Utajiri wa Mo waporomoka kwa dola milioni 300

0
2295

Mwandishi Wetu-Dar es salaam

RIPOTI mpya iliyotolewa na Jarida maarufu linalofuatilia watu wenye ukwasi mkubwa duniani la Forbes, imeonyesha kuwa ukwasi wa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu kama Mo umeporomoka kwa Dola za Marekani milioni 300 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka 2020, Mo ambaye mwaka 2019 utajiri wake ulikuwa unakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 1.9 hivi sasa anamiliki dola bilioni 1.6.

Licha ya ukwasi wake kuporomoka, kijana huyo anayetambulika kama bilionea mdogo barani Afrika, hata hivyo amepanda kutoka nafasi ya 17 aliyokuwa akiishikilia mwaka 2019 hadi kufikia nafasi ya 16 mwaka huu.

Wakati Mo akiporomoka kwa Dola milioni 300, tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dangote yeye utajiri wake umeonekana kupanda mara dufu. 

Wakati ripoti ya Forbes ya mwaka 2019 ikimtaja Dangote kuwa na ukwasi wa Dola bilioni 4.3 ripoti ya mwaka huu imeonyesha amepanda hadi kufikia Dola bilioni10.1 akiendelea kushika nafasi hiyo hiyo ya kwanza.

Utajiri wa Dangote ambaye ni raia wa Nigeria na aliyewekeza pia hapa nchini kupitia kwanda cha simenti mbali  na kutokana na bidhaa hiyo pia unatokana na uwekezaji katika sukari na unga.

Nafasi ya pili katika orodha hiyo ya matajiri wa Afrika imeshikiliwa na bilionea Nassef Sawiris wa Misri ambaye ameonekana kupanda kutoka Dola bilioni 7.5 mwaka jana hadi kufikia dola bilioni 8 mwaka huu.

Nafasi ya tatu imeshikwa na watu wawili Mike Adenuga na Nicky Oppenheimer ambao wote wana miliki dola bilioni 7.7.

Bilionea Johann Rupert ameshika nafasi ya tano ($ bilioni 6.5), Issad Rebrab nafasi ya sita ($ bilioni 4.4), Mohamed Mansour nafasi ya saba ($ bilioni3.3), Abdulsamad Rabiu nafasi ya nane ($ bilioni 3.1), Naguib Sawiris nafasi ya tisa ($ bilioni 3). 

Kwa upande wa wanawake walioingia katika orodha ya matajiri 20 barani Afrika, ni pamoja na binti wa Rais wa zamani wa Angola, Jose Dos Santos, Isabel ambaye ameshika nafasi ya 13 akiwa na ukwasi wa dola bilioni 2.2 na Folorunsho Alakija kutoka Nigeria ambaye ameshika nafasi ya 20 akiwa na dola bilioni moja. 

NDOTO ZA MO

Pamoja na ripoti ya jarida hilo kuonyesha ukwasi wa Mo umeporomoka na wakati huo huo akipanda daraja, mfanyabiashara huyo mwaka jana mwezi Oktoba alipita katika wakati mgumu baada ya kutekwa na watu wasiojulikana  na kushikiliwa kwa takribani siku tisa na hata kutishia maisha na biashara zake kabla ya kuachiwa.

Pamoja na kupita katika hali hiyo bado amekuwa akitekeleza mipango ya kutanua biashara zake.

Mipango hiyo ni pamoja na kuongeza viwanda katika nchi mbalimbali hususani barani Afrika. 

Pia amekuwa na mazungumzo ya kina kuhusu kutanua biashara na viongozi kutoka nchi za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Afrika Kusini, Zambia, Uganda, Madagascar, Comoro.  

Katika mahojiano yake ya hivi karibuni Mo aliahidi kuwekeza Shilingi za Tanzania bilioni 500 hapa nchini na kutengeneza ajira za watu mbalimbali 100,000. 

Mo ambaye ni mpenzi wa mpira wa miguu akiwa amewekeza katika klabu ya kubwa ya Simba Sports Club, ameahidi pia kuwekeza mamilioni ya shilingi kwenye maendeleo ya mchezo huo akishirikiana na ubalozi wa Sweden nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here