Agosti 24, mwaka huu.

Licha ya madai hayo Aprili 2, mwaka huu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Profesa  Godius Khyarara, alitoa rai kwa watu wote  walionunua nyumba za Mtoni Kijichi kukamilisha malipo ya nyumba hizo ndani ya siku 30 na kama hawatafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kunyang’anywa nyumba na kuuzwa kwa wanachama wengine.

Mkurugenzi mkuu huyo alisema, wapo watu wameshikilia nyumba na hawajakamilisha malipo kama mkataba unavyosema na kusisitiza kuwa ndani ya mwezi mmoja kama mtu hajakamilisha malipo, masharti yote ya mkataba yatafuatwa.

Nyumba  hizo  300  zilizoitwa za bei  nafuu  zimejengwa  katika  kiwanja    Namba 1 –308,  kitalu  8  katika maeneo ya Mtoni Kijichi  Temeke , Dar es Salaam.

SARAKASI NSSF

Julai 18, mwakahuu vigogo sita ambao ni wakurugenzi katika Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF), makao makuu jijini Dar es Salaam, wakiwamo mameneja wengine watano walisimamishwa kazi.

Wakurugenzi hao walisimamishwa ili kupisha uchunguzi, baada ya Bodi ya Wadhamini ya Shirika hilo kukutana Julai 15 mwaka huu, chini ya mwenyekiti wake Profesa Samwel Wangwe.

Hatua hiyo ilielezwa ni utekelezaji wa taarifa za wakaguzi wa mahesabu.

Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Yacoub Kidula, Mkurugenzi wa Fedha, Ludovick Mrosso, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Chiku Matessa, Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga, Sadi Shemliwa, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani, Pauline Mtunda na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Crescentius Magori.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles