23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Upinzani Afrika Mashariki utafanikiwa kung’ara?

Na Joseph Odhiambo, Nairobi


HAPA swali kuu ni, je, vyama vya upinzani katika eneo la Afrika Mashariki na Kati bado viko hai? Hili ni jambo muhimu katika mustakabali wa kisiasa katika nchi zote za Rwanda, Tanzania, Uganda, Kenya, Sudan Kusini na Burundi.

Mbunge wa Uganda, Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine, akihutubia mkutano wa kisiasa wa hadhara mjini Nairobi nchini Kenya mwishoni mwa wiki hii, alisikitishwa sana na hali ya kisiasa katika Bara la Afrika na hasa Afrika Mashariki.

Alisema kwa muda mrefu demokrasia katika Afrika imekuwa ikiminywa na watawala hivyo kuzima sauti na uwezo wa vijana huku ufisadi, mapendeleo na uongozi mbaya ukikithiri.

Ndio maana katika ziara hiyo yake nchini Kenya, Bobi Wine, aliungana na mbunge chipukizi wa Kenya, Babu Owino pamoja na wabunge wengine kuanzisha vuguvugu jipya la vijana “Youth For Africa Movement”.

Katika mikutano miwili mikubwa ya kisiasa jijini Nairobi, Bobi Wine na wabunge wenzake chipukizi kutoka Kenya walisema vuguvugu hilo jipya la vijana lina lengo la kupanua demokrasia, kuwapa vijana wa Bara la Afrika sauti na uwezo kuhusu masuala ya uongozi na usimamizi ili kuboresha maisha yao.

“Tumekuja hapa si kuomba bunduki, sisi hatuna haja ya kumuua yeyote, hatutaki umwagikaji wa damu. Tumekuja kutafuta urafiki na kuungana na nyinyi ili tupiganie uhuru wa mamilioni ya wanaonyanyaswa barani Afrika ambao wengi wao ni vijana,” alisema katika mojawapo ya mikutano hiyo jijini Nairobi.

“Pakiwa na maonevu na uongozi wa kiimla nchini Uganda, hii inaathiri si Waganda tu. Ikiwa jambo lolote baya litafanyika nchini Kenya, hii pia inaiathiri Uganda na kadhalika,” alisema huku akishangiliwa.

Ili kuunganisha viongozi vijana barani Afrika viongozi wa vuguvugu hilo jipya la vijana wamepanga kuwa na mkutano mwengine mkubwa wa hadhara jijini Nairobi Novemba mwaka huu ambao utahudhuriwa na viongozi wengine chipukizi kama vile Julius Malema wa Afrika Kusini, Nelson Chamisa, aliyegombea urais wa Zimbabwe katika uchaguzi mkuu hivi karibuni.

Nchini Tanzania nako kumekuwa na malalamiko kuwa demokrasia imekuwa ikiminywa huku mambo mengine yakifanyika kana kwamba nchi hiyo ni ya chama kimoja ilhali kuna vyama vingi vya kisiasa.

Freeman Mbowe ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema. “Tunakuwa na vyama vingi katika maneno na katika karatasi, lakini katika matendo tunatengeneza mfumo wa chama kimoja, nchi hii itazama.”

Lakini kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nchini Tanzania mambo hayakuwa hivi. Kulionekana kuwa na ushindani mkubwa wa kisiasa na wa wazi ncini humo.

Na Oktoba 29, 2015 Rais John Magufuli, alipotangazwa mshindi kwa kura 8,882,935, wadadisi wengi wa kisiasa walibashiri kwamba Edward Lowassa aliyeibuka wa pili kwa kura 6,072,848 angeihangaisha Serikali hiyo mpya na kuwa mkosoaji wake mkubwa. Hata hivyo, mambo hayakuwa hivyo.

Januari mwaka 2018, Lowassa alizuru Ikulu kukutana na Rais Magufuli na baada ya ugeni huo katika hutuba yake alimsifu sana rais wa Tanzania.

“Kwanza nimepata faraja sana kuja ikulu. Mimepata nafasi nzuri ya kuzungumza naye. Kwanza nikupongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, anafanya kazi nzuri nchini, anahitaji kutiwa moyo.”

Tukirudi nchini Kenya mambo si tofauti sana. Tangu Machi 9, mwaka huu kiongozi wa upinzani, Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, walikutana na kufanya mazungumzo marefu katika ofisi rasmi ya Rais. Mwishowe wakachomoza na kupeana mikono ya urafiki na kuahidi kufanya kazi pamoja.

Tufauti na uhasama mkubwa wa kisiasa uliodumu kwa miaka na hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ambapo upande wa Serikali ikiongozwa na Rais Kenyatta na upinzani mkuu chini ya Odinga, baada ya mkutano huo wawili hao walionekana wakizungumza lugha moja na hata kuitana “Ndugu yangu”.

“Tumekuja pamoja na ndugu yangu Uhuru Kenyatta tumeongea kwa kirefu na tumekubaliana ya kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja.”

Kutokana na matamshi hayo ya Odinga, wachanganuzi wengi na hata raia wa kawaida walisema sasa upinzani umekufa nchini Kenya.

Rwanda nako upinzani wa kisiasa wa haja ni kama hakuna. Wadadisi wengi walidhani pengine wanasiasa, Victoire Ingabire Umuhoza na mwanasiasa mwingine wa hivi majuzi tu Diane Rwigara, wangemtia Rais Paul Kagame homa ya kisiasa, lakini mambo yalikuwa kinyume.

Ingabire alikamatwa na hatimaye kufungwa jela miaka 15 kwa makosa ya ugaidi pamoja na kuhatarisha usalama wa kitaifa. Hata hivyo, sasa yuko huru baada ya kupewa msamaha na Rais Kagame.

Naye Diane Rwigara alianzisha kampeni za kutaka kumwondoa Rais Kagame uongozini lakini juhudi zake hazikufika mbali. Tume ya Uchaguzi nchini Rwanda ilimzuia kushiriki kutokana na kutotimiza masharti yaliyohitajika. Baadaye alikamatwa na kushtakiwa kutokana na makosa kadhaa ya jinai yakiwemo kughushi nyaraka.

Burundi nako kwa sasa hakuna upinzani wakumsumbua Rais Pierre Nkurunziza kisiasa. Kwa wengi ishara zimekuwepo tangu kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa kuchaguliwa na kuwa Naibu Spika wa Bunge la Burundi.

Pia wakati chama chake Rwasa cha National Liberation Forces (NLF) kuamua kumtimua kiongozi huyo na viongozi wapya wakaamua kumuunga mkono Rais Nkurunziza, ilionekana kuwa mwanzo wa kifo cha upinzani. Wabunge wa upinzani Burundi walipochaguliwa na kujiunga na baraza la mawaziri, ilikatisha wengi tamaa ya kuwa na upinzani wa nguvu wa kisiasa nchini humo.

Makala haya kwa hisani ya BBC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles