Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) Tanzania wameungana na Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji kuadhimisha kumbukizi ya miaka 30 ya Mpango wa ufadhili wa Taaluma wa Wakimbizi wa Albert Einstein (DAFI) huku Serikali ya Ujerumani ikitoa msaada wa kifedha kuwawezesha wakimbizi vijana kuhitimu elimu ya juu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 7, na UNHCR, Mpango huo umewanufaisha wanafunzi zaidi ya 22,500 kutoka nchini 55, Tanzania ikiwemo.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na uzinduzi wa semina iliyohusu Haki za Wakimbizi na Ulinzi wa Wakimbizi Kimataifa iliyofanyika Julai mwaka huu katika Chuo Kikuu cha Iringa huku wakati jana, yakifanyika jijini Dar es Salaam, viongozi mbalimbali waandamizi na wawakilishi wa UNHCR, Wizara ya Mambo ya Ndani na Ubalozi wa Ujerumani walihudhuria.
Katika kuhitimisha sherehe hizo wanafunzi wawakilishi wa DAFI, washiriki na watumishi wa chuo kikuu hicho walifanikiwa kupanda miti zaidi ya 30 huku kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma nao wakiadhimisha siku hiyo.
Mpango huu nchini Tanzania ulianzishwa mwaka 1994 na mpaka leo zaidi ya wakimbizi 460 wamenufaika kutokana na ufadhili huu kwa kuruhusiwa kwenye vyuo vya ndani kikiwemo Chuo Kikuu cha Iringa, Dodoma, Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Muhimbili, Dar es Salaam.
Akizungumzia ufadhili huo, Yanik Yankeu, Afisa Elimu wa UNHCR Tanzania amesema, nafasi hizo huwanufaisha wanafunzi ambao ni wakimbizi kusaidia nchi zao halisi baada ya kujitolea katika nchi zinazowapokea.
“Programu ya DAFI Scholarship ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wakimbizi kufuata
masomo yao katika ngazi ya elimu ya juu nchini Tanzania,” amesema.
Naye Naibu mwakilishi wa UNHCR, George Kuchio katika hotuba yake ya ufunguzi alisema, “Kama tutawapatia elimu wakimbizi, tunashiriki katika kutatua matatizo yalichangia kuleta mtikisiko uliowasababishia kukimbia nyumba zao,” amesema.
Naye mwanafunzi wa kompyuta Sayansi, Amina Ismail Haji akizungumza kwa niaba ya wanufaika wengine ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwalinda na kuwaruhusu kupata elimu sambamba na kueleza vikwazo wanavyovipata kama wakimbizi akitaja ucheleweshwaji wa ruhusa na gharama za maisha.
Kwasasa wakimbizi wanaopata elimu nje ya mfumo nchini Tanzania ni chini ya asilimia moja huku ukosefu wa mtaala rasmi wa elimu ya wakimbizi kitaifa pamoja na lugha vikitajwa kuwa vikwazo.