30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

UTAFITI: NUSU YA WASICHANA HUOLEWA CHINI YA MIAKA 18

Na JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM

UTAFITI unaonyesha zaidi ya asilimia 50 ya wasichana katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Dodoma na Tabora wanaolewa kabla hawajafika umri wa miaka 18.

Katika Mkoa wa Iringa, ni msichana mmoja kati ya 10 na Dar es Salaam ni msichana mmoja kati ya watano.

Hayo yalibainishwa katika utafiti wa taifa kuhusu vichocheo na madhara ya ndoa za utotoni wa mwaka 2016 uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika la Plan International, Forward na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF).

Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti huo, mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Repoa, Dk. Lucas Katera, alisema utafiti huo uliwashirikisha watu 3,299 kutoka katika mikoa 10 yenye viwango vya juu, kati na chini vya ndoa za utotoni.

Alisema utafiti uligundua kwamba kichocheo kikubwa cha ndoa na mimba za utotoni ni umasikini, jambo ambalo husababisha familia zenye maisha magumu kuozesha watoto wao wa kike wakiwa na umri mdogo.

“Kutokana na hali hiyo, watoto wa kike hujikuta wakikatizwa masomo yao, hivyo kuishia kuwaoza kama njia ya kujipatia mali kupitia mahari inayolipwa kwa familia ambayo mara nyingi ni ng’ombe au fedha taslimu.

“Pia mila na desturi katika makabila mbalimbali kama vile sherehe za matambiko, ngoma za kimila na ukeketaji kwa watoto wadogo, huwa ni ishara kwamba tayari kuolewa na kukubalika kama wake,” alisema Dk. Katera.

Aidha, alisema hali ya kutokuwa na usawa wa kijinsia kati ya wasichana na wavulana, hususani majumbani, inahamasisha ndoa za utotoni kwa sababu mabinti hawana thamani ya kiuchumi zaidi ya mahari na elimu haichukuliwi kama kipaumbele kwao.

Dk. Katera alisema inakidiriwa watoto 36 kati ya 100 huolewa kabla ya kufikisha miaka 18 na wengine 27 kati ya 100 hupata mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la Plan International – Tanzania, Jane Mrema, alisema ripoti hiyo imeonyesha jinsi gani nafasi ya watoto wa kike haionekani kwani takwimu zinazowahusu haziendani na wakati.

“Tanzania hakuna takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa changamoto anazopata msichana kutokana na ndoa za utotoni jambo lililopelekea Plan International kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kufanya utafiti huu,” alisema Jane.

Alisema shirika hilo litaendelea na harakati za kupigana na tatizo hilo na kwamba katika mpango kazi wa miaka mitano kuania 2017 hadi 2022, wanakusudia zaidi ya wasichana milioni moja duniani kuwezeshwa kujitambua na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika suala la maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles