MAISHA ya hayati Robert Mugabe yalikuwa yamegubikwa na sura tofauti tofauti. Ifuatayo ni sehemu tu ya mambo ambayo huenda hukuwa unayajua kuhusu Mugabe
HAPENDI KUSHINDWA Alipokuwa kijana, Mugabe alikuwa hodari katika mchezo wa tenisi.
Kulingana na aliyekuwa mwalimu katika shule ya Wakatoliki alikosomea Mugabe siku aliposhindwa katika mchezo huo, aliitupa raketi yake chini kwa hasira.
Aliwahi kukiri kuwa hakuwa mzuri katika mchezo wa kandanda alipokuwa mdogo, ila baadae alianza kupenda kuutazama mchezo huo.
SHABIKI WA CHELSEA, BARCELONA
Aliwahi kusema kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa klabu za mataifa ya Ulaya za Chelsea na Barcelona.
KUFA NA KUFUFUKA
Wakati akihojiwa kuhusu afya yake alipotimiza miaka 88, alisema;” Nimekufa mara nyingi-hapo ndipo nimemshinda Yesu Kristo. Yesu alikufa mara moja, na akafufuka mara moja,”
MAAJABU YA DINI
Ingawa baba yake na mama yake Bona walimlea kwa kuzingatia maadili ya kanisa la Katoliki,na hata kusoma shule hizo lakini alipohojiwa na kituo cha habari cha Afrika Kusini, SABC, miaka michache iliyopita, alisema kuwa yeye si Mkristo anayetumikia dini kwa sana.
VIFO VYA KAKA ZAKE
Wakati akiwa mdogo alipoteza kaka wawili waliokuwa umri wa mika 10.
Mmoja alikufa kwa kunyweshwa sumu na mwingine alifariki muda mchache baada ya baba yao kuitelekeza familia.
ATELEKEZWA NA BABA
Januari, 2014 katika siku ya mazishi ya dada yake, Mugabe aliwataarifu waombolezaji kuwa mwaka 1934 baada ya kaka yake Michael kufariki, baba yake alianzisha familia mpya na kuzaa watoto wengine.
SHAHADA SABA
Mugabe alikuwa na shahada saba za chuo kikuu kati ya hizo sita alizipata wakati akiwa gerezani.
Shahada hizo ni pamoja na elimu, uchumi, utawala na sheria.
Nyingine alizipata kutoka Chuo Kikuu cha London (external program) alipokuwa katika Gereza la Salisbury.
SHAHADA ZAKE ZA
HESHIMA ZILIFUTWA
Baada ya kukorofishana na nchi za Magharibi wakimtuhumu kwa uvunjaji wa haki za binadamu baadhi ya shahada zake za heshima hazitambuliki.
Mfano Mradi wa Kudhibiti Njaa ulimpokonya tuzo yake ya mwaka 1998 (Award of the Africa Price for Leadership for the Sustainable end of Hunger).
Pia vyuo vikuu vikiwamo vya Michigan, Massachusetts na Edinburgh vilimnyang’anya shahada za heshima.
MTOTO WAKE NA SALY Mtoto wa pekee aliyezaa na mke wake wa kwanza, marehemu Saly Hayfoim Michael Nhamodzenyika
alifariki dunia mwaka 1966 akiwa na umri wa miaka mitatu kutokana na ugonjwa wa malaria.
Alitaarifiwa juu ya kifo cha mtoto wake huyo akiwa gerezani na hakuruhusiwa kuhudhuria mazishi yake.
ALIPATA MTOTO MWINGINE AKIWA NA MIAKA 73
Ana watoto watatu na mke wake wa pili, Grace Marufu, aliyekuwa karani wake. Mtoto wao wa tatu alizaliwa 1997, mwaka mmoja baada ya wao kufunga ndoa.
UHUSIANO NA GRACE
Mugabe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Grace wakati mke wake akiwa mgonjwa wa kansa kabla ya baadae kufariki.
Ilipogundulika kuwa Grace alikuwa mjamzito kisha kujifungua mtoto alipuuzia mashambulizi ya Wazimbabwe na akaamua kumuoa mwaka 1996.
ALISAFIRI ULAYA LICHA YA VIKWAZO
Licha ya vikwazo alivyokuwa amewekewa na nchi za Magharibi, mwaka 2013 Mugabe alisafiri kwenda nchini Italia.
Umoja wa Ulaya (EU)
ilitoa marufuku ya kuingia nchi yoyote mwanachama wake lakini Mugabe alitinga Italia kwa mwavuli wa dini wakati wa sherehe za kuwekwa wakfu Kiongozi wa sasa wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.
