23.6 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

USAID inavyosaidia kurejesha ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa ni eneo muhimu la kijiografia na kiikolojia nchini Tanzania. Eneo hili linaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere (Selous) na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, likiwa njia muhimu kwa ajili ya uhamaji wa wanyamapori kama vile tembo na wanyama wengine wengi.

Hata hivyo, ushoroba huu ulikumbwa na changamoto mbalimbali zilizosababisha uharibifu wake. Hapa ndipo mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umekuwa na mchango mkubwa katika kuurejesha ushoroba huu na kuhakikisha unalindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Sehemu ya pito la wanyama ambalo hutumia kuvuka linaunganisha ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa.

Katika kuliangalia hilo, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), ambacho kinatekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), kiliratibu timu ya waandishi wa habari kwenda wilayani Kilombero mkoani Morogoro kuangalia juhudi za kuurejesha ushoroba huo. Ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa ni kati ya shoroba 20 ambazo Serikali imepanga kuzihifadhi, mbali na zile 61 zilizotambuliwa.

Mei 14, mwaka huu, akizungumza katika mdahalo kuhusu mkakati wa serikali wa kuhifadhi shoroba, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Fortunata Msofe, alisema kati ya shoroba 61 zilizotambuliwa, serikali imelenga kuhifadhi shoroba 20, ambapo kati ya hizo, mbili ziko katika hatua ya mwisho.

“Katika shoroba 20 za kipaumbele, hadi sasa shoroba mbili za Nyerere-Selous-Udzungwa na ile ya Kwakuchinja inayounganisha mbuga ya Tarangire na Lake Manyara ziko katika hatua ya mwisho. Hii ni kutokana na juhudi kubwa ambazo zimefanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau kama USAID kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili,” alisema Dk. Fortunata.

Changamoto zinazoukabili ushoroba huo zimepunguza ufanisi wake katika kuhifadhi wanyamapori. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na ukataji miti kiholela kwa ajili ya kuni na kilimo, uwindaji haramu, na uharibifu wa vyanzo vya maji. Shughuli hizi za kibinadamu zimeathiri sana uwezo wa ushoroba huu katika kusaidia uhamaji wa wanyamapori na kuhifadhi bayoanuai.

Akizungumzia hali hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho, anaeleza kuwa: “Uharibifu wa ushoroba ni tishio kubwa kwa wanyamapori na mazingira. Tunahitaji juhudi za pamoja kurejesha na kulinda eneo hili muhimu ili kuhakikisha uendelevu wake.”

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Akizungumzia ushiriki wa USAID kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili unaolenga kuboresha ulinzi wa ushoroba kwa kushirikiana na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii za wenyeji, Theodora anakiri kuwa kumekuwa na mchango mkubwa katika kuurejesha ushoroba huo.

“Kazi kubwa imefanyika katika kuimarisha ulinzi wa mipaka, kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi, na kuboresha mbinu za kilimo ili kupunguza utegemezi wa watu kwenye misitu. USAID imetoa msaada mkubwa katika juhudi za kuhifadhi ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa. Kupitia msaada huu, tumeweza kuimarisha ulinzi na kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu. Ndiyo maana utaona kwamba sasa kuna uzio ambao unasaidia kulinda wanyama wasiweze kuleta madhara. Hivyo, mchango wa USAID Tuhifadhi Maliasili kupitia miradi ya kulinda ushoroba umeonyesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuhifadhi urithi wa asili,” anasema Mhifadhi Theodora.

Moja ya mikakati muhimu ya uhifadhi endelevu katika Hifadhi ya Udzungwa ni kushirikisha jamii za wenyeji katika mipango ya uhifadhi na ulinzi wa shoroba. Jamii zinazozunguka hifadhi hii zinategemea sana rasilimali za misitu kwa maisha yao ya kila siku. Hivyo, ni muhimu kuzijumuisha katika juhudi za uhifadhi ili kuhakikisha mipango ya uhifadhi inafanikiwa.

Mhifadhi Theodora anasema kupitia miradi ya pamoja ya USAID na wadau wengine, jamii zimewezeshwa katika mbinu mbadala za kujipatia kipato kama vile ufugaji nyuki, kilimo cha kisasa, na utalii wa kiutamaduni.

