UPASUAJI MAJERUHI WA MWISHOLUCKY VINCENT WAFANIKIWA

0
1348
Wanafunzi watatu ambao ni majeruhi wa ajali ya basi wakisikiliza sala na pole kwa viongozi mbalimbali waliojitokeza kuwasindikiza, watoto hao wameondoka jana kwenda nchini Marekani kwa matibabu zaidi.(Picha na Veronicah Mheta)

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MADAKTARI wa Hospitali ya Mercy, Sioux City nchini Marekani, juzi walifanikiwa kumaliza kumfanyia upasuaji mkubwa wa mti wa mgongo Doreen Mshana, ambaye ni majeruhi wa ajali iliyohusisha wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent, iliyopo Arusha.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, ambaye ni mmoja wa waasisi wa Taasisi ya Elimu na Afya (STEM), (Sioxland Tanzania Educational Medical Ministries), alisema Doreen, ambaye ni miongoni mwa majeruhi watatu, alifanyiwa upasuaji huo kwa muda wa saa nne badala ya tano zilizokuwa zimepangwa na madaktari.

“Mtoto Doreen amemaliza kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo kwa ufanisi mkubwa kupita matarajio waliyojiwekea,” alisema Nyalandu.

Alisema zoezi hilo, ambalo lilikuwa chini ya usimamizi wa madaktari sita, wakiwamo Dk. Meyer na Dk. Durward, ambao ni madaktari bingwa, lilipaswa kufanyika kwa muda wa saa 5:30, badala yake lilikamilika ndani ya saa nne.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kwa sasa Doreen ameshatolewa chumba cha upasuaji na kupelekwa katika chumba cha watu mahututi (ICU), huku madaktari wakieleza kuridhishwa na hali ya mtoto huyo.

“Kwakuwa hali yake imeridhisha sana, baadaye leo (jana) watamtoa ICU ambako wamempumzisha baada ya upasuaji na kumrudisha wodi ya watoto  ambako ataendelea na mapumziko,” alisema Nyalandu.

Doreen na wenzake wawili, Saidia Ismail na Wilson Tarimo, wapo nchini Marekani kwa ajili ya matibabu baada ya kupata ajali mbaya ya gari kwa msaada wa Shirika la STEMM.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here