30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

UPINZANI WATAKA JWTZ IDHIBITI UHALIFU RUFIJI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imependekeza Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) litumike kukabiliana na uhalifu katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Pendekezo hilo lilitolewa bungeni jana na Naibu Msemaji wa Kambi hiyo katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga  Taifa, Mwita Waitara.

Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga (Chadema), aliwasilisha maoni hayo baada ya Waziri   Dk. Hussein Mwinyi, kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya   wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Siku za hivi karibuni  kumekuwa na matukio ya ugaidi ya kuvamiwa kwa vituo vya polisi na watu wasiojulikana na kupora silaha, kuwaua   polisi na kuwapora silaha na kuuawa kwa wananchi hasa   viongozi wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.

“Matukio hayo yanaonyesha  watu wanaofanya uhalifu wana mafunzo ya  jeshi na mbinu za vita ndiyo maana wameweza kutekeleza uhalifu huo bila kukamatwa na bila kujulikana kwa majina yao na hata wanakoelekea baada ya kufanya uhalifu.

“Katika hili kuna kila dalili kwamba polisi wamezidiwa mbinu na nguvu za kukabiliana na wahalifu hao. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri na kupendekeza kwamba  Jeshi la Ulinzi liingilie kati kwa kutoa wapelelezi wa  jeshi  wakatoe msaada wa upelelezi na hatimaye kuwabaini na kuwashughulikia wahalifu hao,” alisema Waitara.

Wakati kambi hiyo ikisema hayo, awali, Dk. Mwinyi alipowasilisha bajeti ya wizara yake, aliliambia Bunge kwamba  wizara   kupitia JWTZ  ilishiriki katika operesheni mbili zilizofanyika   katika mapango ya Amboni, Mkoa wa Tanga ambako kulikuwa na wahalifu wengi.

“Katika kukabiliana na uhalifu wizara kupitia JWTZ, imeendelea kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na mataifa mengine katika kupambana na tishio la usalama ukiwamo ugaidi, uharamia na biashara ya dawa za kulevya.

“JWTZ limeshiriki katika operesheni mbili zilizofanyika Amboni,  Mkoa wa Tanga zilizoanza Mei 2016 na kufungwa Desemba 2016 ambako wahalifu hao walidhibitiwa,”alisema Dk. Mwinyi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu, alisema wizara imeshindwa kulipa fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao.

Rajabu ambaye pia ni Mbunge wa Muheza (CCM) alikuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Kamati ilipopitia mpango wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17 ilitoa ushauri katika maeneo 14 yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.

“Mfano wa ushauri uliozingatiwa kwa ukamilifu ni kuhusu kurasimisha katika sheria  a maeneo yote yanayotolewa na mamlaka za mikoa kwa ajili ya matumizi ya jeshi.

“Mfano wa pili ni utekelezaji wa ushauri kuhusu kulipa madeni yote ya wizara yaliyohakikiwa ambayo kati ya Sh bilioni 151.146 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kulipa madeni ya  mkataba, hadi kufikia Machi mwaka huu  Serikali ilikuwa imetoa Sh bilioni 30,” alisema. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles