Na Christian Bwaya,
TUNAWAKUMBUKA walimu waliokuwa na ushawishi kwa wanafunzi katika shule tulizosoma. Hawa ni walimu walioheshimiwa na wanafunzi hata kama walimu wengine walidharauliwa. Neno lao lilitosha kuwatuliza wanafunzi katika nyakati za sintofahamu.
Uwezo huu wa kusema kitu kikasikika ndio tunaouita ushawishi. Hakuna mwalimu asiyependa kuwa nao. Kila mwalimu anatamani asikilizwe. Mazingira yanapomwonesha kuwa hana ushawishi ni rahisi kwake kutumia nguvu kujaribu kurejesha sauti anayoamini ni lazima awe nayo.
Tuliona namna mbili zinazoweza kumhakikishia mwalimu ushawishi. Kwanza, umahiri kazini. Mwalimu anayependa kazi yake ana uwezekano mkubwa wa kuwa na ushawishi kuliko mwalimu mzembe, mvivu asiyeoonekana kupenda kazi yake. Lakini pili, heshima kwa wanafunzi. Mwalimu asiyewaheshimu wanafunzi wake atakuwa na wakati mgumu kuheshimiwa. Tulisema, huwezi kuheshimiwa kama wewe mwenyewe hujiheshimu. Lazima uwaheshimu wanafunzi kwa kusema nao kwa staha hata pale wanapokuwa wamekosea. Ukimheshimu mwanafunzi atakulipa heshima.
Wafundishe kwa vitendo
Huwezi kuwaadhibu wanafunzi kwa kufanya unayoyafanya wewe. Mwalimu anayetukana wanafunzi kienyeji, kwa mfano, anakosa uhalali wa kuwaadhibu wanafunzi wanaojaribu kuwa kama yeye. Kadhalika, mwalimu mhuni anayeonekana mtaani akifanya mambo yasiyokubalika kwenye jamii. Hali hii ya walimu kutokuwa makini na tabia zao imeanza kuwa ya kawaida kwa walimu vijana. Labda kwa kutokufundishwa chuoni, ‘ticha’ anajikuta akifanya mambo yanayomfanya awe sawa na wanafunzi anaowafundisha.
Mwalimu wa namna hii asiye na tofauti na mwanafunzi anajipotezea uhalali wa kumwonya mwanafunzi kwa kufanya kile kile anachokifanya yeye. Dalili kwamba mwalimu umepoteza uhalali na heshima yako ni pale wanafunzi wanapoanza kukuchukulia kama mtu wa kawaida. Walimu wenzako wanaweza kusalimiwa kwa heshima, lakini wewe hutasalimiwa. Walimu mwenzako wanaweza kumwita mwanafunzi ana mwanafunzi akaitikia, lakini wewe usiye na uhalali wa kimaadili ukaita na wanafunzi wakajifanya hawajasikia.
Ukitaka kuwa na ushawishi kama mwalimu, fundisha wanafunzi kwa vitendo. Mwenendo wako kama mwalimu uzungumze kuliko mahubiri ya kimaadili unayoyatoa kwa wanafunzi. Sema kile unachokiishi.
Hata hivyo, usitake kuonekana wewe ni mkamilifu. Wanafunzi hawavutiwi na tabia ya ukamilifu. Wakati fulani kuonesha baadhi ya mapungufu uliyowahi kuwa nayo hukuongezea ushawishi. Kukiri mapungufu yako ya kibidamu huongeza hali ya watu kukuamini kuliko kujifanya wewe ni mtu wa pekee.
 Watie moyo kuliko kuwakosoa
Unaweza usiwe mwalimu unayewatukana wanafunzi lakini ukawa mwalimu mwenye maneno magumu kama vile kuwakosoa, kuwashambulia, kuwakejeli kwa hali waliyonayo na tabia nyinginezo zinazolenga kushambulia hadhi zao.
Hakuna binadamu anapenda kuhusiana na mtu anayemshusha hadhi yake. Kwa kawaida, huwa tunakata mawasiliano na mtu anayetufanya tujisikie hatuna maana yoyote. Maneno magumu yasiyowajenga wanafunzi wako yanajenga ukuta mkubwa kati yenu. Hali hii inakupunguzia ushawishi wako.
Mwanafunzi huhamasika kumsikiliza mtu anayemtia moyo hata katika mazingira ambayo angestahili kukosolewa na kushambuliwa. Kutiwa moyo kunamchangamsha na kumfanya ajiamini. Mtu anayejiamini ni mwepesi kuambilika.
Kama mwalimu, unahitaji kufanya bidii ya kubadili namna unavyowasiliana na wanafunzi wako. Jenga mazoea ya kusema maneno chanya yanayowajenga na kuwainua moyo. Usiwe mtu wa kuona mabaya na mapungufu yao pekee. Ona jema katika udhaifu wao na onesha kwamba bado una imani nao. Unapofanya hivyo bila kuchoka, utajijengea mazingira ya kuaminika.
Watambulishe kwa watu makini
Wakati mwingine wanafunzi wengi wakosa nidhamu kama namna ya kuonesha kuchanganyikiwa kwao. Hawajitambui na hawajui wafanye nini kwenye maisha. Mwanafunzi asiyejua ana malengo gani ya kimaisha na afanye nini kufikia kule anakotaka kwenda, inakuwa rahisi kwake kuiga watu wasio na mwelekeo.
Mwanafunzi wa namna hii, aliyechanganyikiwa asijue anasimamia kitu gani kwenye maisha, anaweza kujifunza tabia mbovu bila upinzani mkali. Hawa ndio wanaojihusisha na mapenzi wakiwa shuleni, wanavuta sigara na wakati mwingine kutumia madawa ya kulevya. Yote haya ni jitihada za kuziba ombwe la kutokujitambua.
Fanya jitihada za kuwakutanisha wanafunzi wako na watu maarufu wanaoweza kuwafundisha kitu fulani cha maana. Watu maarufu waliofanya vizuri kwenye maeneo mbalimbali wanaweza kuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko kwa wanafunzi. Zungumzia maisha ya wanasayansi maarufu, magwiji katika maeneo mbalimbali ambao kwa kusimulia habari zao, ari ya wanafunzi kuiga maisha yao inaweza kuongezeka.
Itaendelea…
Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815