Na JUSTIN DAMIAN,
SEHEMU nyingi duniani, watu wanapenda kunywa kahawa ingawa kwa hapa Tanzania wanywaji ni wachache. Kahawa husaidia kumfanya mnywaji kujisikia vizuri baada ya muda mwingi wa kufanya kazi. Hata hivyo, wapo baadhi ya watu ambao hufikiri kuwa kahawa ni mbaya kwa afya.
Lakini utafiti mpya uliofanywa na Chuo Kikuu cha Edinburg na Southmpton nchini Uingereza umeonyesha kuwa unywaji kahawa unamlinda mnywaji kupata ugonjwa wa saratani ya ini ambao ni hatari na hauna tiba.
Watu ambao wanaiponda kahawa wanasema, kinywaji hicho kina caffeine ambayo inasababisha ugonjwa wa moyo na kuwafanya wanaougua magonjwa ya moyo kufariki mapema zaidi. Tofauti na mtizamo huo, sasa wanasayansi wanasema utumiaji mzuri wa kahawa unaweza kumwepusha mtumiaji na hepatocellular carcinoma ambayo ni aina ya saratani ya ini.
Timu kubwa ya watafiti walichunguza data kutoka kwenye tafiti 26 zilizohusisha zaidi ya washiriki milioni mbili. Watafiti hao waliobobea kwenye masuala ya afya ya umma, waligundua kuwa saratani ya ini aina ya hepatocellular carcinoma ilikuwa ikiwaathiri takribani watu 50 katika kila watu 1000 waliwachunguza katika utafiti huo. Hata hivyo, waligundua kuwa katika kundi la wanywaji wa kahawa, watu 33 walionekana kuwa wameathirika kati ya watu 1000 ikiwa ni upungufu wa asilimia 40 ukilinganisha na kundi la wasiokunywa kahawa.
Watafiti hao pia waligundua kadiri unavyokunywa kahawa zaidi, ndivyo ambavyo unapunguza uwezekano wa kupata aina hii ya saratani. Timu hiyo ilisisitiza kuwa unywaji wa kikombe kimoja cha kahawa yenye caffeine inapunguza uwezakano wa kupata ugonjwa huo usio na tiba kwa asilimia 20 huku unywaji wa vikombe viwili vya kahawa ukiwa unapunguza uwezekano kwa asilimia 35.
Hepatocellular carcinoma inashika nafasi ya pili kati ya magonjwa wa saratani yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani. Kujilinda dhidi ya ugonjwa huu ni jambo jema kwa kuwa hauna tiba lakini pia wanasayansi hao wanasisitiza unywaji kahawa uliopindukia si salama kwa afya ya mtumiaji na hivyo kuwataka watumiaji watumie kwa kiasi.
Wanasayansi wanawezaje kujua ni kiasi cha kahawa mnywaji akitumia hakiwezi kumletea madhara ya kiafya? Dk. Oliver Kennedy wa Chuo Kikuu cha Southampton anasema; “hatua inayofuata ni kwa watafiti kuchunguza ufanisi kupitia utafiti usiochagua sampuli maalum kwa kuzingatia wanywaji wa kahawa ambao wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huu, watu wengi walichangia katika mafanikio ya utafiti huu.”
Pamoja na faida hiyo, unywaji kahawa una faida nyingi ikiwamo kupunguza maumivu ya misuli baada ya kazi. Unywaji kahawa wa kiasi pia unapunguza uwezekano wa kupata ungonjwa kisukari namba mbili – Diabetes Type 2. Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani unaonyesha kuwa unywaji wa kikombe kimoja cha kahawa kwa siku unapunguza uwezekano wa kupata aina hiyo ya kisukari kwa asilimia tisa.
Unywaji kahawa pia unapunguza uwezekano wa kujiua pamoja na mfadhaiko (depression). Utafiti uliofanyika kwa kipindi cha maika 10 uliohusisha wauguzi wanawake 86,000 ulionyesha kupungua kwa uwezekano wa kujiua kwa wale waliokuwa wakitumia kahawa. Utafiti mwingine ulifanyika na Shule ya Afya ya Umma ya Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani ulionyesha kuwa wanawake wanaokunywa vikombe vine au zaidi vya kahawa wanapunguza uwezekana wa kupata mfadhaiko kwa asilimia 20.