30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Unavyoweza kusoma nchini Afrika Kusini

Chuo Kikuu cha Cape Town
Chuo Kikuu cha Cape Town

NA FARAJA MASINDE,

UKANDA wa Kusini mwa Afrika ni moja ya sehemu ambazo wanafunzi wengi wamekuwa wakipendelea kwenda kuchukua taaluma zao katika fani mbalimbali.

Ni kweli kwamba wengi wanapenda kusoma kwenye miji mikubwa kama, Johanesburg, Cape Town, Port Elizabeth, Pretoria na mingine mingi.

Hata hivyo changamoto huwa ni kwa namna gani wanaweza kumudu taratibu na gharama za kusoma nchini humo na hivyo kujikuta baadhi yao wakibadili mawazo ya kwenda kusoma.

Kama hivyo ndivyo basi makala haya huenda yakawa ni msaada mkubwa kwako ili uweze kutimiza ndoto zako nchini humo ambako kunatajwa kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi wa mataifa mbalimbali kwenda kusoma.

VYUO

Vyuo vya Afrika Kusini vimekuwa huru katika kuandaa mitaala yake na programu za mafunzo ambayo imekuwa na tija zaidi ikilinganishwa na ile ya serikali.

Jumla ya vyuo 23 vya umma vinapatikana nchini humo huku vyote vikitoa Shahada ambapo wanafunzi lukuki kutoka nje ya mipaka ya nchi hiyo huenda kuchukua taaluma zao kwenye vyuo hivyo.

Lakini tambua kuwa kuna aina tatu za vyuo ambavyo unaweza kuchukua Shahada yako nchini humo.

Vyuo vya Utamaduni – hivi hutoa mafunzo ya nadharia pekee, vyuo vya Teknolojia – hivi vinatoa mafunzo kwenye taaluma ya Stashahada na Shahada na vyuo mchanganyiko – ambavyo hivi vinatoa taaluma mbalimbali huku vikiwa na wanafunzi wa kada mbalimbali kutoka kila pembe ya dunia.

Nchini humo kuna vyuo vikuu 11 vinavyotoa taaluma ya Utamaduni, sita vya Teknolojia na sita vingine vikiwa vinatoa taaluma mchanganyiko.

GHARAMA ZA MASOMO

Kwa wanafunzi wa kimataifa wanaokwenda kuchukua taaluma zao nchini humo hulipa ada kati ya randi 30,000 mpaka 35,000 kwa kozi ambayo ni zaidi ya Sh milioni 4 za Tanzania, hata hivyo gharama hizo hutegemea na aina ya kozi pamoja na chuo husika.

Hata hivyo ili uweze kusajiliwa kama mwanafunzi wa moja ya vyuo nchini humo ni lazima uhakikishe kwamba unakuwa na kibali cha masomo kwa maana ya ‘Study Permit’ na hii hutegemea tu kama kozi yako inachukua zaidi ya miezi miwili.

Lakini vitu kama bima ya afya, taarifa za mwangalizi wako, barua kutoka chuo unachokwenda kusoma na uhakika wa kifedha ili kuhakikisha kuwa unamaliza masomo yako ni moja ya vitu muhimu ambavyo vimekuwa vikizingatiwa kwa mwanafunzi kusoma nchini humo.

MALAZI

Moja ya kitu mhimu ambacho kimekuwa kikitazamwa na wanafunzi wengi wa kimataifa ni mazingira bora ya kuishi pamoja na kupata mahitaji yote muhimu kama binadamu.

Ni jukumu la mwanafunzi kujitafutia mahala anapotaka kuishi ambapo kila mahala kuna gharama zake licha ya ukweli kuwa gharama za kuishi nchini humo ni nafuu kuliko za nchi kama Uingereza na Marekani.

Kuna gharama za mpaka randi 7,000 kwa mwezi kwenye nyumba ya vyumba vitatu vya kulala iliyoko nje kidogo ya mji huku bei ya chumba kimoja cha kulala kilichoko katikati ya mji ikiwa ni randi 4,500 kwa mwezi.

 USALAMA

Ni kweli kuwa Afrika Kusini imekuwa haina rekodi nzuri sana linapokuja suala la usalama, kwani imekuwa na kiwango kikubwa cha matukio ya ubaguzi na hata uvamizi hivyo ili kuwa salama kwa mwanafunzi huna budi kuzingatia dondoo hizi.

Epuka kutembea peke yako, beba simu yenye chaji muda wote, epuka kukatiza kwenye vichochoro usiku, usibebe fedha nyingi, wajulishe marafiki zako unapotaka kutoka.

Usikubali kupewa lifti au kinywaji na mtu usiye mfahamu na hakikisha unakuwa mwangalizi wa mali zako kwa kutazama mazingira yanayokuzunguka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles