24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

URAIS NA MATESO YA IKULU

MOJA ya mambo ninayoyafurahia sana ni kufuatilia tamthilia za nje, hasa zile zinazohusiana na masuala ya ujasusi pamoja na masuala ya uongozi wa nchi.  Yapo mengi ya kujifunza na yapo mengine ya kuiga.  Lakini kati ya yote, swali kuu ambalo najiuliza kila nikitazama tamthilia hizo, ni: kwanini watu wanautaka Urais?

Rais John Pombe Magufuli wiki iliyopita amelalamikia kazi ngumu aliyonayo na kueleza kwamba Ikulu ni mateso na kazi ya Urais ni ngumu, ni msalaba na inahitaji kumtanguliza Mungu.

Naomba nimuongezee lingine: kazi ya Urais ni jalala

Tuchukue jalala la kawaida la nyumbani.  Licha ya uwepo wa ndoo za takataka kwa ajili ya kuhifadhi taka ndani ya nyumba, yapo pia mashimo ya taka ambayo mara nyingi husubiri ndoo hizo zijae ili yapokee taka zake.  Taka zile zinakuwa hazihitajiki, ila tu zimeachwa ziozee kwenye mashimo zilimotupiwa.  Mashimo hayo ni majalala.

Urais ni jalala.  Urais kwa hapa Tanzania ni cheo cha juu kiliko vyote, kikiwa na maana ya mkuu wa nchi.  Ukuu wa nchi maana yake ni kwamba hatatukuzwa, pengine hata kwa yale mazuri aliyoyatenda, bali atatupiwa taka za aina zote.  Taka zingine kati ya hizo atakuwa anazistahili na zingine hatozistahili.  Lakini kwakuwa ni Rais, kwakuwa ni jalala, ndiyo kazi aliyoiomba.

 

Tunaufahamu sana ugumu wa kazi ya Ikulu, hasa kwa mtu mwenye nia njema ya kuongoza.  Si kazi rahisi hata kidogo na ndio maana walipojitokeza wanaCCM zaidi ya 40 kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuwa wagombea wa kiti hicho, wengi wetu tulibaki tukiishangaa idadi hiyo ilivyokuwa kubwa, ilhali kazi inayoombwa ilikuwa ngumu kuliko zote.

Ni kutokana na ujalala huo wa kazi ya Urais, ndio maana ili kufanikiwa, Rais hawezi kuifanya kazi hiyo peke yake.  Anahitaji timu, anahitaji washauri atakaowasikiliza, lakini zaidi ya yote, anahitaji wananchi anaowaongoza wamwamini na pia awe anawasikiliza, hata kama ni wapinzani wake.

Ili kazi ya Urais iwe na nafuu kidogo, Rais yeyote yule anatakiwa kujua kwamba kutokana na kazi yake kuwa kama jalala, anatakiwa apokee kila kitu, hata zikiwa ni takataka zilizokwisha kuoza.  Lakini zaidi ya yote, hatakiwi kutumia muda mwingi kujaribu kumthibitishia kila mtu kwamba yeye ndiye Rais wa nchi, kwani hicho ni kitu kinachojulikama na hakihitaji ‘approval’ yoyote.

Inapotokea kwamba Rais yeyote anasumbuliwa na maneno ya kawaida sana ya wale wanaompinga na anatumia muda mwingi kulalamika na kujieleza, basi kazi yake ya uongozi wa nchi itakuwa ni ngumu kuliko ambavyo tayari ipo.  Akiruhusu kunyong’onyeka kwa kila kitu kinachosemwa juu yake na kutaka kuadhibu kila mtu anayepingana na maono yake, basi Ikulu kwake haitakalika kabisa.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutamka kwamba Ikulu ni pagumu, ni mzigo na si sehemu ya mchezo mchezo.  Wapo waliomuelewa na wapo ambao walidhihaki na kuona kwamba vyovyote iwavyo, lazima waje kugombea Urais ili waiongoze Tanzania.  Hawakuelewa kwamba uongozi wa kweli ni mzigo na ni jalala.

Si jambo la kushangaza kwa Rais Magufuli kuona mateso ya Ikulu.  Ndani ya miezi 22 ya uongozi wake tayari mambo mengi makubwa yamefanyika, mambo yanayofanya wengine tujiulize endapo wale wagombea wengine 40 ndani ya CCM wangekuwa katika kasi hii hii.  Wangeifurahia Ikulu, au wangelalama kutokana na uongozi kuwa mgumu?

Ushauri wangu kwa Rais Magufuli ni mmoja tu:  Urais ni jalala ambalo kila kitu hutupiwa humo ili kioze.  Ni kazi aliyoiomba mwenyewe na akapewa.  Aache kuhangaika na vitu vidogo ambavyo hutupwa kwenye jalala.  Wakati mwingine hivyo vitu vinatakiwa kutazamwa tu na kuviacha vioze na si kuvigeuza geuza ili vitoe harufu vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles