24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ushuhuda wa kusikitisha mwanamume aliyeoa mwanamke aliyekeketwa

Na Norah Damian, Mtanzania Digital

Stanley Athanas (si jina lake halisi) aliposimama kuchangia mjadala wa ukatili wa kijinsia alivuta hisia za washiriki; wapo walioangua kicheko na wengine walionekana wakisikitika baada ya kusikia anayoyapitia.

Wanawake walisikika wakisema ‘huo ndio ukweli’, ‘semeni tupone jamani’ huku wanaume wakisema ‘kwakweli tunaipata fresh’.

Ofisa Maendeleo wa Kata ya Mzinga, Oliver Gabriel, akizungumza wakati wa mkutano uliohusisha viongozi wa kata kujadili namna ya kuzuia ukeketaji.

Mjadala huo ulioshirikisha viongozi wa Kata ya Mzinga, Manispaa ya Ilala ulijikita kujadili vitendo vya ukatili hasa ukeketaji wakati huu ambapo ni msimu wa utekelezaji mila mbalimbali kwa baadhi ya jamii hapa nchini.

Imezoeleka kuwa wanawake na wasichana waliokeketwa ndio wanaopata madhara ya kudumu kwenye maisha yao kama vile kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua, kupoteza maisha, kuathirika kisaikolojia na mengine lakini madhila yaliyoelezwa na mwanamume huyo yaliwashangaza wengi.

Mwanamume huyo anasema amekuwa akipata taabu wakati wa tendo la ndoa kwa kudai kuwa anatumia nguvu nyingi kumridhisha mkewe.

“Nikitaka kufanya tendo la ndoa mpaka ninywe pombe nilewe ndio nitaweza kumtimizia haja zake mke wangu…naumia hadi mbavu.

“Naomba sana watu waelimishwe faida na hasara za kukeketa, wakishaelewa tatizo litakwisha na sheria nayo ikaze uzi,” anasema.  

Kilio cha Athanas kinaungwa mkono na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzinga, Nyaikoba Ryoba, ambaye anaufananisha ukeketaji sawa na ulemavu na kukiri kuwa mhanga mkubwa wa kitendo hicho ni mwanamume.

“Tujaribu kupinga ukeketaji hauna maana, katika Mtaa wa Mzinga nikisikia kuna jambo la namna hiyo nikabaini mimi naanguka na wewe moja kwa moja ili siku nyingine usifanye vitu vya namna hiyo,” anasema Ryoba.

Mwenyekiti huyo anawataka wananchi kutoa taarifa za viashiria vya ukeketaji ili kuwaokoa wasichana.

“Usimfanye mtu kuwa mlemavu mbele ya safari ya maisha yake, mkisikia togwa inapikwa toeni taarifa,” anasema Ryoba.

Mshiriki mwingine katika mjadala huo na mkazi wa Kata ya Mzinga, Maryselina Rwiza, anaiomba Serikali na wadau kuendelea kutoa elimu kubadilisha mitazamo ya jamii kuhusiana na vitendo vya ukeketaji.

HALI ILIVYO

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia inaonyesha vitendo vya ukeketaji bado vinaendelea kufanyika katika baadhi ya mikoa nchini huku likionekana kuwa zaidi ya mila na desturi kama ilivyozoeleka.

Kulingana na ripoti hiyo, ukeketaji unahusishwa na uuzaji wa viungo kwa wafanyabiashara wakubwa wa madini na samaki ambao wanaamini kuwa vinaweza kutumika kuongeza wingi wa madini na samaki.

Viungo hivyo huuzwa kati ya Sh milioni 1 hadi Sh milioni 20 kutegemeana na wingi.

Katika Kata ya Mzinga viongozi wanakiri ukeketaji upo katika eneo hilo kwa sababu tayari kuna baadhi ya mabinti waliokimbia familia zao kwa kuepuka kukeketwa.

Mwezeshaji katika mjadala huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi, anasema hivi karibuni walifanikiwa kuwaokoa watoto watatu waliokuwa wanataka kukeketwa.

“Baada ya kuona viashiria vya ukeketaji walikimbilia kwa mtu waliyeamini watakuwa salama, mmoja amemaliza darasa la saba, wawili wapo kidato cha kwanza. Ushauri wangu iwepo kampeni maalumu inayoelekeza mtoto akiona viashiria vya kukeketwa afanye nini, hii itasaidia watoto wengi kutokeketwa,” anasema Bishagazi.

Diwani wa Kata ya Mzinga, Bob Isack, anasema mjadala huo ni mojawapo ya mikakati waliyojiwekea kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukeketaji hasa wakati huu ambao ni msimu wa utekelezaji mila mbalimbali kwenye baadhi ya jamii nchini.

“Nina taarifa nyingi na wakati mwingine tunaamka saa 7 usiku, kikinuka siwezi kusema wewe ni mpigakura wangu, kitajulikana baadaye, tujitahidi kuhakikisha tunapunguza haya mambo…mambo ya kura yatafuata baadaye,” anasema Isack.

Viongozi hao wameazimia kuwachukulia hatua watakaoshuhudia vitendo vya ukatili bila kutoa taarifa kwa wakati huku pia wakiendelea kutoa elimu kwa jamii.

Ofisa Maendeleo wa Kata ya Mzinga, Oliver Gabriel, anasema wamejipanga kupambana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto hasa vya ukeketaji.

“Tumejidhatiti kutoa elimu na tutawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo,” anasema Oliver.

Polisi Kata wa Mzinga, Inspekta Peter Malonga, anasema wanamtafuta ngariba anayekeketa katika eneo hilo na kwamba watahakikisha anapatikana.

Anawataka wananchi kutoa taarifa polisi pindi wanapowaokoa wasichana waliokimbia kukeketwa ili wachukuliwe na kupelekwa sehemu salama.

Mjadala huo uliandaliwa kwa ushirikiano na uongozi wa Kata ya Mzinga, Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Wildaf) na kushirikisha wajumbe wa nyumba kumi, wenyeviti wa mitaa, viongozi wa dini, wazee maarufu, mratibu wa elimu, viongozi wa jumuiya za CCM, baraza la kata, viongozi wa Vicoba, kituo cha taarifa na ulinzi shirikishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles