33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

USIVUKE MWAKA 2017 NA MARAFIKI HAWA – 2

marafiki-wabaya

Na ATHUMANI MOHAMED

MAISHA yanahitaji busara ya hali ya juu. Unaweza usione umuhimu sana wa jambo hilo, lakini wakati fulani tatizo likishajitokeza ndipo utakapogundua kuwa kuna makosa ulifanya kutokana na kutotilia maanani jambo fulani.

Lakini katika yote, marafiki ni muhimu sana kwenye maisha yetu, kupitia wao tunaweza kusogea au kuanguka kwa namna moja ama nyingine.

Wiki iliyopita tulitangulia kuona mambo kadhaa. Leo tunamalizia sehemu ya mwisho ambapo pia tutaangalia mambo ya msingi kuzingatia katika kipindi hiki cha sikukuu.

WASALITI

Unaweza kuwa na rafiki yako ambaye mnasaidiana katika mambo mbalimbali. Unampenda kwa dhati, upo naye bega kwa bega kwenye matatizo yake, wakati fulani naye anakusaidia katika mambo yako.

Urafiki wenu umekomaa sana na ni msaada mkubwa hata kwenye matatizo yako ya kifamilia. Lakini baada ya muda unakuja kugundua kuwa mwenzako anakusaliti.

Aidha anapeleka maneno ya uongo kwa mpenzi wako, mke, mume au rafiki yako mwingine ama anaweza kuwa anapeleka maneno ya uchonganishi kwa jamaa zako na wakati mwingine kwa bosi wako ofisini.

Rafiki wa namna hiyo ni msaliti na kwa hakika hafai hata kidogo kuwa na wewe katika mwaka unaofuata. Nafasi uliyompa katika mwaka uliopita inatosha. Mwaka mpya uwe na mtazamo mpya.

Rafiki huyo mwache hukuhuku mwaka 2016, hakufai kuvuka naye kwenda naye mwaka 2017 maana ni kirusi hatari kwenye maisha yako.

 

WASIO NA MALENGO

Unaweza kuwa na rafiki ambaye unampenda sana, lakini maisha yake hayana dira. Si kwamba hana kazi au maisha yake ni magumu tu, hapana. Si mtu wa malengo.

Stori zake, wakati wote ni za starehe tu. Anapenda kukupa habari juu ya klabu mpya iliyofunguliwa mjini. Mtu wa namna hii bado hajamaliza mambo yake.

Mwache na mitazamo yake hiyo. Si ajabu kuna wakati ulijaribu hata kumshauri kwa namna moja ama nyingine ili abadili mtazamo wake, lakini anakuona kama umechelewa maisha.

Huyo kwa hakika hakufai hata kidogo. Kaa naye mbali. Kistaarabu tu kwa ajili ya maisha yako yajayo. Kamwe usikubali mtu akawa kikwazo cha mafanikio katika maisha yako.

VIKAO VYA POMBE

Inawezekana unatumia pombe na rafiki yako naye ni mpenzi wa pombe. Lakini hiyo haikufanyi muda wote ufikirie au uwe maeneo ya kunywa pombe.

Kuna wakati kweli unaweza kukutana na rafiki zako baa na mkawa na mazungumzo ya hapa na pale kwa lengo la kustarehe na kubadilishana mawazo.

Lakini tatizo kuna wale ambao muda wote wanawaza pombe. Ukiona simu ya rafiki yako huyo atakuwa anataka mkutane baa!

Wakati fulani anaweza kuwa ana uhitaji wa jambo fulani au anataka mjadiliane jambo, lakini kwake ni mwiko kufanya mazungumzo sehemu za vinywaji baridi. Anawaza pombe tu.

Hata kama ananunua yeye, lakini mtu wa kupenda sana pombe si mzuri, maana atakuingiza kwenye matumizi makubwa ya fedha na kukumbana na madhara ya ulevi.

Kwa kawaida ulevi si tabia nzuri kwa mtu mwenye malengo ya kufanikiwa kimaisha. Si tatizo kunywa pombe kwa kiasi, lakini kuzidisha ndiyo tatizo.

Unaweza kupanga ratiba nzuri ya kukaa mbali na unywaji wa pombe kupindukia, lakini marafiki wakakufanya uwe mlevi usiye na thamani na ukaharibu maisha yako.

Rafiki wa aina hiyo, kaa naye mbali. Atakuharibia maisha yako. Mwache hukuhuku mwaka 2016, ingia mwaka mpya na mtazamo mpya, ukiangalia marafiki wapya wenye mitazamo ya kimaendeleo zaidi.

Wiki ijayo nitakuletea mada inayozungumzia aina za marafiki unaopaswa kuwa nao katika mwaka mpya wa 2017.

Nawatakieni heri ya Krimasi na maandilizi ya mwaka mpya, panapo majaliwa yake Jalali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles