24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

USAFIRI WA MWENDOKASI KUSUKWA UPYA (5)

  • Jinsi mabasi yanavyoondolewa kwenye ruti kijanja

Na BAKARI KIMWANGA – DAR ES SALAAM


USAFIRI wa mabasi ya mwendokasi, umekuwa ukibeba abiria wengi katika jijini la Dar es Salaam huku changamoto ya uchache na ubovu wa baadhi ya magari ukiwa bado ni kilio kikubwa.

Kutokana na hali hiyo, kila mara mamlaka za Serikali zimekuwa zikiangazia usafiri huo ikiwa ni pamoja na kutoa maagizo kwa mbia aliyepewa kazi ya kuendesha mradi huo kwa kipindi cha mpito.

Jana ripoti hii maalumu iliangazia kilio cha wamiliki wa daladala pamoja na hatua zinazochukuliwa na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani kuhusu ukaguzi wa magari hayo ambayo mengi yamekuwa yakielezwa ni mabavu.

Leo ripoti hii maalumu inamulika ‘ujanja’ unaofanywa na mwendeshaji, Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDA-RT), kuhusu ubora wa magari hayo ambapo kila mara yanapokuwa na hitilafu, sababu anayoitoa ni mvua ndizo zinazosababisha uharibifu huo.

KILICHOJIFICHA NYUMA

Oktoba 26, mwaka jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo aliagiza uongozi wa UDA-RT, kuhakikisha wanayaondoa magari yaliyopo Jangwani pindi wanapoona dalili za mvua.

Katika uchunguzi wake, MTANZANIA limebainika kuwa baadhi ya magari hayo hayana uwezo wa kutembea kutokana na ubovu.

Mabasi zaidi ya 130 yaliletwa nchini mwaka 2016 ambapo hadi sasa yana miaka mitatu, lakini bado kuna utata kuhusu ubora wake huku sababu kubwa ikibaki kuwa mvua kubwa inaponyesha huduma za mabasi hayo husitishwa.

Kwamba kufurika kwa maji katika njia za mabasi hayo na kwenye kituo kikuu ambako mara ya mwisho mabasi kadhaa yaliharibika sababu ya kujaa maji.

Waziri Jafo alitoa agizo la mabasi hayo kuondolewa baada ya kutembelea eneo la Jangwani, Jijini Dar es Salaam yalipo maegesho ya mabasi hayo.

Baada ya ziara yake hiyo, alisema tayari maegesho mengine yameshapatikana hivyo aliwataka UDART kufanya hima kwa ajili ya usalama wa mabasi hayo ambayo ni msaada mkubwa kwa usafiri wa wakazi wa Dar es Salaam kuyahamishia eneo ambalo ni salama.

Aidha, Waziri Jafo aliwataka UDART, DART na DAWASA wasafishe Mto Msimbazi ili kuruhusu maji ya mvua kupita kirahisi ili kuweza kufanyika kwa marekebisho ndani ya maegesho ya Jangwani.

Ajabu ni kwamba pamoja na agizo hilo, yapo mabasi ambayo hawezi kutembea kutokana na ubovu jambo ambalo linazua maswali zaidi.

Mwaka jana, Meneja Uhusiano wa UDA-RT, Deus Bugaywa alieleza kuathirika kwa mabasi 29 kati ya 134 baada ya maji kuingia katika sehemu tofauti za magari hayo zikiwemo injini.

MTANZANIA lilipohitaji ufafanuzi wa kina kuhusu ubovu wa magari hayo huku mengine yakishindwa kutembea kabisa, Bugaywa alimtaka mwandishi atume maswali lakini hata alipotumiwa alishindwa kuyajibu.

MTANZANIA lilimtafuta Bugaywa kwa simu na alipoipokea alisema hawezi kuzungumza kwa sababu yupo hospitali. Alisisitiza kuwa hawezi kujibu chochote kama kuna maswali yametumwa, aliyepo ofisi anaweza kuyajibu, hata hivyo hilo halijafanyika hadi leo.

DART  YANENA

Akizungumza hali hiyo, Meneja Uhusiano wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo haraka Dar es Salaam (DART), William Gatambi, alisema mabasi hayo kwa sasa yamepungua kutoka 140 hadi kufikia 96 au 106.

Alisema mabasi yaliyokuwa yamehamishwa Jangwani, hivi sasa yamerudishwa kwa sababu licha ya tishio la mafuriko yapo mengine ni mabovu kabisa na hayana uwezo wa kutembea lakini hilo mwendeshaji amekuwa halisemi.

“Kwa mfano changamoto ile ya Jangwani kwenye karakana, kabla ya kujengwa ilitolewa ripoti kwa sababu unapotaka kujenga sehemu kama hizo huwa inatakiwa ripoti ya taasisi inayotathimini athari za mazingira (NEMC) ambayo ilitoa ruhusa ya kujenga pale, kwa hiyo mwanzoni hawakuligundua hilo.

“Kama unakumbuka zamani watu walikuwa wanacheza mpira pale lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu ambazo zimekuwa zikifanyika kandokando ya Bonde ya Mto Msimbazi, ndivyo vilivyosababisha mabadiliko ya namna hiyo.

“Kwa mfano, kuanzia Oktoba 26, mwaka jana yalitokea mafuriko yaliyoharibu karibu mabasi 40, lakini Waziri wa TAMISEMI alikuja akawaagiza watoa huduma (UDA-RT) kwamba wanapoona dalili za mvua wayahamishe hayo mabasi kutoka pale karakana yakayaegeshe Gerezani Kariakoo,” alisema.

HITILAFU YA MABASI

Gatambi, alisema kuwa kabla ya mafuriko kulikuwa na mabasi ambayo yalikuwa na hitilafu.

“Lakini kwa kuwa ni mfanyabiashara anakuwa anasingizia kila kitu ni mafuriko kumbe kuna vitu vingine ni matatizo yake mwenyewe… sasa kinachoonekana na macho ya watu ni kwamba mafuriko yalikuta mabasi yakaharibika lakini kumbe alishindwa kuyahamisha kwa sababu yalikuwa na hitilafu yakashindwa kuendeshwa,” alisema Gatambi.

MTOA HUDUMA MWINGINE

Alisema pamoja na hali hiyo, bado kuna changamoto ya upungufu wa mabasi hayo.

Ndiyo maana tulikuwa tunasema wanasubiri kwa sababu ya upungufu wa mabasi si kwa makusudi, lakini suluhu ya aina hiyo Serikali inaleta mtoa huduma wa pili hivi karibuni ambaye ataleta mabasi pamoja na yaliyopo yatakuwa mabasi 305 na haya mabasi yataanza kutoa huduma kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Watu tunaona yanakaiwa, hata mimi ningependa hata leo yaje lakini kutokana na hatua za manunuzi ambazo zinatakiwa zifuatwe kwani ukikiuka baadaye unaweza kushtakiwa,” alisema.

Alisema yatakapokuja mabasi hayo mradi huo utakuwa na mabasi mengi ambapo mengine yatatoa huduma kwenye njia ‘mrishi’ zilizo nje ya barabara za mradi huo.

“Kwa kuwa mtoa huduma wa pili atakuwa ni mwingine kutakuwa na ushindani, siyo mtoa huduma mmoja anayeweza kuwadanganya hivi. Kwa hiyo changamoto kubwa ni hizo hasa ya uhaba wa mabasi ikiisha huduma zitakuwa nzuri,” alisema Gatambi

Alisema wakati mradi huo ulipoanza ulikuwa ukihudumia watu 75,000 na kwa sasa unakadiriwa kuhudumia watu karibu 200,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles