21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Utalii Utamaduni: Mashujaa Vita MajiMaji kukumbukwa Daima

FERDNANDA MBAMILA-SONGEA

 FEBRUARI 27  ya kila mwaka ni siku kubwa sana kwa watu wa Songea, Mkoani Ruvuma kwa sababu ndiyo siku ambayo wakoloni wa Kijerumani walimnyonga na kumkata kichwa kiongozi wa vita vya Maji Maji ambavyo vilipiganiwa kati ya mwaka 1905 – 1907 kupinga ukoloni wa Kijerumani nchini.

Kiongozi wa wananchi wa Ruvuma, Mbano Songea ambaye mji wa Songea umeitwa kwa jina lake alipinga kutawaliwa na Wakoloni wa Kijerumani akawahamasisha wenzake kuingia vitani ukiwa mwendelezo wa machafuko yaliyoanza Rufiji na Kilwa kupinga kutozwa kodi.

Mtafiti wa Makabila Mbalimbali nchini, Omela Musa anasema kuwa chanzo cha vita vya Maji Maji ilikuwa maonezi ambayo utawala wa Kikoloni ulionesha kwa watawaliwa.

“Watu walichapwa viboko kwa kosa lolote, hata kutolipa kodi na kufanyishwa kazi ngumu bila huruma,” anasema Mzee Musa.

Vile vile Watu hawa walipigana kupinga kukandamizwa na kulazimishwa na wakoloni wa Kijerumani namna ya kuishi, mazao ya kuzalisha na nani wa kumtumikia ikiwa picha kamili ya ukoloni mkongwe.


Askari wa Jeshi la Wanachi wa Tanzania wakiwa katika gwaride la maombolezo ya kuwakumbuka mashujaa wa vita vya Maji Maji.

Kumbukizi ya vita hii hufanyika kila mwaka tarehe 27 ambapo Makumbusho ya Taifa la Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaratibu shughuli hiyo katika mji wa Songea, mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma. 

Maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni kwa mwaka 2019 yanalenga katika kuenzi uthubutu wa mababu zetu waliopanda mbegu ya uzalendo, utaifa, amani, upendo na mshikamano wa Taifa letu.

Akizungumza katika tamashao hilo la Kumbukizi ya 112 ya Vita vya Maji Maji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda anasema kuwa, lengo la kumbukizi hii ni kuwakumbuka na kuwaenzi babu zetu waliokufa wakitetea maslai ya nchi yetu.

Mnamo Februari 27, 1907 mababu zetu wapatao 67 walinyongwa na Wajerumani mjini Songea na kuzikwa katika makaburi mawili yaliyopo katika Makumbusho ya Vita vya Maji Maji Songea, anasema Prof Mkenda katika hotuba yake ya mahudhui ya Kumbukizi ya Vita ya Maji Maji iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Lusius Mwenda.


Kaburi la Nduna Songea Mbano lililoko katika Makumbusho ya Maji Maji. Yeye alizikwa peke yake karibu na kaburi la haraiki la mashujaa wa vita vya Maji Maji

Anasema kumbukizi hii hutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika kutunza, kuenzi na kuendeleza uthubutu, uzalendo, amani na mshikamano, vitu ambavyo ni miongoni mwa urithi tuliorithi kutoka kwa mababu zetu na waasisi wa Taifa letu. Siku hii pia hutumika kuibua na kuendeleza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Ukanda wa Kusini hususan Mkoani Ruvuma.

Tangu mwaka 2011 tamasha hili limeshirikisha wageni kutoka Malawi, Msumbiji na Zambia ambapo machifu wa makabila ya Wangoni waishio katika nchi hizo hushiriki. Mwaka huu wa 2019 wageni watatu kutoka Malawi walijumuika pamoja na wenzao katika kumbukizi hiyo. Lengo kuu ni kutumia utalii wa malikale katika kuimarisha urafiki na ujirani mwema baina ya nchi yetu na mataifa mengine.

Vita vya Maji Maji vilianzia maeneo ya Kilwa ambapo kulikuwa na mtu anaitwa Kinjekitile Ngwale ambaye aliwashawishi watu kupambana dhidi ya mtutu wa bunduki wa Wajerumani waliokuwa wakiitawala Tanganyika kwa nguvu akiwaahidi kuwalinda kwa maji ya miujiza.

Kinjekitile anafahamika kwa kuyaunganisha makabila ya eneo hilo la kusini na kadri ujumbe wake ulivyozidi kusambaa, akachangia kuwa mtu wa kwanza kuleta utaifa Tanganyika. Aliwaambia wafuasi wake kwamba iwapo watatumia maji yake yaliyo na dawa, risasi za Wajerumani hazingewaingia ila zingegeuka kuwa maji ila wasitazame nyuma.

Kinjekitile Ngwale anafahamika kwa kuwa mwanzilishi wa vita vya Maji Maji, ingawa yeye mwenyewe alikufa muda mfupi baada ya vuguvugu hilo kuanza lakini hali hiyo haikuwakatisha tamaa wazalendo hao.

Vita vya Maji Maji vilianza mwaka 1905 na kuisha 1907 na vilikuwa mojawapo ya vita vikuu dhidi ya ukoloni barani Afrika. Vita hii ilikuwa kama moto katika nyasi kavu na kusambaa katika makabila ya Wamwera, Wangindo, Wapogoro, Wangoni, Wabena, Wasangu na wengine wengi wa mikoa ya kusini.

Jina la vita hii limetokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na Maji, punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani.

Kulingana na vitabu vya Historia inaaminika kuwa vita vya Maji maji vilichangia vifo vya watu wengi baada ya kuwadanganya kwamba maji yangewakinga dhidi ya risasi. Inakadiriwa kwamba kati ya watu 180,000 na 300,000 walifariki dunia wakati wa vita vya Maji Maji kutokana na mapigano na njaa.

Chifu wa Wagoni wakati huo Nkosi Mputa Gama bin Gwazerapasi alipopata taarifa kuwa kuna maji ya miujiza huko Kilwa, aliwatuma watu wake kwenda kuyaleta.  Maji hayo yalifikishwa kwenye Makao Makuu ya chifu Mputa Gama eneo liitwalo Maposeni.

Chifu Mputa Gama alikuwa na wasaidizi 12 walioitwa Manduna na mmojawapo alikuwa Nduna Songea Mbano ambaye alisifika sana na kuaminiwa na chifu kutokana na uhodari wake katika vita.

Nduna Songea Mbano alikuwa maarufu kuliko Manduna wenzake na hata Chifu Mputa Gama alikuwa anamtegemea sana katika kuwaongoza manduna wenzake na wapiganaji wa vita vya Maji Maji. Nduna Songea alitokea kupata umaarufu mkubwa ikilingalishwa na wenzake 11 kwa kuwa alikuwa na weledi na ustadi wa kuandaa mikakati ya kivita na kutoa maamuzi mazito yasiotetereka na kuyasimamia kikamilifu.

Mratibu wa Kamati ya Wazee wa Mkoa wa Ruvuma Mzee Kassimu Yasini anasema vita vya Maji Maji Mkoa wa Ruvuma vilianzia eneo la Maposeni katika Makao Makuu ya Chifu Mputa Gamatarehe 21/08/1905.

Karibu na eneo hilo kulikuwa na Padri Francis wa Peramiho ambaye alikuwa anawalazimisha Wangoni kuingia Ukristo jambo ambalo lilileta mgogoro mkubwa kati yake na wananchi kwani wengi walikuwa wamejiunga na Uislamu.

Padri huyo alinyongwa na Wangoni mwaka 1905. Wajerumani waliamuru Kibanda cha Chifu kichomwe moto hivyo kusababisha wazee kukasirika sana na kuamuru vita dhidi ya Wajerumani vianze.

Vita vilipiganiwa kwa nguvu sana, wakati Wajerumani walitumia mtutu wa bunduki Wangoni walitumia silaha zao duni za mishale, mikuki, mapanga na marungu.  Mzee Yasini anasema japokuwa walikuwa na silaha duni lakini wingi wao uliwasumbua Wajerumani ambao ilibidi waongeze nguvukazi ya kupambana na Wangoni.

Mzee Yasini anasema wakati vita hiyo ikiendelea Nduna Songea Mbano alikuwa amejificha kwenye pango kubwa lililopo kwenye mlima wa Chandamari na usiku alikuwa anakutana na askari wake nje ya pango hilo na kuwapa mafunzo zaidi ya kivita. Wakati mapigano yakiendelea Wajerumani walianza kumtafuta Nduna Songea kwa lengo la kufanya naye mazungumzo ya maridhiano.

“Katika vita hiyo Nduna Songea alitoa ushindani mkubwa kwa Wajerumani na alionesha ustadi mkubwa kwenye mapigano na sehemu zote ambazo Wajerumani walipigana” anasema Mzee Yasini.

Inaelezwa kuwa Wajerumani walipoona wanaendelea kupata madhara makubwa kutokana na vita hivyo, waliamua kuwakamata ndugu na familiaya ya Nduna Songea. Waliokamatwa ni pamoja na Chifu Mputa Gama na Manduna wengine ambao walifungwa gerezani kwa lengo la kumdhoofisha Nduna Songea. Baada ya kudhoofishwa jeshi lake Nduna Songea aliamua kutoka kwenye pango alikokuwa amejificha na kwenda kwa Wajerumani ili kutaka watu wake waachiwe huru. Kumbe hakujua ukatili mkubwa wa Wajerumani ambao walikuwa hawaheshimu wenyeji.

“Hakufanikiwa hata kidogo maana naye alikamatwa na kuwekwa gerezani na Wajerumani waliwahukumu wafungwa wote kunyongwa hadi kufa akiwemo Chifu wa Wangoni Mputa Gama,” anasema Mzee Yasini.

Kabla ya kunyongwa kwao wafungwa hao waliaamuriwa kuchimba shimo kubwa ambalo baadaye lilitumika kama kaburi lao. Shimo hilo walilichimba kwa muda wa miezi miwili.

“Wafungwa hao walinyongwa kwa zamu, wanne wanne katika eneo lililojengwa mnara wa kumbukumbu ya vita ya Maji Maji na kutupwa katika shimo walilolichimba wakiwa wamekufa. Wote 66 walizikwa ndani ya shimo hilo,” anasema Mzee Yasini.

Februari 27, 1907 ilikuwa siku ya majonzi na masikitiko makubwa kwa watu wa Ruvuma ambapo watu 66 wakiwemo askari walinyongwa kwa sababu ya kushiriki katika vita. Mashujuaa hawa walinyongwa nyuma ya eneo ambalo leo hii linajulikana kama “Songea Club”.

Kulingana na maelezo ya Chifu wa Wangoni aliyepo, Chifu Emmanuel Zulu, mtu wa mwisho kunyongwa miongoni mwa Wangoni alikuwa Nduna Songea Mbano ambaye aliuawa siku ya tatu.

Chifu Zulu anasema Wajurumani walijaribu kumnyonga kwa kamba Nduna Songea lakini alikata kamba ya kunyongewa mara tatu hivyo waliamua kumpiga risasi na kukata kichwa chake na kukipeleka Ujerumani ambapo hakijarudishwa mpaka leo.

“Tunaomba kichwa cha shujaa wetu kirudishwe Tanzania,”anasema Chifu Zulu.

Eneo walilozikwa mashujaa wa Vita vya Maji maji ni eneo muhimu kwa historia ya nchi yetu. Baada ya Uhuru (1961)baadhi ya wazee walianzisha harakati za kuwakumbuka mashujaa hawa. Walianza kufanya maombi yao ya maadhimisho katika eneo lililo karibu na eneo walilonyongwa wapiganaji hao.

Kwa hiyo, kuanzia mwaka 1980 Baraza la Wazee wa Kingoni lilianza kuadhimisha maombolezo ya mashujaa walionyongwa kila ifikapo tarehe 27 mwezi wa pili ya kila mwaka. Makumbusho haya yalifunguliwa rasmi tarehe 7/7/1980 kwenye sikukuu ya Saba Saba ikiwa ni kuadhismisha kuanzishwa kwa Chama cha TANU.

Kuanzia hapo makumbusho haya yaliendelea kutoa huduma chini ya usimamizi wa Mkoa wa Ruvuma na wazee wanaendelea kufanya maadhimisho ya siku ya Mashujaa katika eneo la Makumbusho haya kila mwaka. Tarehe 1/9/2005 makumbusho haya yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Tarehe 8 Desemba 2009 Makumbusho ya Maji Maji ilikabidhiwa rasmi kwa Makumbusho ya Taifa la Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mgeni Rasmi katika kumbukizi ya Mashujaa wa Vita vya Maji Maji mwaka huu 2019 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bibi Christina Solomoni Mndeme ambaye alielezea uthubutu wa mashujaa hao katika kutetea nchi yetu na kwamba unafanana kabisa na uthubutu aliokuwa nao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli katika kujenga uchumi wa Tanzania na kupambana na Mabeberu.

“Njia nzuri ya kuendelea kuwaenzi mashujaa hawa ni kuunga mkono na kutekeleza kwa vitendo dhana ya hapa kazi tu ya Mhe Dkt. Johna Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanania anayoitumia kuhimiza kila Mtanzania kufanyakazi kwa bidii, kulinda rasilimali za taifa, kupambana na kuzuia rushwa na madawa ya kulevya” anasema Bibi Mndeme .

Bibi Mdeme anasema kuwa maeneo ya malikale kama Makumbusho ya Maji Maji na mengineyo ni kumbukumbu za Taifa, vituo vya mafunzo na vivutio vya utalii.

Anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na wizara ya Maliasili na Utalii katika kuyahifadhi, kuyaendeleza maeneo hayo ili yatumike kama vyanzo vya ajira kwa sababu Sera ya Malikale inaruhusu sekta binafsi kuyamiliki na kuyaendeleza kiutalii.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma analipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushiriki kikamilifu katika kumbukizi ya 112 ya Mashujaa wa Vita vya Maji Maji ambapo lilifanya gwaride la heshima na kupiga mizinga ya heshima kwa mashujaa hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,814FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles