Asha Bani-Dar es Salaam
Upatikanaji wa taarifa kamili kuhusu rushwa ya ngono bado ni tatizo kubwa kutokana na jambo hilo kuonekana kuwa la usiri katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 26 na Mkurugenzi wa Mfuko wa Uhifadhi Wanawake Tanzania (WFT), Mary Rusimbi wakati wa kongamano la kujadili masuala ya Rushwa ya ngono ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Kongamano hilo limeandaliwa na Mfuko wa Wanawake nchini (WFT), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) na mabalozi wa nchi za Ireland na Uholanzi likiwa na kaulimbiu ‘Kataa rushwa ya Ngono Jenga Kizazi chenye usawa’.
Amesema ni vema mapambano juu ya rushwa ya ngono yanahitaji kuongozwa na utafiti ili kujua ni wapi wanaweza kuanzia katika kupambana na rushwa hiyo ambayo ni jambo la kikatili.
“Hadi sasa kuna asilimia 98 ya unyanyasaji wa kijinsia hivyo ni muhimu jambo hili kushirikisha watu wote hususani ngazi za familia kutoa ushirikino na kuhakikisha watu wanaofanya vitendo hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema Mary.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi, Janeth Magomi amesema jeshi hilo ni wasimamizi wa sheria na wamekuwa wakifanya kazi katika shuleni, vyuoni na maofisini katika kuhakikisha wanatoa elimu juu ya rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia.
Naye Mkurugenzi wa Tamwa, Rose Reuben amesema kulazimisha ngono na kutoa rushwa ya ngono kwa namna yeyote ni kosa la jinai.
“Jamii ina jukumu kubwa la kutoa taarifa na kuhabarishana kwasababu rushwa ya ngono ina madhara makubwa ikiwamo maambukizi ya maradhi ya ugonjwa wa Ukimwi kuongezeka kwa kasi.
“Maadili kwa sasa yamebadilika na teknolojia imeongezeka, hivyo ni vyema taarifa za rushwa ya ngono na unyanyasaji mwengine wa jinsia ufanyiwe kazi na upingwe kwa kuunganisha nguvu ya pamoja na wadau mbalimbali,” amesema Rose.