Na Mwandishi Wetu-ZANZIBAR
HATUA ya Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico, kutangaza mabadiliko ya kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi bila kushirikisha wawekezaji wa sekta ya utalii, sasa hatima yake ipo mikononi mwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Mbali na hilo, inaelezwa kuwa Waziri Castico amechukua uamuzi huo bila kushirikisha hata baadhi ya viongozi wenzake ndani ya Serikali pamoja na Baraza la Wawakilishi (BLW) kama sheria inavyotaka.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Mohamed Said Dimwa, alisema licha ya hali hiyo lakini bado kamati yake haijahusika na mabadiliko hayo ambayo huenda yakaleta hatari kwa Wazanzibari wengi kupoteza kazi kupitia sekta ya utalii.
Alisema uamuzi uliochukuliwa wa kuongeza mishahara kwa sekta binafsi ni wa Waziri Castico binafsi na si wa Serikali na huenda una lengo binafsi lililojificha ndani yake.
“Nasisitiza tena suala hili halijapita kwenye kamati yetu ya bajeti na kwa sababu suala hili ni kama lisingepita kwetu lingekwenda katika Kamati ya Sheria ndogondogo napo huko nami ni mjumbe lakini pia sijaliona tukijadili.
“Kwa hali hiyo kinachofanyika sasa ni kuomba Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa kumwandikia barua ili kuweza kujadili suala hili kwa haraka kwa kibali chake na kama tukiacha hali hii kuna hatari kubwa kwa wafanyakazi wengi hasa Wazanzibari kupoteza nafasi za ajira kupitia sekta hii.
“…siku zote tunasisitiza kukuza hali bora ya maisha kwa Wazanzibari kama Ilani ya Uchaguzi inavyotuelekeza, tusipochukua hatua za haraka kuna hatari ya kuwarudisha nyuma na kuzuka kwa malalamiko toka kwa wananchi,” alisema Dimwa.
Mshauri wa Rais
Kutokana na sintofahamu hiyo, MTANZANIA lilizungumza na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Uchumi, Balozi Mohamed Ramia, ambaye naye alikiri kusikia suala hilo huku akiahidi kulifuatilia suala hilo kwa undani.
“Hili suala ….. nitalifuatilia ili nione limekaaje,” alisema Balozi Ramia.
Hata hivyo, mmoja wa kiongozi wa SMZ ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema kuwa licha ya suala hilo kutishia hali ya uchumi wa Zanzibar tayari Rais Dk. Shein, amepewa taarifa huko alipo pindi atakaporejea nchini Julai 25, huenda akatoa uamuzi wa Serikali.
“Ingawa Rais (Dk. Shein) yupo nchini Uingereza kwa ziara maalumu, ila ninachokuhakikishia kila siku anapata taarifa ya kinachoendelea nchini. Na kuna hatari hata kiongozi anafanya haya mabadiliko huenda hata akapoteza kazi kama hakujipanga vizuri.
“Mapato ya Zanzibar kwa asilimia 80 yanatokana na sekta ya utalii, maeneo mengine huchangia kiasi lakini si kama sekta hii, hivyo ukiiyumbisha na watu kupoteza ajira kiuchumi Zanzibar itarudi nyuma kuliko ilipo sasa,” alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.
Katibu wa BLW
MTANZANIA lilimtafuta Katibu wa Baraza la Wawakilihi (BLW), Raya Issa Mselem, ambaye alisema kwa sasa anahitaji kufuatilia kwa undani ili kujua suala hilo kama limepita katika kamati ya bajeti ama la.
“Kwanza binafsi nilisikia tu tamko la Waziri mwenye dhamana (Maudline Cyrus Castico) kuwa kuna nyongeza ya mabadiliko ya mishahara kwa sekta binafsi sasa kujua kama limepita kwenye kamati hili sifahamu.
“Unajua hizi kamati za kisekta hata kama hazijadili suala hili lakini pia huangaliwa sera na sheria kwa kuona je, ana nguvu kisheria. Na kazi ya kamati ni kutoa maoni na ushauri kwa Serikali wafanye nini.
“Ila kwa kuwa suala hili sijalifuatilia sana siwezi kusema kama limejadiliwa ama la. Jambo la msingi kuangalia nguvu ya kisheria ambayo imepitishwa na Baraza la Wawakilishi ambalo ndilo lenye uwezo kwa mujibu wa sheria,” alisema Raya.
Waziri Abood
Alipotafutwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood, alisema kwa sasa bado wanaendelea kulifanyia kazi suala hilo kwa ngazi ya Serikali ikiwamo kukutana na wawekezaji wa utalii Zanzibar ili kusikia kilio chao.
Ingawa hakutoa ufafanuzi wa kina taarifa zinaeleza kuwa kesho Serikali itakutana na wawekezaji wa utalii ili kujadili suala hili na kutafuta ufumbuzi wa pamoja.
Waziri Castico
MTANZANIA lilipomtafuta Waziri Castico ili kujua msimamo wake kuhusu hilo, hakuwa tayari kuzungumzia na alipotafutwa kwa njia ya simu iliita bila kupokewa.
Hata hivyo, katika msimamo wake alioutoa wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na MTANZANIA, alisema kwa sasa Serikali inalifanyia kazi suala hilo na anaamini ufumbuzi utapatikana licha ya wadau kutoa maoni yao.
Inaelezwa kuwa suala hilo la mabadiliko ya mishahara kwa sekta binafsi alimshirikisha pia Waziri wa Utalii pamoja na fedha ambao hata wanapotafutwa ili kupata kauli zao hawako tayari kuzungumzia suala hilo.
Hali ya uchumi
Sekta ya utalii imekuwa ikichangia asilimia 7 ya pato la uchumi Zanzibar, ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed, alinukuliwa akisema pamoja na ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kuimarika, lakini bado ukuaji wa uchumi huo hauendani na ongezeko la idadi ya watu katika visiwa hivyo.
Alisema kasi yao ya ukuaji wa uchumi ipo karibu asilimia 6.7 na walioitarajia ni asilimia 7.2 kwa mwaka 2017, lakini anahisi ingekuwa zaidi ya hapo kwa vile ongezeko la idadi ya watu ambalo kwa sasa limefikia asilimia 2.8 ikiwa ni karibu na asilimia tatu.
“Sasa bado kasi yetu inakuwa lakini ninahisi kwamba ingekuwa zaidi ya kiwango hicho tulichokipangia, tunakuwa kwa asilimia 2.8 karibu tatu lakini ili kuweza kumudu mahitaji ya watu basi tunahitaji uchumi wetu ukuwe kwa asilimia 10 kupitia dira yetu ya maendeleo ya 2020 ambayo bado hatujaifikia,” alisema.
Mishahara
Serikali ilitangaza kuanzia Julai Mosi mwaka huu kuwepo kwa mabadiliko ya kima cha chini kwa wafanyakazi wenye mikataba ya maandishi kwa taasisi ndogo zitakazoainishwa kwenye kanuni kimeongezeka kutoka Sh 145,000 hadi 180,000.
Kwa wafanyakazi wenye mikataba ya maandishi imeongezeka kutoka kiwango cha sasa cha Sh 145,000 hadi 300,000.
Huku kwa vibarua wa kutwa wenye ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 10,000 hadi 30,000 kwa siku na kwa vibarua wa kutwa wasio na ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 7,000 na kufikia 25,000.