MZUNGU ALIMSAIDIA KUTOROKA
Alipoachiwa kutoka kifungoni na wakoloni, alisaidiwa na mzungu kukimbia Zimbabwe.
Mzungu huyo alimsaidia kuvuka mpaka kuingia Msumbiji ambako alikwenda kujiunga na Jeshi la Ukombozi.
MSIMAMO DHIDI YA USHOGA
Mtazamo wake juu ya ushoga si jambo la kushangaza. Mugabe anawachukia mashoga na hayani baadhi ya maneno yake kuhusu vitendo vya ushoga: “Ukiwachukua wanaume wawili na kuwafungia ndani ya chumba kimoja kwa muda wa miaka mitano na kuwaambia wapate watoto na wakishindwa kufanya hivyo basi ni bora kuwakata vichwa vyao.”
SHABIKI WA KRIKETI
Alidhihirisha hadharani kupenda mchezo wa kriketi. Alipata kuwa mlezi wa jumuiya ya mchezo wa kriketi wa Zimbabwe na nyumba yake ipo karibu na uwanja wa michezo wa Harare.
“Kriketi inafanya watu wawe wangwana, na pia inawafanya watu kuwa wema,” Mugabe alisema miaka kadhaa baada ya Zimbabwe kujinyakulia uhuru.
“Nataka kila mtu acheze kriketi Zimbabwe; nataka nchi ya Zimbabwe iwe nchi ya wangwana.”
MAZOEZI NA VYAKULA VYA KIENYEJI
Mugabe alipenda kufanya mazoezi na miaka sita iliyopita alisema;
“Mimi hujihisi mgonjwa wakati sijafanya mazoezi ya viungo vya mwili,”
Alisema alikuwa anaamka kati ya saa kumi na kumi na moja alfajiri.
Siri nyingine ya maisha yake marefu alisema ni kupenda kwake sana ‘sadza’ – chakula cha kienyeji kinacholiwa sana Zimbabwe, na ambacho kina virutubisho vingi muhimu. Vilevile alikuwa havuti sigara, ingawa alikuwa anakunywa pombe kidogo anapokula chakula cha jioni.
ALIMPENDA CLIFF RICHARD KULIKO BOB MARLEY
Inaelezwa kuwa wakati wa maandalizi ya kusherehekea uhuru wa Zimbabwe 1980, Mugabe hakumtaka mwimbaji Bob Marley aalikwe kutumbuiza watu, ila alimtaka muimbaji maarufu wa Uingereza, Cliff Richard. Pia alikuwa anampenda mwanamuziki, Jim Reeves.
AONEKANA KATIKA FILAMU
Katika filamu ya mwaka 2005 ya American Thriller (The Interpreter) iliyochezwa na Sean Penn na Nicole Kidman, Mugabe anaonekana akizungumzia njama ya mauaji ya kisiasa, baadae filamu hiyo ilipigwa marufuku nchini Zimbabwe.
MPENZI WA NGUO MARIDADI
Mugabe alikuwa anapenda sana suti zinazoutosha mwili wake sawasawa na tai zinazofanana na kitambaa.
Alikuwa akiwavutia sana wanamitindo nchini Zimbabwe kwa mavazi yake.
KWAME SHUJAA WAKE
Inaelezwa Mugabe alipenda siasa akiwa Ghana alipokuwa mwalimu; mahali alipokutana na mke wake wa kwanza, Sally Hayfron.
Aliporudi Zimbabwe, aliwaambia wananchi jinsi Ghana ilivyojinyakulia uhuru na jinsi uhuru ulivyo kitu kizuri.
Katika mahojiano mwaka 2003, Mugabe alisema: “Niliwaambia pia kuhusu Kwame Nkrumah jinsi alivyojitolea na kuiongoza Ghana kupata uhuru; Kwame aliwaambia wananchi wa Ghana kuwa Ghana haingekuwa nchi huru bila ya jitihada na kujitolea kwa kila mtu”.
‘BIRTHDAY’ ZAKE KUFURU
Mugabe alikuwa akifanyiwa kumbukizi ya kuzaliwa na chama chake kwa uzito mkubwa.
Alikuwa akiandaliwa zawadi kubwa mno na mfano mmoja wapo ni kumbukizi ya mwaka 2014 wakati alipotimiza miaka 90 ambapo alipokea zawadi ya kiti chenye madini ya dhahabu uzito wa tani moja na almasi.