32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

USHAWISHI WA MWALIMU UNAVYOWEZA KUJENGA NIDHAMU KWA WANAFUNZI

Na Christian Bwaya


SHULE zetu zinakabiliwa na changamoto kubwa ya nidhamu. Walimu wetu wanafundisha wanafunzi wanaojihusisha na vitendo vya uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, matumizi ya dawa za kulevya na hata uhusiano ya kimapenzi. Sambamba na utovu huo mkubwa wa maadili, wanafunzi wengi hawana usikivu si tu kwa walimu bali hata wazazi na watu wengine wanaowazidi umri.

Ni kawaida, kwa mfano mwanafunzi kubishana na mwalimu hadharani akipinga adhabu halali iliyotolewa kwa lengo la kumwadabisha. Mwanafunzi hufanya hivyo kwa lengo la kujipatia sifa kwa wanafunzi wenzake kwamba naye ana ubavu wa kubishana na mwalimu. Hali hii husababisha mchoko wa mawazo kwa walimu wetu na wakati mwingine huweza kuwachochea kuchukua hatua kali zinazoweza kusababisha madhara makubwa kwa wanafunzi.

Tumesikia matukio ya baadhi ya walimu kuwapa adhabu kali mno wanafunzi. Wapo walimu waliosababisha majeraha kwa wanafunzi na wakati mwingine hata kifo.  Katika mazingira kama haya, wakati wote, jamii imemnyooshea kidole mwalimu kwamba hana sifa za kuwa mwalimu.

Moja wapo ya sifa muhimu ya mwalimu ni uwezo wa kuchagua adhabu inayomfaa mwanafunzi aliyekosea. Natambua wapo walimu wasio na sifa. Lakini wakati huo huo naweza kuelewa kwa nini mwalimu anaweza kujikuta kwenye mazingira ambayo hana namna nyingine ya kufanya isipokuwa kuitikia ghadhabu yake na kutoa adhabu isiyolingana na kosa la mwanafunzi.

 

Nafasi ya ushawishi

Katika makala haya ninalo pendekezo moja kwa walimu linaloweza kusaidia kuepusha karaha ya kujikuta katika mazingira ya kutoa adhabu zinazoweza kuleta madhara kwa wanafunzi. Pendekezo lenyewe ni mwalimu kujenga ushawishi wake.

Ushawishi ni mamlaka aliyonayo mwalimu yanayompa uhalali na sauti ya kusema jambo na likasikika kwa wanafunzi. Mwalimu mwenye ushawishi hana sababu ya kutumia nguvu wala mabavu kuwafanya wanafunzi wamsikie. Ushawishi unampa sifa za kukubalika na kueleweka bila kulazimika kutisha, kupigana wala kutoa adhabu. Unapokuwa na ushawishi kama mwalimu, wanafunzi wanaweza kukusikiliza kirahisi sana hata kama hawawasikilizi walimu wengine. Nitajadili mbinu kadhaa zinazoweza kukusaidia mwalimu kuongeza ushawishi wako kwa wanafunzi wako.

 

Umahiri wa kazi

Wanafunzi wana tabia ya kumpenda mwalimu anayejua somo lake. Kama unataka kuwa na ushawishi kwa wanafunzi wako, hatua ya kwanza kabisa ni kufanya kazi yako kwa weledi. Fundisha kwa bidii. Jitume kufanya kazi. Wanafunzi wakijisikia kupata kile wanachostahili watakuheshimu.

Vipo visingizio vingi vinavyoweza kutumika kuhalalisha uvivu na ubabaishaji kwa baadhi ya walimu. Mazingira ya kazi, yanaweza kukukatisha tamaa na kudhoofisha ari yako ya kazi. Lakini fahamu kwamba wajibu wako kama mwalimu ni kufanya wajibu wako kama mlivyokubaliana na mwajiri wako. Umahiri na bidii kazini ni suala la maadili ya kazi na sio hiari.

Unapochagua kuwa mwalimu mvivu na mbabaishaji, elewa kwamba si tu unavunja maadili ya kazi yako kama mwalimu, lakini unajipoteza nguvu yako kama mwalimu. Wanafunzi hawatakuheshimu na utafanya kazi ya ziada kusikika kwa wanafunzi hali inayoweza kukulazimisha kutumia mabavu kila unapohitaji kuwaelekeza wanafunzi.

 

Heshima kwa wanafunzi

Walimu wengi wanawadharau wanafunzi. Dharau ni kumwonesha mwanafunzi kwamba hawezi, hana thamani na hastahili heshima kama binadamu timamu. Mwalimu mwenye dharau huwa na maneno ya kejeli, yasiyo na staha kwa wanafunzi. Pia dharau inaweza kumfanya apende kuwakosoa na kuwakatisha tamaa wanafunzi kuliko kuwajenga na kuwatia moyo.

Yapo mazingira yanayowafanya walimu wawadharau wanafunzi. Kwanza, uwezo mdogo wa wanafunzi darasani. Kama mwalimu, anatamani kuwa na wanafunzi wenye uwezo. Inapotokea wanafunzi hawaoneshi uwezo anaoutarajia, anakuwa mwepesi kuwaonesha dharau. Pili, ni tabia mbovu za wanafunzi.

Walimu wengi huwatendea vitendo visivyo na staha wanafunzi kama kisasi cha utovu wao wa nidhamu. Hili ni kosa kubwa la kifundi kama nitakavyoeleza hivi punde. Tatu, ni hulka binafsi ya mwalimu. Wapo walimu, kama watu wengine mtaani, wana tabia ya kuwadharau watu kwa sababu zisizoeleweka.

Hakuna binadamu anayesukumwa kumheshimu mtu asiyemheshimu. Tunapenda kuheshimiwa hata kama hatustahili heshima. Una wajibu wa kuwaheshimu wanafunzi kama kweli unahitaji wakuheshimu. Heshima ni pamoja na kuzungumza na mwanafunzi kwa lugha ya staha na kuwa tayari kuwasaidia kuwa watu bora zaidi bila kujali hali waliyonayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles