26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

‘Uspecial One’ haukumnusuru kutimuliwa Chelsea

mourinhoADAM MKWEPU NA MITANDAO

KAMA kuna jambo ambalo lilikuwa gumu kwa mashabiki wa klabu ya Chelsea kulipokea, ni taarifa ya kufukuzwa kwa kocha wao, Jose Mourinho.

Lilikuwa jambo la ghafla lakini yote kwa yote huo ndio ulikuwa uamuzi sahihi uliochukuliwa na bodi ya klabu hiyo kutokana na matokeo mabovu.

Hiyo ilikuwa njia pekee kwa Wanadarajani ambao wapo nafasi ya 16 wakiwa na pointi 15 tofauti ya pointi 20 dhidi ya vinara, Leicester City.

Chelsea hadi sasa imepoteza michezo tisa na uamuzi wa bodi ya Chelsea chini ya mmiliki wake, Roman Abramovich, ulichukuliwa baada ya mabingwa hao watetezi kufungwa 2-1 Jumatatu iliyopita na Leicester City.

Mechi ambazo Chelsea wameshinda ni tatu; dhidi ya Aston, West Brom na Arsenal.

Matokeo mabovu yalionekana kumshtua Mourinho na kumpa wasiwasi ambapo ilimfanya kutamka hadharani kwamba anahujumiwa na baadhi ya wachezaji wake, huku mmoja wa wachezaji muhimu wa klabu hiyo, Cesc Fabregas, akiwataka wenzake kucheza kwa bidii kulingana na mshahara wanaolipwa.

Ni miezi saba tu sasa imepita tangu Chelsea itwae ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini msimu huu wameanza vibaya na hawana dalili ya kutetea ubingwa wao.

Mbali na kufukuzwa kwa Mourinho katika klabu hiyo hali kama hiyo iliwahi kumtokea Robert Di Matteo aliyeshinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 lakini akaonyeshwa mlango wa kutokea kutokana na matokeo mabovu.

Tangu kutwaa ubingwa wa England kwa kuifunga Crystal Palace Mei mwaka huu, Mourinho ameweza kudumu Chelsea kwa siku 227.

Inaonekana jambo la ajabu Chelsea kumtimua Mourinho aliyeiongoza timu hiyo kunyakua mataji mbalimbali ikiwemo msimu huu kuivusha hatua ya mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya na kabla ya msimu kuanza kusaini mkataba mnono wa miaka minne.

Jitihada zake zinaweza kuwa sababu ya mmiliki wa klabu hiyo, Abramovich kuwa tayari kumpa muda zaidi licha ya mwelekeo mbovu wa timu.

Unafikiri kwanini mmiliki huyo alikuwa na imani ya kutosha juu ya kocha huyo ingawa hakuwa na matokeo mazuri? Ni juu ya ahadi zake kwa Abramovich baada ya kuzungumza na baadhi ya wachezaji mapema kabla mambo hayajaanza kuharibika.

Mara kadhaa Abramovich amekuwa akimkingia kifua Mourinho kutokana na matokeo mabovu huku akisema klabu hiyo haina mpango wa kumtimua.

Lakini kwa Mourinho, matokeo mabovu yamekua yakimtesa na kwa kiasi fulani akiwahusisha waziwazi wachezaji wake na matokeo hayo mabovu.

Mathalani katika mchezo dhidi ya Leicester City, Mourinho alisema wachezaji wake wamemsaliti na wanamhujumu kwani wanachokifanya mazoezini si kile ambacho wanakifanya uwanjani.

Hatua hiyo ni baada ya kuona wapo baadhi ya wachezaji katika kikosi chake wamepoteza imani naye kutokana na kucheza bila kufuata maelekezo yake.

Aidha, mbadala wa kocha huyo ni changamoto kubwa kwenye klabu hiyo kwa kuwa makocha wachache wanaweza kuufikia uwezo wake katika ushindani wa makombe na kutumia muda mwingi kuwa katika kiwango cha juu.

Miongoni mwa makocha wanaotajwa kumridhi Mourinho Chelsea ni Guus Hiddink, Diego Simeone, Pep Guardiola na Brendan Rodgers.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles