24.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

UNFPA yakabidhi jengo la Wazazi na vifaa tiba Hospitali ya Rufaa Amana

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa na Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA) limekabidhi jengo la wazazi na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini Dar es Salaam.

Aidha, limetoa sare maalum kwa waendesha bodaboda wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kuhamasisha chanjo ya Uviko-19.

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Lungwa(katikati) akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Meneja wa Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka UNFPA, Felista Mbawana amewaambia waandishi wa habari kwenye hafla hiyo iliyofanyika hospitalini hapo Julai 26, 2022 kuwa kukabidhi jengo hilo kutawasaidia wakina mama kujifungulia sehemu salama.

Amesema gharama ya ukarabati huo pamoja na vifaa vingine vilivyotolewa ni Sh milioni 400.

“Katika mradi wa kukabidhi jengo hili na vifaa tiba ikiwamo na sare za bodaboda wa jijini Dar es Salaam gharama ya vitu vyote inafikia kiasi cha Sh milioni 400.

“Kuhusu sare hizi za bodaboda tumezitoa tukiamini kwamba wanapovaa sare hizo watasaidia kuhamasisha jamii kuchanja chanjo ya Uviko-19 hatua ambayo itasaidia jamii yetu kuwa salama kwani hatuwezi kuwa salama hadi pale kila mmoja wetu atachanja,” amesema Felista.

Felista ameongeza kuwa wanawake wanahitaji huduma ya uzazi hivyo wakashirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuboresha huduma hiyo.

“Ujio wa janga la Uviko-19 kwa mara ya kwanza kulikuwa na changamoto nyingi hasa kwa wanawake wajawazito hivyo ikatulazimu kuboresha huduma za afya ya uzazi ikiwamo ukarabati wa jengo,” amesema Felista.

Wanawake waliojifungua.

Katika hatua nyingine Felista amewasihi wanawake wajazwazito kufika kwenye vituo vya kutolea huduma badala ya kubaki nyumbani.

“Wakina mama wanatakiwa kufika kupata huduma ya afya ya uzazi katika vituo vya afya ili waweze kujifungua sehemu iliyosalama kuliko kubaki nyumbani jambo ambalo siyo salama sana,” amesema Felista.

Awali, Mwakilishi Makazi wa UNFPA Tanzania, Mark Bryan Schreiner alisema kuwa utafiti wa ‘Mwelekeo wa Vifo vya Wajawazito’ wa Shirika la Afya Duniani(WHO) na washirika wa Umoja wa Mataifa, kwa kulinganisha takwimu za kimataifa, unabainisha takwimu za vifo vya uzazi nchini Tanzania ziko ‘juu sana’.

Mwakilishi Makazi wa UNFPA Tanzania, Mark Bryan Schreiner akizungumza katika hafla hiyo.

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Lungwa aliwashukuru UNFPA kwa kutoa msaada wa wodi ya wanawake na watoto ikiwamo vifaa vya afya na lezi za waendesha bodaboda.

“Tunatambua kwamba kila moja ya maisha haya yanayopotea kutokana na vifo vinavyoweza kuzuilika kwa watoto wachanga na wajawazito ni mengi mno. Bahati mbaya sana kwa wanawake na wasichana wengi, hasa wale waishio vijijini, wanapohitaji sana huduma za afya ya uzazi, zahanati ya afya iko mbali na haifikiki kutokana na umbali na ukosefu wa usafiri au vitendea kazi.

“Kwa wale wanaofika kliniki ya afya, kituo kinaweza kukosa vifaa vya kutoa huduma za afya ya uzazi na uzazi zinazookoa maisha zinazohitajika, hivyo ndiyo sababu UNFPA tunaendelea kutoa mchango wetu katika kuhakikisha kuwa tunaboresha mazingira haya,” amesema Mark.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufanya mazungumzo na wadau wa afya wengine lengo likiwa ni kusaidiana na serikali kuboresha afya.

Amefafanua zaidi kuwa watu wengi wamekuwa wakifika mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma ya afya ya uzazi.

“Kartika kuboresha huduma za afya ndani ya mkoa wetu wa Dar es Salaam, Hospitali ya Amana itajengwa majengo nane ya gorofa ambapo mpango huu maandalizi ya ujenzi wake yanaendelea kufanyika.

“Mbali na hospitali ya Amana, maboresho mengi yataendelea katika maeneo mengi ya mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuboresha miundombinu na kujengwa hospitali za ghorofa kutokana na uhitaji huduma za afya ni kubwa,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles