Na Malima Lubasha, Serengeti
MKUU wa Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, Kemirembe Lwota ametoa siku saba kwa uongozi wa Kijiji cha Nyamihuru Kata ya Busawe, Tarafa ya Ngoreme, kukutana haraka na wananchi waliovamia eneo la shamba la kijiji ili kuzungumza na kukubaliana namna ya kumaliza mgogoro wa ardhi uliopo ambao umekwamisha ujenzi wa sekondari mpya.
Lwota ametoa maagizo hayo Agosti 2, 2024 wakati alipofika eneo hilo lililotengwa na kijij kwa ujenzi wa Sekondari hiyo na kusikiliza maelezo ya uongozi na malalamiko ya wananchi.
Amesema kuwa katika kusikiliza maelezo ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamihuru, David Mugendi pamoja na wavamizi ambao inadaiwa wapo 19 alibaini kuwa kulikuwa na udhaifu wa uongozi wa kijiji na kuwaagiza mwenyekiti, mtendaji wa Kata na katibu Tarafa kukutana na wananchi hao ili kuondoa mchangamoto hiyo ya ardhi na ifikapo tarehe 10 mwezi huu apewe taarifa walivyokubaliana.
Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa Serikali imetoa fedha zaidi ya Sh. 500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari mpya katika kijiji hicho ili kuwapunguzia mwendo watoto kutembea umbali mrefu lakini watu wachache wamekwamisha.
“ Mimi kama Mkuu wa Wilaya sitakubali kuona fedha hizi zinarudishwa serikalini eti wananchi wa kijiji cha Nyamihuru wamekataa kupisha eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa sekondari naagiza viongozi wa ngazi zote wa Kata na Tarafa wakiwamo wananchi mlimalize tatizo hili nitakuja kupewa majibu kuwa limekwisha tuanze ujenzi,”amesema Lwota.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambaye pia ni Diwani Kata ya Busawe, Ayubu Makuruma amesema eneo hilo lilikuwa ni shamba la kijiji wananchi wakilima mazao mbalimbali alishazungumza na wananchi waliokuwa wamejenga eneo hilo baadhi kwa hiari yao wameamua kuondoka baada ya kuona umuhimu wa kujenga shule ya sekondari eneo hilo.
Amesema serikali imetoa fedha kwa ajili ya kujenga sekondari eneo hilo kwa faida ya watoto ambao wanatembea umbali wa kilometa 32 kwenda na kurudi kutoka shule jambo ambalo limepokelewa vizur na wananchi wa kijiji hiki na kukubali kuanza kuleta mchanga, mawe na kufanya usafi eneo la ujenzi kama nguvu kazi yao na kumuomba mkuu wa wilaya kuona anamalizaje changamoto iliyojitokeza.
“ Mkuu wa Wilaya umesikiliza maelezo na malalamiko ya wananchi hawa waliovamia eneola kijiji waki wamo viongozi wa chama nikuombe urudi tena kuzungumza na wananchi wote wa kijiji uwasikilize na kutoa maelekezoya serikali,”amesema Makuruma