22.7 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Upelelezi kesi ya Mchungaji Gwajima wakamilika

gwajimaNA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
UPELELEZI wa kesi inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima na wenzake watatu umekamilika na kesi inatarajiwa kuanza usikilizwaji wa awali Julai 2, mwaka huu.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro aliifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, Kimaro alidai kesi ilikuwa inatajwa, lakini upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Riwa aliyakubali maombi ya upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hadi Julai 2, mwaka huu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni msaidizi wa askofu huyo, Yekonia Bihagaze (39), mfanyabiashara George Mzava (43) na mkazi wa Kimara Baruti, Geofrey Milulu (31).
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima anadaiwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika Packers Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwamba ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu wa amani.
Katika kesi ya pili namba 84, Gwajima anakabiliwa na shtaka moja la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi kinyume cha sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kwamba kati ya Machi 27 na 29, mwaka huu ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802 , risasi tatu za pisto na risasi 17 za shotgun.
Shtaka la pili na la tatu linawakabili washtakiwa waliobaki ambao wanadaiwa kwamba Machi 29 mwaka huu katika Hospitali ya TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi hizo bila ruhusa kutoka mamlaka husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles