Arodia Peter, Dodoma
Usanifu wa Barabara ya mchepuo wa Mlima Nyoka ya mkoani Mbeya hadi Songwe, yenye urefu wa kilometa 48.9 inatarajia kukamilika Februari 2020.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda (Chadema), bungeni leo Ijumaa Mei 10, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe amesema upembuzi na usanifu wa kina wa barabara hiyo ulikamika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
“Hata hivyo, ilionekana ipo haja ya kufanya mapitio ya usanifu huo ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 Sh bilioni 2.6 kimetengwa kukamilisha usanifu huo,” amesema.
Kamwelwe amesema kazi hiyo ya upembuzi yakinifu wa kina wa barabara hiyo utakapokamilika na Serikali kupata fedha, ujenzi wa kiwango cha lami utaanza.