“Tumeweza pia kushirikiana na wenzetu wa Reforest Africa ambao ni taasisi inayojishughulisha na uoteshaji miti. Hili wamelifanya hata katika maeneo ya ushoroba huu ambapo wamepanda miti ya asili zaidi ya 15,000 kwenye eneo la shoroba lililotumiwa awali na wananchi kama mashamba ya kilimo cha miwa. Mkakati ulipo ni kuhakikisha kwamba wanaotesha miti 100,000. Kifupi naweza kusema kwamba hatua za uokoaji wa ushoroba huu zinaridhisha,” anasema Mhifadhi huyo.

Reforest Africa na Urejeshaji wa Shoroba

Reforest Africa ni Shirika linalojishughulisha na urejeshaji wa misitu, kugundua mbinu mpya za kuokoa na kukuza misitu kwa wakati mmoja na kuzitumia kwa mandhari ya misitu inayohitaji usaidizi. Lasima Nzao ni Meneja Programu wa Reforest Africa ambapo anasema kuwa wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa unarejea katika hali yake.

“Shughuli kubwa tunayofanya ni urejeshwaji wa misitu kwenye maeneo ya ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa ambayo awali wananchi waliyatumia kama mashamba ya miwa. Kwa kupanda miti ya asili na kurejesha maeneo ya misitu, mradi huu unalenga kuhifadhi na kuongeza makazi ya viumbe hai mbalimbali, ikiwemo wanyama, ndege, na mimea adimu. Pia, Reforest Africa inashirikiana na jamii katika kuanzisha miradi ya kiuchumi inayotegemea misitu kama ufugaji nyuki na utalii wa kiikolojia,” anasema Nzao.

Meneja Programu wa Shirika la Reforest Africa, Lasima Nzao(wapili kutoka kulia) akiwaelezea waandishi wa habari kuhusu mradi wa uoteshaji miti.

Akizungumzia mchango wa USAID, Nzao anasema kuwa wanawasaidia katika nyanja mbalimbali ikiwamo usalama wa msitu wa Magombela na urejeshaji wa misitu.

“Mfano, kwenye mradi huu wa USAID Tuhifadhi Maliasili wenyewe unalenga kuokoa shoroba ambapo katika eneo la Msitu wa Hifadhi Asili wa Magombela, ambao ndiko ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa unaingilia, USAID kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wanatusaidia kuhakikisha kuwa msitu unakuwa salama. Hivyo, USAID wanatusaidia katika mradi wa kuotesha miti kuanzia hatua ya kukusanya mbegu, uandaaji wa vitalu, miti na hatua ya kwenda kuotesha miti katika shoroba ikiwamo uangalizi na udhibiti wa moto,” anasema Nzao.

Sehemu ya miti iliyopandwa na Reforest Africa katika eneo la ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa.

Nzao anasema hadi kukamilika kwa mradi huo wamelenga kupanda miti ya asili 100,000 kutoka katika aina 27 tofauti na angalau asilimia 70 mpaka 100 iweze kukua.

“Tunatamani kuona kwamba hata baada ya mradi kufikia ukomo, asilimia kubwa ya miti iwe hai. Ndiyo maana hata kwenye eneo la ushoroba ambako miti imepandwa, kuna watu wanaifanyia usafi. Lengo letu ni kupanda miti 50,000 kufikia Juni mwaka huu na hadi sasa tuna miti 37,000 kutokana na changamoto ya mvua,” anasema Nzao.

Meneja Uhusiano na Jamii-Reforest Africa, Peter Nnyiti, akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani).

Meneja Uhusiano na Jamii kutoka Reforest Africa, Peter Nnyiti, anasema mbali na upandaji wa miti hiyo katika maeneo yanayohusishwa na ushoroba huo, pia wanajikita kutoa elimu kwa jamii hususan wanafunzi ili waweze kutambua umuhimu wa kutunza na kulinda misitu.

“Wakati mradi huu unaanza, kwanza USAID Tuhifadhi Maliasili walitujengea uwezo kuhusu namna gani miti inaandaliwa sambamba na mbinu za kuishirikisha jamii katika kuisimamia na kuhakikisha inakua. Jambo ambalo limeweza kuwa na manufaa makubwa,” anasema Nnyiti na kusisitiza kuwa kila siku kuna mabadiliko ya ushiriki ya urejeshaji kutoka kwa wanajamii.

Sehemu ya mbegu za miti inayopandwa na Shirika hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles