27.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

UPINZANI WAMSHUTUMU MUGABE KUSABABISHA WASHINDWE UCHAGUZI

HARARE, ZIMBABWE


WAKATI chama tawala nchini hapa kikijitwalia theluthi mbili ya viti bungeni, upinzani umemshutumu Kiongozi mkongwe wa zamani, Robert Mugabe kwa kuwagharimu katika uchaguzi.

Akizungumza na wanahabari, ofisa mwandamizi wa MCD Alliance, Douglas Mwonzora, alisema kitendo cha Mugabe kutangaza kumuunga mkono mgombea wao, Nelson Chamisa, kumewagharimu baada ya wapigakura kukisusa chama chao.

Aidha Mwanzora alidai chama tawala cha ZANU-PF kimewahonga wapigakura wa maeneo ya vijijini.

Uamuzi wa Mugabe kutangaza kumuunga mkono Chamisa siku moja kabla ya uchaguzi, badala ya mrithi wake, Rais Emmerson Mnangagwa, ulimkasirisha mshirika wake huyo wa zamani aliyegeuka kuwa hasimu.

Mnangagwa alimjibu Mugabe, akiwaonya wapigakura kuwa yeye na Chamisa ni kitu kimoja na hivyo kumchagua mchungaji huyo ni kuchagua kivuli cha rais huyo wa zamani.

Kwa sababu hiyo, Mnangagwa aliwataka wapigakura waamue kumpa kura Mugabe waliyemchoka, na ambaye atawarudisha walikotoka au yeye aliyedhamiria kuleta mageuzi.

Lakini pia wapinzani wakiongozwa na Chamisa, wamedai kushinda uchaguzi huo na wameshutumu kitendo cha kucheleweshwa kwa matokeo ya urais kuwa njama za kupika matokeo kumnufaisha Mnangagwa, madai ambayo Tume ya Uchaguzi (ZEC) imeyakana.

Tuhuma hizo zimekuja huku ZANU-PF ikitwaa theluthi mbili ya viti 210 vya ubunge.

Huku viti vitatu tu vikiwa bado kutangazwa, ZANU-PF ilipata viti 144 kulinganisha na 61 vya MDC, ikimaanisha kuwa chama tawala kimepata wingi wa kutosha kukiwezesha kubadili katiba.

Wakati waangalizi wa kimataifa wa Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na ile ya Soko la Pamoja (COMESA) wakiusifu uchaguzi huo kuwa ulikuwa huru, wa haki na wenye ushindani,  wale wa Umoja wa Ulaya (EU) wameorodhesha matatizo kadhaa katika uchaguzi wa urais na ubunge, ikiwamo vitisho, matumizi ya rasilimali za Serikali na kutoaminika kwa Tume ya Uchaguzi.

Aidha waangalizi hao wa EU, ambao ripoti yao ni muhimu katika kuamua kuiondolea vikwazo na kuipatia misaada Zimbabwe, wamehoji kitendo cha kufikia jana alasiri kuendelea kucheleweshwa kwa matokeo ya urais.

Kiongozi wa upinzani, Chamisa, ametuhumu kuwa mchelewesho huo ni mbinu ya kupika matokeo ya uchaguzi ambao amedai ameshinda.

ZEC imekuwa ikidai hakuna udanganyifu bali inahitaji muda zaidi ili kuhesabu kura.

Hata hivyo, EU ilikiri uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na kuna kuimarika hali ya kisiasa, ijapokuwa uwanja haukuwa sawa.

Hii ni mara ya kwanza kipindi cha miaka 16 kwa Serikali kuruhusu waangalizi wa EU na Marekani kutathimini uchaguzi nchini hapa.

Kwa kutazama matokeo yaliyokuwa yakiingia kutoka ZEC mapema jana, ilikuwa dhahiri Zanu-PF itapata wingi wa viti bungeni.

Mchuano katika baadhi ya majimbo ulikuwa wa karibu mno, hali iliyoonyesha viti vingeenda upinzani iwapo MDC haingegawanyika baina ya MDC Alliance ya Chamisa na MDC-T ya Thokozani Khupe.

Iwapo hakuna mgombea atakayepata kura zaidi ya asilimia 50, kutakuwa na uchaguzi wa marudio Septemba 8.

Ni uchaguzi wa kwanza tangu Mugabe kuondolewa madarakani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,044FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles