KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema inashiriki katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ikiwa na moyo mzito kutokana na sintofahamu ya hali ya kisiasa inayoendelea Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo imetupa lawama kwa kile walichodai haipendi Serikali ya Tanganyika kujivika koti la Muungano kutokana na ukoloni unaofanywa Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na msemaji wa kambi hiyo, Ally Abdallah Saleh, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, ambapo alisema tangu kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa Rais na Wawakilishi hadi uchaguzi wa marudio, majeshi ya JWTZ yapo Zanzibar yakiwa na sare kama vile nchi iko vitani.
“Mheshimiwa Spika, kama Jeshi la Tanganyika linatumika kuulazimisha Muungano, ni dhahiri kwamba Muungano huo hauna ridhaa ya wananchi, na kwa sababu hiyo hautadumu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa Serikali hii ya awamu ya tano kwamba:
“Kama kweli ina nia ya kuuenzi na kuudumisha Muungano, basi izingatie maoni ya wananchi waliyoyatoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo wa Muungano ili kuwa na Muungano unaoridhiwa na wananchi wa pande zote mbili za Muungano,” alisema Saleh.
DEMOKRASIA
Akizungumzia hali ya demokrasia alisema kwamba Uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba, 2015 uligubikwa na ukandamizaji wa demokrasia.
Alisema pamoja na hali hiyo, Watanzania walishuhudia uchaguzi uliotoa Rais wa Muungano na wabunge wa Muungano ukitenganishwa na ule ambao vyama vya siasa vilikuwa vikiwania urais wa Zanzibar, uwakilishi na udiwani.
Saleh alisema kwamba chaguzi hizo mbili zilisimamiwa na tume mbili tofauti huru na zenye sheria zake na mamlaka zake, hoja ambayo ndiyo nguzo kuu ya Serikali ya Muungano kukubali uharamia uliofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa madai kuwa haikuwa na nguvu ya kuingilia hali iliyojitokeza Zanzibar ya kubakwa demokrasia.
HASARA ILIYOPATIKANA
Saleh alisema Serikali ya Muungano imeingia hasara ya kukatishwa kwa misaada na Marekani kupitia Shirika lake la Millennium Challenge Corporation (MCC) kwa kiwango cha dola za Kimarekani milioni 473 (takribani shilingi trilioni moja za Kitanzania) ili iweze kuendelea kuibeba CCM na kulazimisha itawale Zanzibar kwa nguvu.
“Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu masharti ya misaada hii ni kukuza demokrasia katika nchi husika. Hivyo Serikali ilivyoamua kubaka demokrasia Zanzibar ilijua athari zake ni pamoja na kupoteza misaada ya namna hiyo. Kwa hiyo, Serikali ya Muungano isijidai kwamba ina uwezo wa kujitegemea na kwa hiyo haihitaji misaada, huo ni uongo kwani hata bajeti ya Serikali ni tegemezi kwa asilimia 37.5,” alisema.
KUVUNJIKA MUUNGANO
Alisema ni wazi kuwa yote yanayotokea Zanzibar ni kutokana na kile alichokiita ‘mawazo-pingu’ kuwa kukiwa na mabadiliko ya uongozi Zanzibar basi Muungano wa Tanzania utavunjika.
Alisema mawazo hayo ni potofu lakini yameshika mizizi ndani ya watu wenye sauti kwenye siasa na usalama nchini.
JANUARY NA MUUNGANO IMARA
Awali akiwasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba, alisema kuwa Muungano upo imara leo kuliko jana.
Alisema wataendelea kutimiza wajibu wao wa kuulinda na kuuimarisha Muungano huo kwa kuwa jukumu la kuimarisha Muungano wamelilia kiapo na linavuka mipaka ya itikadi za kisiasa.
Alisema hadi kufikia sasa ofisi yake imeshughulikia changamoto 11 za Muungano na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu ambapo mwaka 2016/2017 wataendelea kuratibu vikao vya kuondoa changamoto zilizobakia katika utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni mafuta na gesi asili, usajili wa vyombo vya moto, hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zilizokuwa katika Bodi ya Safari ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu ya Tanzania.
MAZINGIRA
Kuhusu mazingira, alisema asilimia 61 ya nchi inatishiwa kuwa jangwa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea nchini.
Alisema kutokana na uharibifu huo kila mwaka wanapoteza hekta 372,000 au takriban ekari milioni moja za misitu hali ambayo ni mbaya kiasi cha kuzorotesha jitihada za maendeleo na ustawi wa Watanzania kwa miaka mingi ijayo.
Alisema katika miaka 10 iliyopita nchi imepoteza eneo la misitu linalolingana na ukubwa wa nchi ya Rwanda ambapo Dar es Salaam peke yake hutumia magunia laki 2 hadi 3 ya mkaa yenye wastani wa kilo 50 kwa mwezi.