23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Upungufu wa kisheria wampa ushindi Lipumba

KULWA MZEE-DAR EA SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya bodi ya wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), iliyokuwa ikihoji uhalali wa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba kwa sababu yana upungufu wa kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Benhajj Masoud aliyekuwa akisikiliza maombi hayo namba 23 ya mwaka 2016.

Katika uamuzi wake wa kuyatupa maombi hayo, alisema kiapo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, hakioneshi kama alipewa idhini na bodi hiyo kufungua shauri hilo na kusaini hati ya kiapo.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Masoud alisema mahakama inazingatia hoja kuwa, kama kulikuwa na idhini ya bodi ya wadhamini ya CUF ya kumruhusu Sharifu Hamad kufungua shauri hilo na kusaini hati ya kiapo kinachosapoti maombi yao kama sheri ya mapitio inavyoelekeza.

Alisema katika hoja hiyo, kiapo cha waleta maombi  kilichowasilishwa mahakamani, hakikuwa na kielelezo cha kuthibitisha kama bodi hiyo ya wadhamini ilimpa mamlaka Maalim Seif ya kufungua shauri hilo na badala yake kulikuwa na  saini yake katika kiapo hicho.

“Suala hilo linahitaji nyaraka za ushahidi kuonesha maamuzi yaliyopitiwa na bodi ya wadhamini ikiwa ni pamoja na majina ya wajumbe na siku waliyokaa na kumteua Maalim Seif kufungua shauri hilo,”alisema.

Alisema  katika kiapo cha msingi, waleta maombi walidai Lipumba aliitisha kikao isivyo halali na kutaja majina ya watu watano kama wajumbe wa bodi, majina hayo pia yapo katika nyaraka za Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama wajumbe wa bodi ya wadhamini.

Alisema katika majibu ya hoja za Sharifu Hamad, alitarajia angeweza kubainisha majina hayo kuwa nani ni nani lakini haikufanya hivyo.

Kuhusu hoja kama mleta maombi amejenga kesi yake alisema, Mamlaka ya Msajili wa Vyama Vya Siasa hayaishii kwenye kusajili na kubadilisha majina ya vingozi wa chama husika, ndiyo maana ana uwezo wa kufuta chama cha siasa kinapokiuka sheria.

“Kutokana na hali hiyo, mahakama imeridhika na kilichofanywa na msajili kwamba kipo ndani ya mamlaka yake na kwamba anaona tafsiri ya sheria juu ya Msajili wa vyama vya siasa inapaswa kupewa tafsiri ndogo  badala ya kusema msajili tu,”alisema.

Alisema kutokana na mazingira hayo, anatupilia mbali maombi  ya wajumbe wa Bodi ya wadhamini ya CUF bila kutoa amri nyingine yoyote.

Shauri hilo lilifunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho wanaomuunga mkono Maalim Seif, dhidi ya Prof. Lipumba, M wanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Msajili wa Vyama vya Siasa, wakipinga uamuzi  wa Msajili kumtambua Profesa Lipumba kuwa bado ni mwenyekiti halali wa CUF.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016 ni  viongozi 10 wanaomwunga mkono Profesa Lipumba, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), ambaye pia ni mbunge wa Kaliua mkoani Tabora, Magdalena Sakaya.

Akizungumza nje ya mahakama, Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Thomas Malima, aliwakaribisha wanachama waliojitenga kutokana na mgogoro huo kurejea na endapo wataleta mgogoro watashughulikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles