Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), kupitia serikali ya Marekani, limetangaza kuwekeza dola milioni 8.3 za Kimarekani kwa kampuni tisa za Tanzania ili kukuza biashara, kuboresha usalama wa chakula, na kuimarisha ushindani. Msaada huo pia utaiwezesha Tanzania kuongeza ushindani katika mauzo ya nje kupitia Mpango wa Ukuaji na Fursa Afrika (AGOA).
Mkurugenzi wa Mipango wa USAID/Tanzania, Craig Hart, aliyasema hayo leo, Agosti 20, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya maonyesho ya shughuli za biashara na uwekezaji ya USAID Afrika. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.
“Leo tunasherehekea ushirikiano wa USAID na kampuni tisa katika sekta muhimu zikiwemo asali, korosho, na nguo. Ushirikiano huu unatarajiwa kuzalisha ajira 2,000, kuongeza dola milioni 42.5 katika mauzo mapya nje ya nchi, na kukuza nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uchumi wa kanda,” alisema Hart.
Hart alizitaja kampuni tisa za ndani zitakazonufaika na ruzuku chini ya Mradi wa Biashara na Uwekezaji wa USAID Afrika. Kampuni hizo ni BioBuu, Biotan Limited, Central Park Bees, Minjingu Mines and Fertilizer Limited, Mount Meru Millers, Red Earth Limited, Sabayi Investments Limited, Tanzania Tooku Garments Co. Ltd, na Mtu wa Tatu (Love Honey).
“Tunafungua njia kwa Tanzania kuwa kikapu cha chakula kikanda, muuzaji wa nishati nje, na kitovu cha ubunifu unaoendeshwa na vijana. Kupitia AGOA, tunasaidia kampuni za Kitanzania kupata masoko Marekani,” alisema Hart.
AGOA ni sehemu muhimu ya sera ya kiuchumi ya Marekani na Afrika, inayozipa nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara fursa ya kuuza bila ushuru kwa soko la Marekani kwa zaidi ya bidhaa 1,800. Hart alieleza kuwa Tanzania imejipanga vyema kupanua uzalishaji wa asali, ambapo kwa sasa ni nchi ya pili kwa uzalishaji barani Afrika na muuzaji mkuu barani Ulaya. Aliongeza kuwa kampuni ya Man Limited (Upendo Honey), kwa kushirikiana na USAID, inalenga kuongeza mauzo ya asali nje ya nchi kwa asilimia 767.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Seleman Jafo, alisema kuwa Mradi wa Biashara na Uwekezaji wa USAID Afrika (ATI) umekuwa chachu katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watu wa Tanzania.
“Onyesho hili la shughuli za mradi wa ATI ni ushuhuda wa dhamira yetu ya pamoja kufungua fursa kubwa za uchumi wa Tanzania kupitia ongezeko la biashara na uwekezaji, kwa kuwawezesha wafanyabiashara na kukuza ubunifu katika sekta muhimu za uchumi wetu,” alisema Jafo.
Aidha, Jafo alibainisha kuwa Tanzania imeshuhudia ongezeko la mauzo ya nje ya baadhi ya bidhaa chini ya usaidizi wa mradi huo, uzalishaji wa ajira mpya, na uwezeshaji wa wajasiriamali ambao sasa wanachangia kuimarika kwa uchumi wa nchi.
“Tunapoangalia sekta zinazosaidiwa kupitia Mradi wa ATI, tuna matumaini makubwa kwamba mauzo yetu ya nje chini ya mpango wa AGOA yataongezeka sana wakati mipango yote itakapotekelezwa vyema,” aliongeza Jafo.
Pia, Jafo alisema kuna haja ya kuendelea kukuza na kuimarisha uwezo wa uzalishaji na usambazaji ili kukidhi mahitaji ya soko, na kupanua kapu la mauzo ya nje kwa kujumuisha bidhaa zilizoongezwa thamani na zenye viwango vya juu. Hata hivyo, alisisitiza kuwa, ingawa mafanikio yameshapatikana kupitia Mradi wa ATI, bado kuna kazi kubwa mbele ya kutumia kikamilifu fursa za biashara na uwekezaji.