Na Fredy Azzah, Dar es Salaam
WAKATI marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakitarajiwa kukutana Dar es Salaam leo kujadili mzozo wa Burundi, wapinzani wa Rais Pierre Nkurunziza, wameapa kwa kusema kuwa ni lazima kiongozi huyo ang’atuke madarakani.
Pamoja na hali hiyo pia wameonya kuwa silaha zinazozagaa kwa wanamgambo nchini humo zikusanywe kwa vile ni hatari hata kwa usalama wa nchi jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Vuguvugu linaloendesha maandamano nchini humo, Chauvineau Mugwengezo, alisema kutano wa wakuu wa nchi za EAC ni lazima uzingatie suala hilo na yanayoendelea nchini mwao.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Paul Kagame (Rwanda), Uhuru Kenyatta (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) pamoja na Rais anayelalamikiwa kwa kutaka kuwania tena muhula wa tatu wa uongozi kinyume cha katiba ya Burundi, Pierre Nkurunziza.
Mugwengezo alisema mkutano huo ambao utakuwa chini ya Mwenyekiti wa EAC Rais Jakaya Kikwete, lazima uhakikishe unaweka mazingira ya uchaguzi nchini Barundi kwa kuwashirikisha wanasiasa wote wa taifa hilo washiriki kwa ukamilifu.
Mwenyekiti huyo wa Vuguvugu la maandamano Burundi alisema masharti mengine ni kuachiwa raia wote waliokamatwa na kuwekwa gerezani kwa sababu ya kufanya maandamano pamoja na kurudishwa viongozi wa siasa waliokimbia nchini humo kwa kuhofia kuuawa kwa sababu ya kumpinga Rais Nkurunziza.
Alisema pia ni lazima Serikali ya Burundi ikubali kuwanyang’anya silaha zote wanamgambo wa Imbonerakure nchini humo.
“Watumie mbinu zote, ziwe za siasa ama kidplomasia, wahakikishe Nkurunziza anaondoka baada ya mihula yake miwili.
“Huo wa tatu ni kuvunja Katiba ya nchi na mkataba wa Arusha ambao Julius Nyerere na Nelson Mandela walihakikisha unafikiwa na ukaipa Burundi amani kwa miaka 10 sasa,” alisema.
Alisema mkataba wa Arusha na Katiba ya nchi hiyo hairuhusu mihula mitatu kwa kiongozi yeyote atakayetawala Burundi.
“Hausemi kuwa uwe umechaguliwa na wananchi wala wabunge, unasema utawala uwe wa mihula miwili, lazima hili liheshimiwe.
“Hata kwenye Katiba ya nchi yetu inaanza kwa maneno; ‘Kwa kuzingatia Mkataba wa Arusha’, hii ina maana kila kitu kinazingatia mkataba wa Arusha,” alisema Mugwengezo.
Alisema nchi za Ulaya, Amerika, Umoja wa Mataifa (UN) na mataifa mengine, yamempa ushauri Rais Nkurunziza lakini bado hataki kuusikia.
Mugwengezo alisema hivi sasa maelfu ya watu wameikimbia nchi hiyo kutokana na kuhofia usalama wao, hasa ikizingatiwa kuwa wanamgambo wa Imbonerakure wanaua raia.
“Hawa wanamgambo wa Imbonerakure wanaweza kumchapa bakora hata ofisa wa jeshi na hakuna anayewazuia. Silaha zilizo mikononi mwao hawa wana mgambo zinatishia hata usalama wa nchi za jirani ikiwamo Tanzania, lazima silaha hii zitoke mikononi mwao,” alisema.
Kiongozi huyo alimtuhumu Rais Nkurunziza kuwa anawasaidia wanamgambo wa Imbonerakure hali ambayo inachangia kuvuruga amani ya nchi hiyo.
Alisema baada ya kufuatilia mazungumzo ya marais hao yatakayofanyika Dar es Salaam, watarudi Burundi kuungana na wananchi wanaoendeleza maandamano.
Burundi imeingia kwenye machafuko baada ya CNDD-FDD kumteua Nkurunziza awania urais kwa muhula wa tatu na hadi sasa watu zaidi ya 10 wamefariki dunia kutokana na mapambano yanayoendelea kati ya waandamanaji na polisi.