25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Unaweza kutumia nyakati ngumu kujitathmini

Na CHRISTIAN BWAYA

AKUMBUKA miaka ya nyuma kidogo nikiwa mwanafunzi kuna wakati nilihitaji kiasi fulani cha fedha. Ingawa sikuwa na ujasiri wa kumwambia mtu, hata mwenzangu niliyekuwa naishi naye chumba kimoja pale hosteli, ukweli nilikuwa naujua mwenyewe. Nilihitaji fedha, sikuwa na mahali pa kutegemea, lakini pia sikutaka kukopa.

Katika hali hiyo ya kukata tamaa kimya kimya nisijue nifanye nini kupata fedha nilijifunza jambo ambalo kama nisingepitia kipindi hicho pengine ingechukua muda mrefu kujifunza. Saa nyingine unaweza kujifunza mambo muhimu yatakayobadilisha maisha yako unapopita katika nyakati ngumu.

imejifunza shule ya kweli na muhimu katika maisha unaipata unapopitia katika tanuru la moto. Wakati wengine wakichukulia nyakati ngumu kama sehemu ya kujilaumu, kujishutumu, kuwashutumu wengine, unaweza kabisa kutumia nyakati ngumu kujitathmini, kuielewa hali yako, kuitazama kesho yako na mambo yakabadilika.

Nakumbuka nilitafuta mahali palipotulia uwanjani nikajilaza chini ya mti nisijue nifanye nini. Katika hali hiyo ya utulivu nilijiuliza maswali. Hivi nikiendelea kujiumiza kwa mawazo kwamba nilichokuwa nakihitaji hakipatikani kwa wakati huo, kuna chochote ninachoweza kukibadili? Kukata tamaa kungenisaidia namna gani? Wazo dogo kama hilo lilibadili hali yangu.

Nilijipa changamoto ya kuona tofauti. Nikaamua badala ya kuona vile mambo yalivyokuwa magumu, vile hali ilivyokuwa haiendi, bora niamini hali yangu si mbaya kihivyo. Kufikiri kwa namna hiyo kulifungua ufahamu wangu. Nikaanza kuona uwezekano katika ugumu uliokuwepo.

Kuna namna fulani imani ilijengeka ndani yangu. Nikaanza kusema maneno ya ujasiri. Nikaanza kutamka maneno ya matumaini. Kadiri nilivyotamka ndivyo ujasiri ulivyojengeka ndani yangu. Nikaanza kuona shida yangu inaondoka.

Nikaanza kuona juma linalofuata kuna jambo jema litatokea. Nikaanza kukumbuka mistari kadhaa kwenye biblia iliyojaza moyo wangu matumaini yasiyo ya kawaida. Nikajiona nikifanikisha kile nilichotaka kukifani- kisha. Kutokuwa na fedha wakati huo haikuwa tabu.

Nilijiona kama mtu mwenye fedha zitakazotatua tatizo nililokuwa nalo. Sikuwa na chembe ya wasiwasi. Kila kitu kilionekana kuwa mahali pale. Kadiri nilivyokuwa nalitazama juma linalofuata kama juma la tofauti, ndivyo nilivyoendelea kuwa na moyo uliochangamka.

Nikaanza kujitamkia kwa sauti kiasi cha fedha nitakachokipata juma linalofuata na namna nitakavyokitumia kumaliza shida yangu. Kumbuka sikuwa na mpango wowote utakaoniingizia fedha wakati huo.

Lakini ndani yangu nilijitazama kama mtu anayeenda kwenye mashine ya kutolea fedha na kuchukua kiasi cha fedha nilichokihitaji kumaliza uhitaji wangu. Halafu sikuwa na hata na chembe ya wasiwasi.

Jambo la kushangaza ni kwamba juma lililofuata bila kutegemea, nilitafutwa na mtu ambaye sikuwahi kuonana naye kabla, hatukuwa tukifahamiana, lakini alihitaji nimsaidie kazi fulani aliyoamini nilikuwa na utaalam nayo. Nilishangaa kwa sababu mazungumzo yetu yaliishia kuku- baliana malipo sawasawa na kiasi nilichokuwa nimekiona nikiwa nimejilaza chini ya mti, uwanjani.

Unaweza kuuita huo ni muujiza. Unaweza kusema ilitokea kwa ba- hati. Lakini baadaye nilikuja kujifunza namna unavyoweza kuuelekeza ufahamu wako ukakuletea kile unachokihitaji.

Nikajifunza kumbe kile unachokiingiza kwenye ufahamu wako, ukakiruhusu kijenge taswira halisi, kina nguvu ya kuongoza mustakabali wako. Ukiingiza kushindwa, uwezekano ni mkubwa, utaishia kushindwa. Ukiingiza kuweza, hakika utaishia

kuweza. Ukitafakari jambo hili unaweza kuona ni kama mchezo wa kuigiza. Unaweza kuhisi ni ile mizaha ya watu wanaojipa matumaini hewa yasiyo na uhalisia. Lakini mimi binafsi nimejifunza kuwa hicho unachoweza kukiona kama aina fulani ya mzaha, kina nguvu kubwa ya kufanya mambo yakatokea sawasawa na vile ufahamu wako ulivyokaa.

Nikirejea majadiliano yetu ya juma lililopita, ufahamu usioon- gozwa na utashi wako umebeba nguvu kubwa ya kukubalisha. Shida yetu naamini ni kushindwa kuuongoza ufahamu huu na badala yake tunajikuta tunaongozwa nao.

Lakini ninachojua ni kwamba ukiweza kuamuru sehemu ya ufahamu wako isiyoongozwa na utashi wako ikawa na ujumbe unaofanana na kile unachokitaka, jambo hilo unalotaka litokee hakika litatokea.

Huu si uchawi wala si mafundisho ya dini bali namna ya kutumia nguvu ambayo naamini Mwenyezi Mungu ameiweka ndani yetu. Uwezo wa kutumia nguvu hiyo uko mikononi mwako.

Kama ambavyo mimi nilikaa chini ya mti nikajiona nikipata nisichokuwa nacho, nikajiona nimepata nisichokuwanacho, nikaaminisha ufahamu wangu kuwa ninachokihitaji ninacho tayari hata kama katika uhalisia hakikuwepo, na wewe unaweza kuanza kufanya zoezi hili lenye muujiza wake.

Kwa mfano, badala ya kuona umasikini na kuruhusu mawazo ya umasikini yatawale maisha yako, anza kufikiri kama mtu asiye na shida ya fedha. Ufanye ufahamu wako uone hali njema unayotaka ikutokee. Ufanye ufahamu wako uone uhalisia wa kile unachokitarajia.

Ukiweza kuondoa mashaka na wasiwasi, moyo wako ukaamini kile unachokitarajia kitatokea, hakika utapata kilekile ulichotaka kitokee.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles