24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Utata kifo mmiliki wa shule

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MAZINGIRA ya kifo cha mmiliki wa shule za Zamzam ya jijini Dodoma, Rashid Bura (60), umegubikwa na utata baada ya mwili wake kukutwa hauna nguo huku ukiwa na majeraha katika mkono na mguu.

Bura alikutwa akiwa amefariki juzi Mtaa wa Kuu eneo la Majani ya Chai huku mazingira ya kifo chake yakiacha maswali mengi kwa wakazi wa mjini Dodoma.

Mwili wa marehemu huyo ulizikwa jana katika makaburi ya  Chamwino na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa mjini hapa, ambapo wakati mwili huo ukiwasili nyumbani kwake katika eneo la Chang’ombe Extension  saa sita mchana ukiwa katika gari la Polisi lenye namba PT 3762 hali ya huzuni, majonzi vilitawala   huku kila muombezaji akiwa amepigwa na butwaa.

Mazishi hayo yaliongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu pamoja na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gilles Muroto

MTOTO WA MAREHEMU ASIMULIA

Akizungumza na MTANZANIA mtoto wa marehemu, Ally Bura (26),  alisema baada ya kuona baba yao hapatikani alikwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kutoa taarifa na kufungua jalada la uchungizi ili kujua alipo baba yao.

 “Nilipoona baba hapatikani kwa siku ya tatu nilikwenda kwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, nikamueleza tukafungua jalada la kupotea baada ya hapo tulikwenda kwa Sheikh wa Mkoa, ambapo alisema yeye alimtuma baba yao katika mkutano Dar es Salaam na alinifahamisha kwa kunipigia simu kwamba amesharudi.

“Lakini majibu hayo yalizidi kutupa maswali yaliyokosa majibu yeye, huku tukitaka kujua wapi alipo baba na kwa nini hapatikani. Baada ya maelezo ya Sheikh Mustapha akili ilinituma kwenda ofisi kwake baba (marehemu) Mtaa wa Kuu Majani ya Chai kwa lengo la niangalie kama yupo.

 “Nilikwenda huku kichwa kikiwa ninaniuma sana nilipanda Hiace (daladala) za Chang’ombe lakini roho yangu ikiwa inasita nikasema bora niende ofisi kwake nikamwangalie kama yupo.

 “Nilipofika pale nje nikakuta wauza magazeti nikawauliza mzee mmemuona (baba), wengine wakasema jana wengine wakasema juzi basi nikasema mzee atakuwa yupo ngoja nipande juu nikamwangalie.

“Nilipopanda juu ya ghorofa nikakuta geti la nje lipo wazi lakini ule mlango wa ndani umefungwa ila kila ninavyousogelea mlango harufu inazidi kuwa kali ya kama kitu kimeoza.

“Nilikuwa nina ufunguo wangu maana kulikuwa na funguo mbili moja alikuwa nayo mzee ila nyingine aliacha wa ziada nyumbani, nikafungua na ule ufunguo lakini ukawa haufunguki nikichungulia sioni kitu ila harufu ninaisikia.

“Ikabidi niende ofisi ya pili jirani na pale kwa baba nikawakuta wamefungua milango na madirisha yote, nikawauliza hii harufu mmeanza kuisikia tangu lini? wakanambia kama siku tatu hivi.

“Nikapiga mahesabu na mzee jinsi ambavyo haonekani, nikajua basi huyu atakuwa mzee nilirudi nikauparamia mlango ukafunguka na kukuta mwili wa baba ukiwa umelala chini huku ukiwa nauna nguo na ukiwa umevimba kupita kiasi,” alisema

MWILI HAUNA NGUO

“Ulivyofunguka nikamkuta mzee amekaa chini kaishabadilika kavimba ( mtoto analia), alikuwa kaharibika sana na tuliukuta mwili ukiwa hauna nguo na simu yake ipo mezani na kwenye pochi yake kulikuwa kuna hela na simu ilikuwa imezimwa.

“Baada ya hapo nilimpigia simu mimi mwenyewe Kamanda wa Polisi (Gilles Muroto),  akasema asiingie mtu mpaka walipofika baada ya muda walifika na kuanza kufanya uchunguzi,” alisema.

KAULI YA RAFIKI YAKE

Rafiki wa karibu na mwanzilishi mwenza  wa Taasisi ya Dalai Islamic Center, Abdillah Mboryo alisema mwili wa Bura ulikutwa umeharibika vibaya ndiyo mana wamefanya haraka kuuzika katika makaburi ya Chamwino jijini hapa.

Mboryo alisema kwa mara ya mwisho Bura alionekana siku ya Jumapili jioni ya Desemba 22, mwaka huu aliposali  katika Msikiti wa Nunge na baadaye aliwanunulia kahawa baadhi ya watu eneo la karibu.

Alisema  jioni hiyo ya Jumapili marehemu alimpigia simu Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab kumpa mrejesho wa kile kilichojiri katika mkutano wa amani uliofanyika jijini Dar es Salaam.

“Lakini baada ya hapo hakuonekana wala simu yake haikupatikana hadi jana (juzi) mwili ulipokutwa ofisini ukiwa na majeraha matatu na hakuwa na nguo hata moja,” alisema Mboryo.

Alisema mwili wake ulikutwa na  majeraha katika mkono wa kushoto, mguu  na michirizi mwilini  hali inayoashiria huenda ameuawa.

SHEIKH WA MKOA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu alisema alipokea simu ya mwisho ya marehemu siku ya Jumapili jioni ikimweleza kwamba kazi aliyomtuma ameishaifanya.

“Wakati ananipigia simu nilikuwa naongea na simu nyingine nilipomaliza kuzungumza nikapokea yake, akaniambia kazi uliyonituma nimeishaliza na nimeenda salama na nimerudi salama, nikamwambia asante na ninashukuru,” alisema.

Sheikhe Mustapha alisema Bura alikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya amani ya Mkoa wa Dodoma na alielekea jijini Dar es Salaam akiwa na mjumbe mwingine, Mchungaji  Timothy Holela kwa ajili ya mkutano wa viongozi wa dini nchini.

 “Sio kwamba nilimtuma alienda kwenye majukumu yake ya mkutano wa amani kwa viongozi wote nchini,”a lisema

ADAI NI TAASISI

Akizungumza wakati wa ibada iliyofanyika nyumbani kwake Chang’ombe Extension jijini hapa, Sheikhe Mustapha alisema marehemu Bura, alikuwa ni zaidi ya taasisi hivyo wamepoteza mtu muhimu.

“Tumezika taasisi, mwanaharakati bora kabisa, huu ni msiba mkubwa sana kwetu, msiba ambao umetuumiza sana, tunamwachia Allah tunatakiwa tushukuru kwa kila jambo tuseme ‘Innalilah Waina Ilah Rajiun’,” alisema Sheikh Mustapha

ALIYEKUWA NAYE ATOA KAULI

Akizungumza na MTANZANIA Mjumbe wa kamati ya amani ya Mkoa wa Dodoma,  kutoka Kanisa la Kiinjli na Kirutheli Tanzania (KKKT),  Mchungaji  Timothy Holela,  ambaye alisafiri na marehemu kwenda jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa amani, alisema kuwa walikubaliana baada ya kumalizika mkutano siku ya Jumamosi waondoke saa nne asubuhi siku ya Jumapili kurejea Dodoma.

“Jambo la kushangaza nilipofika Ubungo saa mbili asubuhi na kumpigia simu alisema yeye kaishafika Mikese Morogoro nikamuuliza mbona umewahi kuondoka akaniambia usafiri wa shida hivyo nimeamua kuondoka mapema,” alisema

Alisema alifika Dodoma saa nne usiku siku ya Jumapili lakini hakuangaika kumtafuta akijua kwamba amefika salama.

“Nikashangaa siku ya Jumatano nikipokea simu kutoka kwa ndugu zake ikiniuliza Bura yupo wapi? nikawashauri waende katika Ofisi ya Kimbinyiko kuuliza kwani ndiyo basi alilokuja nalo, baada ya hapo nami nikawa na maswali mengi rafiki yangu amepatwa na tatizo gani, mpaka nikaja kusikia taarifa za kifo chake,” alisema Mchungaji Holela

KAMANDA WA POLISI

MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi, Gilles Muroto, ambaye alisema kuwa uchunguzi  kuhusu kifo cha marehemu Bura bado Jeshi la Polisi linaendelea nao na pindi watakapokamilisha watatoa taarifa yao.

BURA NI NANI

Akimzungumzia marehemu Bura, mkurugenzi mwenza wa taasisi ya Dalai Islamic Centre, Abdillah Mboryo, alisema enzi za uhai wake aliwahi kufanya kazi Jeshi la Polisi Kitengo cha Upelelezi katika mikoa mbalimbali.

Mbali na hilo pia alikuwa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pia amewahi kuwa mlinzi wa Rais katika utawala wa awamu ya kwanza wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Alisema alizaliwa miaka 60 iliyopita katika Kijiji cha Dalai wilayani Kondoa mkoani Dodoma ambapo ameacha mjane aitwaye Kuruthumu Mohammed na watoto watano.

Alisema mpaka mauti yanamfika alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya  Dalai Islamic Centre ambayo ilikuwa ikijihusisha na kusafirisha mahujaji kwenda nchini Makka pamoja na kuwa mmoja wa wamiliki wa shule za Zamzam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles