30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

UNG’ANG’ANIZI WA BIYA NA ‘KUFELI’ KWA SIASA CAMEROON

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM                |                       


CAMEROON ni Taifa lisilotulia kuanzia maisha ya kawaida hadi ya kisiasa zake kutokana na wingi wa migogoro, mivutano na siasa dhaifu zilizokosa dira na tiba kwa miaka mingi sasa.

Migogoro hiyo imegeuka kuwa katili huku majeshi ya Serikali yakipambana na wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mwa nchi na waasi watakao kujitenga wa eneo lizungumzalo Kiingereza (Anglophone) wakisumbua kaskazini na kusini magharibi mwa nchi.

Asilimia 20 ya wakazi milioni 24.6 wa taifa hilo wanazungumza Kiingereza na walio wengi Kifaransa.

Lakini utawala wa wanasiasa wazungumzao Kifaransa (Francophone) pasipo usawa ni chanzo cha mgogoro wa muda mrefu nchini humo.

Hilo linawakasirisha wazungumzao Kiingereza walio wachache waishio magharibi mwa nchi wanaolalamika kutengwa, kukandamizwa na kukosa uwakilishi wa kutosha na mfaidiko sawa wa ulaji wa keki ya taifa hilo.

Uwakilishi wa wanasiasa wazungumzao Kiingereza katika ngazi mbalimbali za kijamii umeanguka mno tangu Shirikisho la Jamhuri ya Cameroon lilipokuwa Jamhuri ya Muungano wa Cameroon mwaka 1972.

Ikumbukwe kabla ya 1961, eneo la kusini mwa Cameroon lilikuwa likitawaliwa na Uingereza kutokea Nigeria. Kisha likaunganishwa kujiunga na Jamhuri ya Cameroon.

Kutokana na kuwa na pande mbili sasa Francophone na Anglophones ikakubaliwa kuwepo serikali ya kugawana madaraka. Lakini makubaliano hayakuheshimiwa, Wazungumzao Kifaransa wakatumia wingi wao kukandamiza Anglophone, ambao uwakilishi ukazidi kupungua miaka hadi miaka,

Hali hiyo, ndiyo chanzo cha miito ya kutaka eneo hilo lizungumzao Kiingereza, kujitenga kutoka Cameroon huku likishuhudia migomo na maandamano ya mara kwa mara dhidi ya serikali.

Matumizi ya nguvu ya jeshi katika mgogoro huo na ule dhidi ya BokoHaramu ukashuhudia mamia wakiuawa na wengine 180,000 kukimbia makazi.

Wanaharakati wa Anglophone wanaotaka kuundwa kwa Jamhuri ya Ambazonia, wameonya kwamba hawataruhusu uchaguzi wowote utakaoendeshwa na utawala wa Yaoundé kufanyika katika ‘nchi yao.’

Lakini chama tawala Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM kimeapa kwamba lazima uchaguzi ufanyike eneo hilo na kwamba Wacameroon wana haki ya kwenda kupiga kura au la.

Ushahidi wa kutisha wa mauaji yanayoendeshwa na majeshi ya usalama, ambayo yamejitokeza wiki za hivi karibuni yameashiria ukubwa wa matatizo yanayoikabili nchi.

Lakini Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 7, ambao ungepaswa kuleta suluhu ya matatizo hayo, unatarajia badala yake kuyaongeza.

Paul Biya, ambaye ameitumkia Cameroon kama rais kwa miaka 36, akiwa na umri wa miaka 85, kwa mastaajabu ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda muhula mwingine madarakani.

Lakini je, Wacameroon, ambao zaidi ya asilimia 60 ni vijana wenye umri chini ya miaka 35, wanaamini nchi yao iko katika mwelekeo sahihi?

Licha ya yote kuna viashiria fulani vinavyoibeba Cameroon. Ukuaji wa uchumi kwa ujumla unatia moyo licha ya kupunguza kasi yake katika miaka ya karibuni, na ukosefu wa ajira umeelezwa kuwa chini, hasa unapoulinganisha na mataifa jirani.

Lakini pia bado wananchi wengi wanaishi katika umasikini na nchi hii ni miongoni mwa mataifa 25 yanayoongoza katika orodha ya mataifa yanayonuka rushwa duniani kwa mujibu wa taasisi ya Transparency International.

Tofauti na viongozi wengine walio madarakani kwa miaka mingi, Biya si sehemu ya maisha ya kila siku ya Wacameroon wengi.

Akikosolewa kama rais kivuli kwa sababu ya safari zake ndefu na za mara kwa mara nje ya nchi, Biya huendesha shughuli za serikali kwa rimoti akiwa hotelini nje ya nchi kwa muda mwingi.

Baraza lake la mawaziri hukutana kwa nadra mno kama ilivyotokea mapema mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza kipindi cha miaka miwili.

Na maelezo yake ya kwanini anataka kuongoza kwa muhula mwingine wa saba madarakani ni kwamba eti watu wengi bado wanampenda na wamemshawishi kwa kumlilia na kumpigia magoti aendelee kubaki madarakani.

Hata hivyo, inahesabiwa kuwa mwiko kuzungumzia uking’ang’anizi wake madarakani.

April 2016, baadhi ya wafuasi wa upinzanin akiwamo mgombea urais wa mwaka 2011,  Edith Kah Walla walikamatwa na kushikiliwa katika mji mkuu wa Yaoundé baada ya kuandamana kumpinga Biya na dhidi ya ukandamizaji wa sauti zinazopinga jaribio lake la kutaka kuwa ‘rais wa maisha.’

Hata hivyo, njia mpya kushughulikia tatizo hilo ya kumng’oa kihalali haionekani kuwa njiani bado.

Bado upinzani wa nchi hii licha ya kutamani kumng’oa Biya, umeparanganyika na mara nyingi hauna nguvu.

Wagombea 28 wamejitokeza kugombea urais, upinzani ukishindwa kukubaliana mgombea mmoja huku wengine 20 wakijitokeza kuwania kiti hicho cha enzi lakini wakimuunga mkono Biya. Ajabu sana!

Kila mfumo wa uwakilishi kidemokrasia na ufanisi hasa ujenzi wa ushirika imara wa upinzani, ambao ungepaswa kuwa suluhu hauna matumaini kabisa.

Pengine haishangazi, baadhi wameamua kuchukua uamuzi wa kutaka kujitenga. Cameroon inaonekana kukabiliana na si tu na kukosekana kwa uongozi fanisi bali pia uwapo wa siasa zilizoshindwa.

Rais Biya ni mtawala anayeshika nafasi ya pili kwa kutawala muda mrefu barani Afrika. Amepitwa na mwenzake wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang’ Nguema Mbasogo tu kwa miaka mitatu. Biya aliingia kwa mara ya kwanza Ikulu Novemba 6, 1982, wakati taifa hilo likiwa chini ya mfumo wa chama kimoja.

Hata hivyo, licha ya taifa hilo kuwa katika zama za mfumo wa vyama vingi, Biya amefanikiwa kusalia mamlakani kwa miaka hii yote kwa mbinu zikiwamo ubabe, ulaghai na rushwa.

Mwaka 2011, baada ya Katiba ya taifa hilo kufanyiwa mabadiliko yenye utata ya kumruhusu kuwania kiti cha urais tena, alifaulu kushinda tena uchaguzi mkuu kwa asilimia 78 ya kura zote zilizopigwa na kusalia mamlakani kwa miaka mingine saba.

Ushindi huo mkubwa, uliwafanya wakosoaji wake wengi kuhoji na kushuku uhalali wa uchaguzi huo kiasi cha jina la mtaalamu wa wizi wa kura kumkaa vilivyo.

Akifahamika kama Simba Mtu’, jina la utani alilipata baada ya kudumu katika siasa za juu kwa muda mrefu, likitoka katika timu ya taifa ya mpira wa miguu, maarufu kama ‘Simba Wasioshindika,’ wakati ilipoingia robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1990, kiongozi huyo lakini pia amekuwa akitumia mbinu za mnyama huyo tangu mwanzo.

Alizaliwa katika kijiji kilichopo kwenye msitu wa ikweta kusini mwa Cameroon, akaja someshwa na wamisionari wa Kikatoliki katika seminari ya karibu, akiwa na ndoto ya kuwa padri.

Lakini baadaye, akachagua kusomea sheria na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Paris.

Alipohitimu akarudi nyumbani kufanya kazi katika utumishi wa umma.

Mtaalamu huyo mfupi akapanda ngazi akishika nyadhifa andamizi na kuondokea kuaminiwa na Ahmadou Ahidjo, ambaye alikuwa mkuu wa nchi tangu uhuru upatikane mwaka 1960.

Akawa waziri mkuu mwaminifu wa Ahidjo kwa miaka saba, hadi mwaka 1982 – wakati kwa mshangao wa wengi Ahidjo alipotangaza kujiuzulu urais na kumkabidhi madaraka Biya.

Ahidjo alishikilia uenyekiti wa chama tawala akidhani kuwa ulikuwa na nguvu zaidi kuliko nafasi ya urais.

Lakini Biya, alikuwa mwepesi katika kuvizia na kushambulia, akawaondoa wafuasi wa Ahidjo na hivyo kumlazimisha baba huyo wa uhuru kukimbilia uhamishoni.

Baadaye akajikuta akinusurika kupinduliwa mara mbili, tukio la kwanza likiwa mwaka 1983 na lingine mwaka mmoja baadaye.

Ahidjo alinyooshewa kidole kama mhusika mkuu wa njama hizo na mahakama ya kijeshi ikamhukumu adhabu ya kifo akiwa hayupo.

Kiongozi huyo wa uhuru akafariki dunia, baadaye nchini Senegal, na mwanafunzi wake huyu wa zamani aliyemgeuka hakuwa tayari kuuruhusu mwili wa mwalimu wake huyo kuletwa nyumbani kwa mazishi.

Biya pia alionesha ubaya kwa kipindi cha miaka mingi kwa washirika wake walioonesha kukinyemelea kiti chake hicho.

Mmoja wa madaktari wake yuko jela kwa tuhuma za rushwa, waziri wa zamani wa mambo ya ndani ndiyo ameanza hivi karibuni kutumikia kifungo cha miaka 25 jela kwa tuhuma kama hizo; waziri mkuu wa zamani anakabiliwa na kesi huku wengine wawili wakiwa wamekimbilia uhamishoni.

Hata hivyo, amekuwa akikwepa kujenga urafiki nao, akijiweka mbali na baraza la mawaziri – baadhi ya mawaziri wanateuliwa na kutimuliwa bila hata kuonana na rais kipindi chote wakiwa nyadhifani.

Katika jukwaa la kimataifa, pia ameonesha nguvu zake halisi – akimlazimisha jirani mwenye nguvu zaidi wa Cameroon, Nigeria kukabidhi Peninsula yenye utajiri ya Bakassi.

Awali nchi hizo mbili zilikuwa zimepambana mara kadhaa kugombea eneo hilo tajiri kwa mafuta na Biya aliamua kwenda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuamua kesi hiyo.

Aidha Biya alidai kuwa anataka kukumbukwa kwa kuleta demokrasia nchini Cameroon.

Ni baada ya kusalimu amri kwa shinikizo la kuhitimisha mfumo wa chama kimoja na mwaka 1992 alishinda uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo kwa asilimia 40 tu ya kura huku kukiwa na tuhuma za wizi wa kura.

Mpinzani wake mkuu, John Fru Ndi anaaminika kuwa alishinda uchaguzi huo, lakini Jaji wa Mahakama Kuu alimtangaza Biya mshindi.

Tangu, hapo rais akaja na mbinu zilizomshuhudia akishinda uchaguzi mmoja baada ya mwingi na hajawahi kupata chini ya asilimia 75 ya kura.

Wakosoaji wake wanasema rais na washirika wake wamehakikisha Wacameroon hawana chaguo lingine zaidi yake, huku chama chake kikihakikisha kinashinda kila chaguzi kwa kutumia mbinu zote.

Ni hilo lililomfanya pia abatizwe kuwa mtaalamu wa wizi wa kura.Na rushwa ni suala lililotawala uongozi wa Biya kipindi chote akiwa madarakani.

Licha ya kuanzisha tume ya kuzuia rushwa, bado saratani hiyo adui wa haki imejikita mizizi katika kada zote za jamii na kukwamisha maendeleo ya nchi, na kuifanya Cameroon ishinde taji kama nchi inayonuka rushwa kuliko zote duniani mara mbili katika miaka ya 1990.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles