27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

USILAZIMISHE MAPENZI, KAMA HUMPENDI KAA PEMBENI

WATU wengi hawapendi kuambiwa ukweli, lakini ilivyo ni kuwa, kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi.

Kama ndivyo, kwanini uwe mtumwa? Huna sababu ya kuingia katika uhusiano tata, ambao mwisho wa siku utaishia kulia huku wa kukubebembeza akikosekana.

 

UNAMPENDA?

Suala la mapenzi huhusisha moyo zaidi, moyo wako ndiyo mwamuzi wa mwisho katika hilo, hata siku moja usikubali kulazimisha moyo wako kwa mtu ambaye hujaridhia. Achana na imani kwamba ukimkataa kijana fulani basi bahati inaweza kukupita, nani amekudanganya?

Suala la kuolewa halina bahati, Mungu mwenyewe ndiye mpangaji, unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa?

Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi. Mapenzi ni nguzo katika maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako.

Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe. Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda?

Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi. Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye!

Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi ndugu zangu. Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla.

Hii inamaana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana, na hazima utamkaribisha.

Kuna kule kusema ‘unafikiria’ kwa lengo la kutokujionyesha ni rahisi, hiyo ni sawa lakini siyo kwamba kweli unataka kufikiria kumpenda. Kama moyo wako hautaki, usilazimishe.

 

HUWEZI KUJIFUNZA KUPENDA

Baadhi ya wasichana akitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanamume huyo.

Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanamume huyo. Baada ya wazo hili kuingia akilini, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa.

Usikubali kuingia katika ndoa ya aina hii hata siku moja. Mwisho wa siku utajikuta ukilia. Kamwe huwezi kujifunza kupenda.

 

MADHARA YA KULAZIMISHA PENZI

Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndiyo msingi wa uhusiano.

Kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote. Hayo ndiyo mapenzi ya kweli, siku zote hujisikia mwepesi na huru kwa mwenzako.

Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? Ni matatizo tupu.

 

FIKIA MAAMUZI

Usijaribu kuingia katika mkumbo wa kujifunza kupenda, ni jambo gumu ambalo huweza likaharibu maisha yako kabisa.

Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo.

Je, unapenda kujifunza masomo haya zaidi kupitia group la WhatsApp la Love Moment? Kama ndivyo karibu inbox, andika ujumbe wako ukitaka kujiunga na kundi hilo, nasi tutakuunganisha.

 

Jiandae kupokea kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA, kitaingia mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles