29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

URUSI YAIONYA UINGEREZA KUTOLITISHA TAIFA LENYE NYUKLIA

MOSCOW, URUSI


SERIKALI ya Urusi imeionya Uingereza kuacha kulitisha taifa lenye nguvu ya nyuklia.

Badala yake imemtaka Waziri Mkuu wa Uingereza, awasilishe sampuli ya sumu ya Novichok iliyotumika kumshambulia jasusi wa zamani wa Urusi.

Kwa mujibu wa Ubalozi wa Urusi mjini London, ni kupitia sampuli hiyo ndiyo itaweza kuifanya Urusi ifikirie kutoa maelezo inayotaka Uingereza kuhusu sumu hiyo.

Kutokana na msimamo huo wa Serikali ya Rais Vladimir Putin, saa 24 zilizotolewa na Uingereza kuitaka Urusi kutoa maelezo kuhusu kuhusishwa kwake na shambulizi la sumu dhidi ya Sergei Skripal na binti yake Yulia zimemalizika pasipo kueleza chochote.

Uhusiano kati ya Uingereza na Urusi umezorota kwa haraka katika kipindi cha siku 10 tangu jasusi huyo na binti yake kushambuliwa kwa sumu mjini Salisbury, kusini magharibi mwa Uingereza.

Juzi Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, alisema kuna uwezekano mkubwa Urusi inahusika kwa njia moja au nyingine kwa sababu imeshindwa kudhibiti sumu hiyo.

Lakini Urusi kupitia ubalozi wake mjini London, ilisisitiza haitatekeleza wito huo hadi pale itakapopokea sampuli ya kemikali hiyo, huku pia ikitoa mwito kufanyika uchunguzi wa pamoja kuhusu hilo.

Ubalozi huo umeongeza Urusi haihusiki na shambulizi hilo kwa namna yoyote na kuonya Uingereza inapaswa kutambua watajibu vikali adhabu yoyote itakayotolewa.

Umesema hizo ni njama za kuivuruga Urusi inayoandaa michuano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia.

May alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Urusi iwapo itashindwa kutoa maelezo ya kina kuhusu tuhuma hizo kufikia usiku wa kuamkia jana.

Hatua zinazofikiriwa ni pamoja na kuzuia mali za viongozi wa Urusi na maofisa wengine wa nchi hiyo.

Pia kuzuia Urusi kuwekeza katika masoko ya kifedha ya Uingereza na kuwafukuza wanadiplomasia wa nchi hiyo.

May alitarajia kuainisha hatua hizo mbele ya Bunge jana baada ya mkutano wa Baraza la Usalama la Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles