31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

UNAWEZA KUTENGENEZA BILIONI 2 KWA MIEZI MIWILI

Dawa za kulevya

NA LUQMAN MALOTO,

BRIAN O'Dea, raia wa Uingereza, alikuwa bilionea wa unga kabla hajaacha. Katika kitabu chake kinachoitwa ‘High: Confessions of a Pot Smuggler’, kilichotoka Aprili 11, 2006, anaeleza kuwa alifanikiwa kuifanya biashara hiyo kwa mafanikio kwa sababu haikuwa rahisi kumkamata.

O’Dea ambaye aliwahi kufungwa Marekani miaka 10, anaandika kuwa wakati fulani baada ya kutoka jela hakuwa na fedha, hivyo alikwenda Colombia na kujitambulisha kwenye genge la Sinaloa, linaloongozwa na ‘mtu mbaya’, Joaquin Guzman ‘El Chapo’ kuwa naye ni memba ila alikuwa jela.

Huko alipewa gram 50 tu za cocaine ambazo alipita nazo sehemu zote za ukaguzi lakini wakaguzi hawakugundua alibeba unga kwa sababu walimuona ameshika pakti ya sigara. Naye kuwapoteza aliifungua kabisa na kutoa sigara moja na kuvuta.

Kwamba unaona pakti la sigara, unafungua unakuta sigara zenyewe lakini ndani watu wabaya wamefunga mzigo kati ya gram 50 mpaka 100. O’Dea anasema baada ya kuuza gram hizo 50 Marekani, aliendelea kuzungusha cocaine ambazo ndani ya miezi miwili zilimfanya atengeneze dola moja milioni, Sh 2.23 bilioni kwa sarafu ya sasa.

Mtu anatoka jela kisha anaanzia mtaji wa gram 50 halafu kwa haraka ndani ya miezi miwili anafikisha utajiri wa Sh 2.23 bilioni, je, biashara hiyo nguvu yake ni kubwa kiasi gani?

UGUMU WA VITA

Vita ya dawa za kulevya ni sayansi. Wakili wa Mahakama Kuu Marekani, Erick Sterling ambaye ni mtafiti wa kesi za dawa za kulevya duniani, anasema kuwa biashara ya dawa za kulevya ni kesi ngumu kuliko kesi nyingine zote.

Sterling anasema: “Ugumu wa kwanza wa vita dhidi ya dawa za kulevya ni kuwa hakuna mlalamikaji. Kesi nyingine zote kuwa kuna walalamikaji. Hata mauaji, ndugu watalalamika ndugu yao kuuawa kisha uchunguzi utaanzia hapo.

“Dawa za kulevya hakuna chanzo cha kuziwezesha mamlaka za Serikali kuanza uchunguzi. Inatakiwa mamlaka zenyewe zianze uchunguzi bila uhakika, kwa kuanza kubahatisha kisha zimhisi mtu na kufuatilia nyendo zake mpaka mwisho.”

Sterling hapo anatuonesha kuwa ushindi wa vita dhidi ya dawa za kulevya ni mgumu kupatikana. Mpaka kumhisi halafu kumfuatilia na kujiridhisha ni mhusika kazi ni kubwa. Ndiyo maana nimesema vita ya dawa za kulevya haipaswi kutekelezwa kwa oparesheni.

Shushushu mstaafu wa Marekani, Howard Wooldrige, anasema kuwa ukitaka usifanikiwe katika mapambano dhidi ya wahalifu wa dawa za kulevya basi ujaribu kutumia njia za mkato.

Vema kutambua kuwa vita hii ni ngumu na inahitaji utulivu kuweza kufanikiwa. Wahusika wachunguzwe, wafuatiliwe na kuwakamata kisha kuwafikisha mahakamani wakiwa na mashitaka yenye nguvu.

Biashara ya unga inaendeshwa kiuharamia, kwa hiyo serikali nayo hupaswa kuiendesha vita kiuharamia ili kuwakamata wahalifu wenyewe. Kuwavizia na hata kuwazunguka kwa kununua watu kwenye makundi yao au kuwachomekea askari wenye kujifanya wana mtandao.

NYENZO SITA ZA MAPAMBANO

Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji mambo sita. 1. Ukweli 2. Uaminifu 3. Maarifa 4. Nyenzo 5. Ujasiri 6. Fedha.

Ukweli; iwe kweli kuwa dhamira ya mapambano ipo. Na iwe kweli utashi upo. Na iwe kweli watu wamejitoa kupambana bila kutazama sura ya mtu.

Uaminifu; lazima kuwe na uaminifu. Biashara ya unga inashawishi mno, fedha zipo nje nje. Anakamatwa mtu na mzigo wa Sh 10 bilioni. Hashindwi kutoa hata Sh bilioni 2 ili aachiwe huru na mzigo wake.

Maarifa; elimu ya kutosha kuhusu namna biashara ya dawa za kulevya inavyoendeshwa na jinsi ya kukabiliana nayo. Usipokuwa na watu wenye maarifa ya kutosha, biashara hii haitamalizwa nchini na duniani kote.

Nyenzo; vitendea kazi ni muhimu. Majasusi wa mataifa mengine huchomeka vifaa maalumu kwa siri kwenye nyumba, ofisi na magari ya watu wanaowahisi ni wauza dawa za kulevya ili kunasa siri zao. Vifaa vipo vya aina nyingi.

Ujasiri; bila ujasiri huwezi kuiweza vita hii. Watu wengine wanatisha lakini inatakiwa kuwakabili tu.

Fedha; mambo yote matano niliyobainisha hapo yanahudumiwa na fedha. Watu kuwa wakweli, waaminifu, wenye kutumia maarifa yao na majasiri kama wanalipwa vizuri. Fedha pia ndiyo hununua nyenzo. Lazima mtu apewe sababu ya kukataa hongo ya wauza unga. Akiwa na njaa atapokea rushwa.

Vita ya unga hutaka ukweli na isiendeshwe kwa ubaguzi. Marekani inaingia hasara kubwa leo kwa sababu miaka ya nyuma mapambano yao dhidi ya biashara ya dawa za kulevya ilibagua, ililenga Wamarekani weusi tu.

John Ehrlichman, ambaye alikuwa mshauri mkuu wa masuala ya sera wa Rais wa 37 wa Marekani, Richard Nixon, alifanya mahojiano miaka ya 1980 na mwandishi wa nchi hiyo, Dan Baum, akamweleza kuwa Nixon alipambana na Wamarekani weusi katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Nixon ndiye kiongozi wa kwanza kutangaza dawa za kulevya kuwa adui namba moja wa umma wa Wamarekani. Hata hivyo, pamoja na kutumia nguvu kubwa na fedha, vita hiyo imeendelea kushamiri.

Sababu ni ubaguzi, badala ya kushughulika na dawa za kulevya kiukweli, wewe unawalenga watu fulani. Matokeo yake, Wazungu walitumia mwanya huo kujitandaza na biashara hiyo na kuisababisha hasara kubwa Marekani.

Siyo huyo Nixon tu, idara ya kwanza ya kupambana na dawa za kulevya Marekani, iliundwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 na iliongozwa na mwanasiasa, vilevile mwanaharakati, Harry Anslinger ambaye aliwaandama Wamarekani weusi.

Anslinger kabla ya kuteuliwa na Rais wa 35 wa Marekani, John Kennedy mwaka 1961 kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Kudibiti Dawa za Kulevya (FBN), alishakuwa akitumiwa na Serikali kwenye mapambano hayo japo hayakuwa rasmi. Na mapambano yake aliwalenga Waafrika.

Kwa maneno yake, Anslinger alisema Wamarekani weusi ndiyo wanaoingiza dawa za kulevya Marekani, akasema kuwa fani za sanaa ambazo zinaundwa na Wamarekani weusi zimejaa mihadarati.

Huu ni muongozo kuwa kama kweli tunahitaji kushinda vita hii lazima ukweli na uaminifu uongoze mapambano haya. Wasibaguliwe watu. Kila anayehusika aingizwe kundini. Na wasiohusika wasionewe, watendewe haki.

Alama ya kwanza ya kushindwa vita hii ni kubagua, nimetoa mfano Marekani. Katika hili, mapambano ya sasa yameanza kusemwa kuwa na ubaguzi. Hii ni sumu. Haki itendeke.

MAHITAJI YA FEDHA

Bajeti ya Shirika la Ujasusi la kupambana na dawa za kulevya Marekani (DEA) ni Dola mbili bilioni, Sh 4.47 trilioni kwa mwaka. Bajeti ya jumla ambayo hupewa Ofis ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Marekani (ONDCP), ni dola 25 bilioni, Sh55.9 trilioni.

Bajeti nzima ya vita ya dawa za kulevya kwa mwaka 2016 Marekani ilifikia dola 30 bilioni, Sh670 trilioni. Fedha ambazo ni zaidi ya mara mbili ya bajeti ya Serikali ya Tanzania, kwa kipimo cha bajeti iliyopo.

Intelijensia ya Marekani ni kali sana na uwekezaji wao kifedha ni mkubwa lakini hali inazidi kuwa mbaya mno. Vita ya dawa za kulevya ina msisimko mkubwa kishetani. Kadiri unavyoipiga vita ndivyo inavyoshamiri.

Kuanzia wakati wa mdororo mkubwa kiuchumi (Great Depression) mwaka 1930 mpaka mwaka 1960, Marekani ilikuwa na kiwango cha wafungwa gerezani chini ya 150,000. Mwaka 1970, baada ya Rais wa 37 wa Marekani, Richard Nixon kutangaza kuwa adui namba wa nchi hiyo ni dawa za kulevya, hapohapo kasi ya wafungwa ikawa kubwa mpaka kufikia watu 250,000.

Watu zaidi ya 2.2 milioni wamefungwa Marekani, kati ya hao, asilimia 40 wanatokana na vita ya dawa za kulevya. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 5 ya watu wote duniani ni raia wa Marekani, takwimu pia zinabainisha kwamba asilimia 25 ya wafungwa wote duniani wapo Marekani.      

Takwimu zinaeleza kuwa asilimia 50 ya Wamarekani wote kwa namna moja au nyingine hutumia dawa haramu za kulevya kwa sababu mbalimbali.

Hiyo ndiyo laana ya unga, jinsi mapambano yalivyo makali, ndivyo na kuenea kwake kunakua kwa kasi kubwa. Rais wa 41 wa Marekani, George Bush (Bush baba), alipoingia madarakani aliwekeza fedha nyingi mno, akiwa ni Rais wa kwanza wa Marekani kufanya hivyo, lakini matokeo yake biashara ilishamiri.

Imeandaliwa na Luqman Maloto ambaye ni mchambuzi na mshauri wa siasa, jamii na sanaa. Tovuti yake ni www.luqmanmaloto.com ambayo ni maarufu kama Maandishi Genius.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles