MARA kwa mara kumekuwa kukifanyika tafiti mbalimbali duniani kuhusiana na vyuo vya elimu ya juu ambazo hutumika kuonyesha vinavyofanya vizuri kwa kipindi husika na vile vilivyoanguka.
Wanafunzi wengi vyuoni wamekuwa wakijikita katika kufanya tafiti mbalimbali wanapokuwa kwenye hatua ya elimu ya juu ambapo wasomi wanasema kuwa kwa asilimia kubwa kumekuwa hakuna mchango wowote ambao umekuwa ukiletwa na tafiti hizo kutoka kwa wanachuo.
Uingereza ni kati ya nchi ambazo vyuo kupitia wanafunzi wengi wamekuwa wakitumia mabilioni ya paundi kufanya tafiti zao ambazo wataalamu wanasema zimekuwa hazina chachu yeyote kwenye jamii.
Profesa Lord Nicholas ambaye ni mchumi katika chuo kikuu cha London, kupitia waraka wake auliotoa kwa vyuo vikuu nchini humo anasema kuendelea kufanya tafiti kwa kutumia njia zinazotumiwa hivi sasa na wanafunzi vyuoni hakutakuwa na matokeo yoyote chanya kwa chuo na taifa kwa ujumla.
Pia anawataka wafanyakazi wanaohusika na vitengo vya utafiti kuhakikisha kuwa wanawatathmini na kuwapima wanafunzi wanaotaka kuja kuomba kufanya utafiti kuliko kuacha vyuo vikuu kujisimamia vyenyewe.
Anasema vyuo vinapojisimamia vyenyewe na kuwasilisha tafiti zake kwa kutumia wasomi wenye mawazo yasiyokuwa na tija hakuwezi kuwa na faida kwa wengine zaidi ya manufaa ya chuo pekee.
Hata hivyo waziri wa elimu ya juu wa Uingereza, Jo Johnson, anasema utafiti ni muhimu kwa ustawi wa uchumi sanjari na kuinua kiwango cha elimu.
Hata hivyo, Lord Stern, ambaye anahusika na usimamizi na upimaji wa tafiti zinazofanywa na vyuo nchini Uingereza (REF), anasema tafiti ni kitu cha msingi ambacho kimekuwa kikisaidia kukua kwa taaluma.
Anasema pia zinasaidia jamii inayotegemea wasomi kutatua changamoto wanazokabiliana nazo licha ya kuwapo kwa madhaifu makubwa katika tafiti ambazo zimekuwa zikifanyika kwa miaka ya hivi karibuni nchini humo.
Anasema katika kipindi cha mwaka 2015/16, kiasi cha paundi bilioni 1.6 kimetumika kufanya utafiti kwenye vyuo vikuu ambacho kimetolewa na REF kusimamia mipango ya utafiti kwa miaka mitano mpaka 2020 au zaidi ili kuhakikisha wanafunzi pamoja na vyuo wanafanya taifiti zenye mwamko kwa jamii.
“Ni muhimu kuwa na utafiti wenye tija ili kuimarisha taalumua nzima ya Uingereza na kuhakikisha kunakuwa na mwamko mkubwa kupitia tafiti zinazofanyika.
“Tunahitaji kuona mwamko mkubwa zaidi kwenye tafiti kwani kumekuwapo na mlolongo mkubwa wa tafiti ambazo hata hivyo zimekuwa hazina faida yeyote kwa taifa na kujikuta serikali zikipoteza fedha ambazo zimekuwa zikitumika kusimamia tafiti hizo.
“Ukiangalia kwa miaka ya hivi karibuni vyuo vingi vimekuwa na tabia ya kufanya tafiti kwa ajili ya kushika nafasi za juu kwenye orodha ya vyuo bora duniani na Ulaya, lakini hakuna ubora katika tafiti wanazofanya wanafunzi wake,” anasema Stern.
Anasema ni vyema vyuo vikafanya tafiti za kusaidia kuinua taaluma kuliko kulipua kwa lengo la kuwania nafasi ya juu kwenye viwango vya ubora.
Aanavionya vyuo ambavyo vimejikita katika kufikiria suala la kuwa bora kwenye orodha kuliko kufanya tafiti zenye mashiko.
Changamoto chuo cha London
Mwaka 2014 katika orodha ya vyuo bora duniani, Chuo kiikuu cha London kilishindwa kutamba mbele ya vyuo vya, Oxford, Cambridge, Imperial.
Hata hivyo changamoto kubwa inayovikabili vyuo vingi vya Londoni ni kutokana na kujikita kwenye kutafiti wa masuala ya kiuchumi.
Ambapo kuanzia mwaka 2014 takribani tafiti 52,000 zimefanywa na wanafunzi wa vyuo vya Oxford, London na Cambridge zikihusu masuala ya uchumi na kuyapa kisogo mambo mengine.
Stern pia, anasema kuwa amekuwa kwenye mkakati wa kuishauri serikali juu ya kubadili muundo mpya wa ufanyaji tafiti kwenye vyuo vikuu kwa lengo la kuboresha na kuwa na matokeo chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.