31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Unaweza kuwa na kipaji kwa kujifunza, si kuzaliwa

CHRISTIAN BWAYA



IMEJENGEKA dhana kuwa watu huzaliwa na vipaji fulani. Jamii inaamini wapo watu waliozaliwa kuwa waimbaji maarufu, wachoraji, wabunifu, viongozi mashuhuri au wazungumzaji mahiri. Kwamba watu hawa wanaouwezo wa kufanya vitu ambavyo wengine hawana uwezo wa kuvifanya kwa urahisi, basi maana yake watu hao walizaliwa na vipaji vyao. Je, ndivyo unavyofikiri?

Kama ndivyo, basi hauko peke yako. Wapo watu wengi wanaofikiri uwezo wa mtu wa kufanya vitu kwa namna tofauti na wengine ni wa kuzaliwa zaidi kuliko kujifunza. Hatufundishwi kucheza mpira, kuimba, kuchora, kuandika, kuongoza na sifa nyinginezo. Kipaji, kwa mtazamo huu, kinachukuliwa kama sifa maalum anazozaliwa nazo mtu bila kulazimika kujifunza.

Hatahivyo, kuna mambo ya kutazama. Juzi nilikutana na rafiki yangu wa siku nyingi ambaye sikupata kuhisi angeweza kuwa mchoraji. Miaka 15 iliyopita nilikaa naye kwa muda mrefu na hakuonesha uwezo wowote wa kuchora hata ramani inayoeleweka. Leo hii nilishangazwa kuona anakipaji cha kuchora kwa umahiri wa hali ya juu. Kama nisingekuwa namfahamu, nisingeamini kwamba miaka kadhaa iliyopita, hakuwa na dalili zozote za kipaji cha kuchora.

Katika kutafakari uwezo huu mkubwa alionao rafiki yangu huyu, nimejiuliza alizaliwa nao? Kama uwezo huu ulikuwa ndani yake tangu miaka hiyo ya nyuma, mbona hakuonesha hata dalili zozote za kuchora? Kitu gani kimetokea na kumfanya awe mchoraji hodari?

Baada ya mazungumzo ya muda, ikaonekana mazingira yalimlazimisha kuwa na bidii ya kujifunza kuchora. Motisha ya kupenda kuchora ilitengenezwa na mahitaji ya kujiajiri aliyokuwa nayo miaka michache iliyopita. Baada ya kuona fursa katika sanaa, akaamua kuwa karibu na wachoraji wazuri. Jitihada za kujifunza namna ya kubuni mchoro, uwekaji wa kivuli, upakaji rangi na ujuzi mwingine wa kisanii, zilizaa matunda. Kila hatua aliyoonesha ilimpa motisha ya kuendelea kujifunza zaidi.

Tukiwa shule, namkumbuka mwenzetu mmoja ambaye tulizoea kumcheka kwa vile asivyojua kuimba. Kila alipoimba tulishindwa kuendelea. Sauti yake ilikuwa kichekesho na ilitufanya tumwone kama mtu anayelazimisha kuimba bila kipaji.  Hata hivyo, hakukata tamaa. Alifanya mazoezi ya kuimba kila mara, alijizuia aina fulani ya vinywaji,  na daima alionekana akisikiliza waimbaji maarufu wa nyimbo alizozipenda.

Baadayamudamfupi, alitokeakuwamwimbajimahirisanawanyimbohaposhuleni. Si tualiwezakuimba, lakinialikuwanauwezomkubwawakupigaainambalimbali za vyombo vya muziki kwa ustadi wa hali ya juu.

Ingawa ni kweli kwamba kipaji kinaweza kurithiriwa, inavyoonekana mazingira ndiyo yenye nafasi ya kukuza kipaji cha mtu. Inapotokea mazingira yakakutengenezea motisha ya kuonesha uwezo fulani mapema, upo uwezekano mkubwa wa kuongeza bidii ya kujifunza uwezo huo hata kama utafanya hivyo bila kujua.

Tunawatazama waigizaji maarufu kama watu waliozaliwa wakijua kuigiza, wachezaji maarufu kama watu waliozaliwa wakijua kucheza. Mara nyingi tunapowatazama watu hao, hatufikirii jitihada kubwa wanazozifanya nyuma ya pazia kufikia hapo wanapokuwa wamefikia.

Tunafikiri mtu anaweza kuzaliwa tu akaibuka na kipaji fulani bila kujifunza na kufanya jitihada za kujenga uwezo huo.

Ni kweli wapo watu wanaokuwa na uwezo wa kujifunza kufanya kitu fulani bila kutumia nguvu nyingi. Lakini hiyo haiondoi uwezekano wa mtu yeyote mwenye jitihada kujifunza na kuwa mahiri kwenye eneo hilo. Ipo nafasi muhimu ya mafunzo na jitihada katika kukuza kipaji cha mtu.

Ukweli ni kwamba kipaji kinategemea mazingira yanayokuzunguka. Ikiwa hapatakuwa na utayari na mahitaji ya kisaikolojia ya kukufanya ukaona sababu ya kujifunza kufanya kitu fulani, ni vigumu ukakifanya kitu hicho. Usipojisikia fahari ya kuwa mwimbaji maarufu, si rahisi uweke bidii kwenye uimbaji. Usipojisikia ufahari wa kuwa mchezaji maarufu, ni vigumu kupata muda wa kufanya mazoezi ya michezo. Kila kitu kinaanzia na msukumo unaojengeka ndani yako na kutengeneza hamasa ya kufanya kitu.

Ninachotaka kukisema ni kwamba ukiamua unaweza kuwa na kipaji chochote unachokitaka. Muhimu ni kudhamiria na kuchukua hatua za kufanya bidiii inayohitajika. Unaweza kuwa mchezaji maarufu, mwigizaji maarufu, mwimbaji maarufu na kila aina ya uwezo unaoufahamu ikiwa utaamua kwa dhati kuelekeza nguvu zako kwenye uwezo huo. Amka na jifunze uwezo huo kadri ya mahitaji yako. Ukidhamiria, kwa vyovyote utafanikiwa.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU) Simu: 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles