26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Urafiki wa kupeana wake washamiri barani Afrika

Mwanamke wa kiafrika akimnyonyesha mtoto wake.
Mwanamke wa kiafrika akimnyonyesha mtoto wake.

UKISTAAJABU ya Musa, utaona ya Firauni. Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea mila na desturi zilizopitiwa na wakati ambazo bado zingalipo barani  Afrika, hasa maeneo ambayo jamii ndogo ndogo zinaishi kwa kujitenga na nyinginezo.

Miongoni mwa mila hizo ni zile za kubadilishana wake, vitendo ambavyo ni maarufu miongoni mwa makabila ya Namibia.

Hata hivyo, haviko Namibia pekee bali kwa namna nyingine viko katika baadhi ya jamii kama za Nigeria na vimeshamiri kwa namna tofauti Ulaya hadi kuambukiza mataifa mengine ya Asia kama vile India.

Namibia iliteka vichwa vya habari wakati mbunge mmoja alipotaka mila hiyo iwe sehemu ya sheria za nchi.

Hilo lilizua mjadala kuhusu haki za wanawake na uhalali wa kuiendeleza katika jamii ya kisasa.

Ikijulikana kama lugha ya kwao “okujepisa omukazendu,” yaani ‘kumtoa ofa mke kwa mgeni’ haikuwa ikifahamika nje ya jamii hizo, ambazo idadi yao haifiki  watu 100,000.

Ni aina ya makubaliano ya kiungwana ambayo marafiki wanabadilishana wake zao bila kikwazo chochote.

Katika hili, ni wazi wake hawana usemi kupinga suala hilo. Badala yake hubadilishwa, na kuzunguka baina ya wanaume tofauti tofauti katika nchi, ambayo kuna moja ya viwango vya juu kabisa vya maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Lakini makabila ya Ovahimba na Ovazimba yanayoishi kwa kuhama hama hutetea mila yao hiyo yakisema inaimarisha urafiki na kuzuia uzinzi.

“Ni utamaduni ambao unatengeneza umoja na urafiki,” alisema Kazeongere Tjeundo, Mbunge na Makamu wa Rais wa chama cha upinzani cha Democratic Turnhalle Alliance of Namibia (DTA ).

“Ni juu yako kuchagua miongoni mwa wenzako nani unamruhusu alale na mkeo,” anasema Tjeundo, ambaye anatokana na kabila la Ovahimba.

Tjeundo amekuwa mstari wa mbele kushinikiza sheria ya kubadilishana wake tangu alipotangaza kutetea kiti chake cha ubunge kuelekea uchaguzi wa Novemba 2014.

Ikiwa inatumika zaidi katika eneo la Kunene la Kaskazini Magharibi karibu na mpaka wa Angola, makabila hayo kwa kiasi kikubwa yamejitenga na sehemu kubwa iliyobakia ya nchi.

Makabila hayo yamekuwa yakipuuza kuingia katika maisha ya kisasa, wakifuga mifugo na kuabudu mizimu.

Kutokana na wasiwasi kuwa VVU inaweza kutumika katika kile alichokiita kuwa kisingizio cha kusitisha mila yao hiyo ya kale, mbunge huyo wa Jimbo la Opuwo Vijijini na wenzake wanatafuta namna ya kuifanya kuwa salama zaidi.

Wengi katika makabila hayo bado wanaishi katika vibanda vya matope na miti na wanaume kwa wake hutembea wakiwa vifua wazi.

Wanawake huvaa sketi fupi za ngozi ya mbuzi na vikorokoro vingine vingi kiunoni, shingoni, miguuni na mikononi huku wakipaka ngozi zao tope la kujikinga na jua.

Tofauti na mataifa au sehemu nyingine ikiwamo Ulaya, ambako kitendo hicho hufanyika kwa ajili ya starehe, wahusika hukutana vibandani mwao, ambapo mume au mke wa kundi lingine hutokomea katika vibanda tofauti wakati wa kubadilishana.

Wanawake hawawezi kupinga kulala na mwanamume aliyechaguliwa na waume zao, kitu kinachowakasirisha wanaharakati kama Rosa Namises ambaye anasema kitendo hicho ni ubakaji wa hali ya juu.

“Kitendo hicho hakinufaishi wanawake bali wanaume ambao wanataka kudhibiti wenzi wao pamoja na kuridhisha tamaa za miili yao,” alisema Namises, mbunge wa zamani ambaye anaongoza taasisi isiyo ya kiserikali ya utetezi wanawake iitwayo Woman Solidarity Namibia.

Makundi mengine kama vile Namibia’s Legal Assistance Centre (LAC), kituo cha sheria kilichoapa kulinda haki za Wanamibia wote, kimepinga uwepo wa mila hiyo katika nchi ambayo asilimia 18.2 ya wakazi wake milioni 2.1 wanaishi na VVU, kwa mujibu wa takwimu za taifa hilo.

“Ni kitendo kinachowaweka wanawake katika hatari ya kiafya,” alisema Amon Ngavetene, ambaye anasimamia miradi ya Ukimwi ya LAC. Alisema kwamba kiuhalisia wanawake wengi wanapinga kitendo hicho na wangependa kiharamishwe.

Lakini Kambapira Mutumbo (40), anasema anajisikia vizuri na mila hiyo na kwambe amekuwa akilala na marafiki za mumewe bila matatizo.

“Nimefanya mara nyingi na sina tatizo na mila hii. Ni nzuri kwa sababu ni sehemu ya utamaduni wetu. Kuna haja gani sasa ya kuibadili?” alihoji.

Cloudina Venaani,  mchambuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo (UNDP) nchini Namibia, anaamini wanawake hawaipendi mila hiyo ila wanavumilia tu kwa sababu wanahofia kuwakosea waume zao.

Wenyeji hata hivyo wanasisitiza kuwa mila hiyo haikiuki haki za wanawake, wakidai wanawake pia wako huru kuchagua wanawake wa kulala na waume zao – hata kama inatokea kwa nadra.

Wanasema waume kwa wake wengi wa Namibia na duniani kwa ujumla wanatoka nje ya ndoa kwa siri, wakati wao hufanya kwa uwazi na kuondoa hofu na wasiwasi wa kukamatwa.

Na mbunge wa Tjeundohe, Uziruapi Tjavara, ambaye ni chifu wa Mamlaka ya Jamii ya Otjikaoko katika Mkoa wa Kunene, anataka mila iendelee lakini ikiendana na elimu ya Ukimwi.

Nchini Nigeria pia kunaaminika wanawake wa Benue hupewa wageni wa kulala nao kama sehemu ya starehe. Ijapokuwa watu wengi kutoka jimbo la Benue wamekuwa wakikana madai hayo, lakini wachache wako wazi kukiri hilo.

“Shangazi yangu ana rafiki hapa Lagos, ambaye anatokea katika Jimbo la Benue. Siku moja, shangazi yangu alimfuma akifanya mapenzi na mwanaume mwingine wa Benue na alikasirika sana, “ anasimulia shuhuda mmoja na kuendelea;

“Mwanamke huyo alimueleza shangazi kuwa mbona hilo ni suala dogo kama ilivyo kwa utamaduni wao na kuwa hata mumewe anatoka na mke wa mwanaume huyo.”

Lakini pia kama utadhani vitendo hivyo viko Afrika tu utakuwa umekosea kwani vimeota mizizi katika mataifa ya magharibi ambako kunaongoza duniani kwa kila aina ya anasa.

Baba lao inasemekana ni Italia, ambako inakadiriwa wenzi 500,000 na hata zaidi ya milioni mbili mara kwa mara hushiriki vitendo vya kubadilishana wake zao.

Hubadilishana rasmi katika vilabu binafsi vya ngono, huku maelfu zaidi wakifanya vitendo hivyo katika maeneo ya maegesho ya magari, ufukweni na hata makaburini.

Pia iliripotiwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia,  Silvio Berlusconi aliwahi kutania kuwa alijaribu kumkuwadia mkewe Veronica kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Denmark Anders Fogh Rasmussen.

“Rasmussen ni waziri mkuu mzuri zaidi Ulaya. Nadhani nitamtambulisha kwa mke wangu kwa sababu yeye yu mzuri zaidi kuliko Cacciari,” Berlusconi alisema akirejea tuhuma ambazo mkewe alizikana kuwa alivutiwa na meya wa zamani wa Venice, Massimo Cacciari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles